Angela Msimbira OR-TAMISEMI

Serikali inakamilisha tathmini ya upembuzi yakinifu wa shule zote za msingi kupitia mradi wa kuboresha elimu ya awali na msingi Tanzania Bara (BOOST) ili kuandaa mpango endelevu wa uboreshaji wa elimu ya awali na msingi nchini .

Hayo yamesemwa leo Novemba 1, 2022 na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Davidi Silinde kwenye Mkutano wa Tisa wa Bunge, kikao cha kwanza kilichofanyika Jijini Dodoma

Akijibu swali la Joseph Kakunda Mbunge wa Sikonge aliyetaka kujua lini Serikali itajenga shule mpya ya msingi katika maeneo ya Mbirani, Makibo, Kiyombo na Tutuo Silinde amesema serikali imeamua kufanya tathmini hiyo kwa lengo la kubaini taarifa za eneo la shule ilipo, hali ya mazingira ya shule, umbali wa shule moja hadi nyingine na umbali wa shule na makazi ya watu ili kandaa mpango endelevu wa uboreshaji elimu nchini

Amesema katika mwaka wa fedha 2022/23 kupitia mradi wa Boost Serikali imetenga Shilingi bilioni 230 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya shule za msingi katika Halmashauri zote 184 ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge.