Na Mwandishi wetu – New York, Marekani

Serikali kupitia Wizara ya Afya, imewataka Wadau wa Sekta ya Afya kuimarisha ushirikiano ili kutatua changamoto zinazokabili eneo la rasilimali watu wa sekta ya afya.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, wakati akishiriki mjadala uliofanyika jijini New York, Marekani pembezoni mwa Mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa uliokuwa na kauli mbiu ya Ushirikiano kwa Matokeo na ulishirikisha viongozi wa ngazi za juu kutoka Serikalini, Sekta Binafsi, Asasi zisizo za Serikali kutoka mataifa mbalimbali.

Aidha, Waziri Ummy amewataka wadau hao kuzingatia dhana ya mpango-mmoja (one-plan) katika kuandaa na kutekeleza vipaumbele vya Mpango Mkakati wa tatu wa miaka mitano wa Rasilimali watu katika Sekta ya Afya (2020-2025) ili kufikia malengo ya mkakati huo.

Waziri Ummy amesema Tanzania ni moja ya nchi zenye uhaba mkubwa wa Watumishi wa Afya na kubainisha kuwa Serikali ya awamu ya sita chini ya Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka kipaumbele katika kutoa ajira za watumishi wa afya kwa lengo la kuboresha ubora wa huduma za afya.

Katika eneo la ushirikiano kwa matokeo, Waziri Ummy ametoa uzoefu wa Tanzania katika kutumia dhana ya kushirikisha wadau wa kisekta ili kuandaa, kutekeleza na kufanya ufuatiliaji wa pamoja katika mpango mkakati wa rasilimali watu.

“Tuna mafanikio yaliyopatikana kupitia ushirikiano huu ni pamoja na kugharamia mishahara kwa baadhi ya watumishi ambao Serikali imesaini mikataba na Hospitali zinazosimamiwa na Mashirika yasiyo ya kiserikali, kutoa ajira za muda na kusomesha watumishi” amesema Waziri Ummy Mwalimu.

Waziri Ummy ametoa rai kwa mataifa na serikali, mashirika ya kimataifa na nchi wahisani kuweka kipaumbele katika masuala ya rasilimali Watu wa sekta ya afya ili kufikia Azma ya afya kwa wote ifikapo mwaka 2030.