Na Zuena Msuya, Dar es Salaam

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema kuwa, Serikali inaendelea kuunga mkono juhudi za Sekta Binafsi katika kuhakikisha watanzania wote wanatumia nishati safi ya kupikia ili kutimiza azma ya Serikali ya kuhakikisha asilimia 80 ya watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia hadi kufikia mwaka 2034.

Hayo yalielezwa na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba wakati akizindua Umoja wa Wafanyabiashara wa Gesi za Mitungi ya Kupikia nchini (TZLPGA), Machi 15, 2023 jijini Dar es Salaam.

Mramba amewapongeza wafanyabiashara hao kwa kuanzisha umoja huo kwakuwa watakuwa wakiweka mipango ya pamoja kuhakikisha kuwa watanzania wote wanatumia nishati safi ya kupikia kwa vile wao ndiyo wadau wakubwa wa kusambaza gesi za mitungi kwa matumizi ya majumbani kwa ajili ya kupikia.

Amesema, Serikali imeweka wazi na mfumo rafiki wa uwekezaji nchini ili kila mwekezaji aweze kuwekeza katika sekta husika ili kutimiza azma ya Serikali inayotaka 80% ya watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia ndani ya kipindi cha miaka kumi.

“Tunaendelea na mpango mkakati wa miaka kumi, kwa kuweka sheria, kanuni na taratibu ili ikifika mwaka 2034, tuhakikishe Watanzania zaidi ya asilimia 80 wawe wanatumia nishati ya kupikia na mipango hiyo inaendelea vizuri sana” , amesema Mramba.

Amefafanua kuwa, takwimu zinaonyesha kuwa watu 32,000 wanafariki kila mwaka nchini Tanzania kutokana na kutumia nishati isiyo salama kwa kupikia, hivyo katika kukabiliana na changamoto hiyo Serikali inashirikiana na wadau kuhamasiha watanzania kutumia nishati safi ya kupikia kwa kuwawekea mifumo rahisi na rafiki.

Amewataka wafanyabiashara hao kutanua wigo wa biashara hiyo hadi vijijini na kwa gharama nafuu, ili kila mtanzania aweze kumudu gharama hizo.

Kwa upande wake Mwenyekiti Mteule wa umoja huo, Benoit Araman ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Oryx Energies Tanzania aliishukuru Serikali ya Awamu ya 6, inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mkazo katika matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Araman amesema wao kama wadau wakuu wa kusambaza gesi za mitungi majumbani hapa nchini wanaihakikishia Serikali kuwa wako tayari na wamejipanga kuhakikisha bidhaa hiyo inawafikia watanzania wote tena kwa gharama nafuu na kuboresha njia za upatikanaji wake.

Umoja huo unaundwa na Kampuni 6 zinazofanya biashara ya gesi za mitungi kwa matumizi ya majumbani ambazo ni CAMGAS, O-GAS, LAKE GAS, TAIFA GAS, ORYX GAS na MANJI GAS.

By Jamhuri