Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia

Serikali imewataka wadau wa sekta ya mawasiliano kuzitunza na kuziteketeza taka hatarishi zinazotokana na vifaa vya kielektroniki kwa sababu taka hizo hatarishi zimekuwa zikiongezeka hali inayopelekea hatari za kiafya kwa watumiaji wa bidhaa hizo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 20,2023 jijini Dar es Salaam, mara baada ya kufungua Warsha ya tano (5) ya Uhamasishaji wa Usimamizi Taka za Kielektroniki kwa Ukanda wa Afrika Mashariki(EACO), Waziri wa Habari,Teknolojia na Mawasiliano Nape Nnauye amesema kutokana na Teknolojia inavyozidi kukua na watu kununua vifaa hivyo imeonekana kuwa baada ya miaka kadhaa vifaa hivyo vikifa hutupwa holela hivyo kupitia warsha hiyo ya leo iangaliwe namna ya vifaa hivyo vikifa vikusanywe na kugeuzwa fursa ili visizagae mazingira.

Waziri wa Habari, Teknolojia na Mawasiliano Mhe. Nape Nnauye akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufungua Warsha ya tano (5) ya Uhamasishaji wa Usimamizi Taka za Kielektroniki kwa Ukanda wa Afrika Mashariki(EACO) leo Machi 20,2023 Jijini Dar es Salaam.

“Taka zinazotokana na vifaa vya elekroniki Sasa limekuwa tatizo na limeendelea kukua siku hadi siku watu Wanaweza wasione Kwa haraka matokeo yake kwani na watu wanatupa popote vifaa vingine vinaweza kuwa sumu na vikaleta madhara kwa Jamii hivyo kupitia Mkutano huu utakaofanyika kwa siku tatu utaleta suluhisho namna Bora ya kuzikusanya taka hizi na kuzigeuza fursa ili kudhibiti uharibifu wa Mazingira” amesema Waziri Nape.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt. Jabiri Bakari amesema mpaka Sasa hawana takwimu sahihi za hizo taka za kielektroniki lakini hivyo kuna baadhi ya Kampuni na taasisi chache zimeanza kukusanya taka hizo na watahakikisha wanashirikiana nao na kuwapatia utaratibu mzuri ili wasizifukie kwani zinaleta shida kimazingira.

Aidha Dkt.Bakari amezitaka taasisi mbalimbali ikiwemo Vyuo Vikuu kuzifanyia tafiti taka hizo hatarishi ilikuweza kuondokana natatizo lauharibifu wa mazingira.

Nae Katibu Mamlaka ya Mawasiliano Jumuiya Ukanda wa Afrika Mashariki EACO Dkt. Ally Simba amesema wameangalia kwa Ukanda huu wa Afrika Mashariki na ikaonekana kuwa taka za vifaa vya Kielektroniki zinakuwa kwa kasi zaidi kuliko taka nyingine hivyo hivyo lazima waweke mikakati ya pamoja kuweza kudhibiti taka hizo.

“Takwimu zinaonesha takribani watu Bilioni 7 Duniani wanatumia vifaa vya kielektoniki hivyo vinapokufa hawana hutupwa hivyo na kuzagaa hivyo kupitia warsha hii tumeona vifaa vya Kielektroniki si tatizo isipokuwa inatakiwa mikakati taka hizo kugeuzwa kuwa fursa wa kuzichakata kama taka nyingine”amesema Dkt Simba.

By Jamhuri