Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani

SERIKALI mkoani Pwani, imeagiza wawekezaji wanaohitaji kuwekeza mkoani humo wahakikishe wanahodhi maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji pamoja na kongani ,ili kuepuka kufanyiwa utapeli na kununua maeneo yaliyo kwenye migogoro ya ardhi.

Aidha halmashauri za mkoa huo zimetakiwa kupima maeneo ya uwekezaji ili kuzirahisishia taasisi wezeshi ikiwemo Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA),Shirika la Umeme (TANESCO), Mamlaka ya Maji Dar es Salaam na Pwani (DAWASA) na Shirika la maendeleo Petroleum (TPDC)ziweze kuweka mazingira wezeshi katika mipango yao.

Agizo hilo limetolewa na mkuu wa Mkoa wa Pwani, alhaj Abubakari Kunenge wakati alipokagua na kutembelea ujenzi wa mradi wa Kiwanda Cha Kinglion Steel kinachojishughulisha na utengenezaji wa bidhaa zitokokanazo na chuma,huko Zegereni, Kibaha.

Kunenge alieleza, hilo ni agizo la Serikali na ndio msimamo wa mkoa.

“Uwekezaji mkubwa kama huu unahitaji miundombinu yenye gharama,mfano barabara,maji,umeme wa kutosha,gesi ya kutosha, Kwahiyo tuna waambia wawekezaji wetu,vitu hivi ni gharama kubwa”

“Wawekezaji wetu si rahisi kufuata kila mwekezaji kumuwekea kuleta miundombinu haraka bila mpangilio ,licha ya kwamba Serikali inafanya jitihada kubwa chini ya Rais wetu Samia Suluhu Hassan kuendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji kila Kona ili kuvutia wawekezaji ndani na nje ya nchi.”alifafanua Kunenge.

Akielezea kuhusu kiwanda alisema kitakuwa ni moja ya viwanda vikubwa Mkoani Pwani na kikikamilika kitakuwa ni kikubwa Afrika Mashariki na Kati.

Akitoa taarifa ya mradi wa ujenzi huo, Arnold Christian Lyimo , meneja Kinglion Investment co.ltd ametaja changamoto wanayokabiliana nayo ni uhitaji wa barabara kiwango cha lami km 2 ambayo itasaidia kurahisha usafirishaji wa bidhaa kwenye eneo hilo.

Alisema, ujenzi utakapokamilika wanatarajia kuzalisha tani 300,000 kwa mwaka zinazotokana malighafi ya chuma .

Pamoja na hilo Lyimo alisema ,pia ujenzi ukikamilika watatoa ajira 400 za moja kwa moja na 5,000 zisizo rasmi .

Alieleza, ujenzi huo ulianza march 2022 na utakamilika April 2024 na utaanza uzalishaji Juni 2024 ambapo utagharimu Bilioni 163.

Meneja wa TARURA Mkoani Pwani,Leopold Runji alisema ,kwasasa wamekamilisha ujenzi wa barabara kuanzia Madafu-Misugusugu km 12 iliyogharimu bilioni 17.

Anasema ,kutokana na changamoto ya barabara kuelekea kiwanda Cha Kinglion wanatarajia kwa kuanza kujenga kwa kiwango cha changarawe kipande kitakachogharimu kiasi Cha sh.milioni 220.

By Jamhuri