Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameagiza kampuni zote zilizopewa kazi za upimaji wa viwanja kwenye Jiji la Dodoma na zimeshindwa kukamilisha kazi hiyo, ziwe zilikuwa na mikataba ama hazikuwa na mikataba zichukuliwe hatua kali za kisheria kutokana na Kampuni hizo kuzalisha migogoro ya ardhi.

Pia amegiza watafutwe na kukamatwa vibarua na mawakala wa Ardhi wote ambao wanatembea na nyaraka za Serikali na kuuza viwanja kwa niaba ya maofisa wa Jiji huku akiagiza baadhi yao kukamatwa na kuchunguzwa kutokana na kuendelea kuuza viwanja kwa njia haramu.

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo October 6,2023 kwenye kikao alichokiitisha ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma cha viongozi wa majiji ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya, Tanga na Dodoma ili kujadili migogoro ya ardhi iliyokithiri kwenye majiji hayo na kutafuta suluhisho.

“Tunatambua makampuni mengi hapa Dodoma ni ya watumishi wenyewe kama ambavyo imeelezwa kwenye ripoti Mkurugenzi alikuwa na kampuni mbili, Mhasibu wake ana kampuni yake na wanazitumia kupima maeneo, kwa hiyo ni miradi yao.”amesema

Amewaagiza Wakuu wa Mikoa wahakikishe kuwa Kamishna Msaidizi wa Mkoa, Maafisa Mipango Miji wa Majiji, Halmashauri na Manispaa hawana sababu ya kuchukua watumishi wa muda kufanya kazi ya upimaji bali wafanye wao ili kuepusha mianya ya rushwa.

“Bw. Justin Albert, Freddy Mathias, Elias na Magige watafutwe, wachunguzwe na vyombo vya dola kuhusu nyaraka za Serikali walizonazo, na wazirejeshe nyaraka za Serikali wanazozitumia vibaya kwa kuendelea kuuza viwanja maeneo ya Jiji ya Ukanda wa Kijani, Mkonze, Ndachi, Chinyika, Ng’ong’ona na Mkalama.” amesema