Serikali yazungumzia ongezeko la bei ya mahindi, mchele

Serikali imesema kuwa matokeo ya tathmini iliyofanywa katika kipindi cha mwezi Agosti 15 hadi na Septemba 15, mwaka huu yamebainisha ongezeko dogo katika baadhi ya bidhaa za vyakula hususan mchele, mahindi, na maharage.

Aidha, kupanda kwa bei za bidhaa hizo ni kutokana na uhaba wa mvua kwenye maeneo mengi katika msimu wa kilimo wa mwaka 2021/2022 uliosababisha kupungua kwa uzalishaji wa mazao hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri wa Uwekezaji,Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji amesema hayo kwenye mkutano wa kutoa taarifa ya mwenendo wa bei za bidhaa nchini kwa mwaka 2021/22 uliofanyika jijini Dar es Salaam

Amesema kuwa uzalishaji wa mahindi kwa mwaka 2020/21 ulikuwa tani 7,039,064 na mahitaji yalikuwa tani 5,978,257 hivyo nchi ilikuwa na ziada ya mahindi ya tani 1,060,807.

Waziri wa Uwekezaji,Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji akizungumza na waandishi wa habari katika kituo cha uwekezaji TIC leo wakati alipotangaza hali ya bei za bidhaa nchini.

Alisema kuwa mwaka 2021/2022 uzalishaji wa mahindi ulishuka kwa asilimia 7.1 hadi tani 6,537,203 na mahitaji yaliongezeka kwa asilimia 0.9 hadi 6,034,943. Hivyo, ziada ya mahindi ilipungua kwa asilimia 56.6 hadi tani 502,260.

Dkt Kijaji ameongeza kusema kuwa kwa mwaka 2020/21 uzalishaji waa mchele ulikuwa tani 2,686,829 wajati mahitaji yalikuwa tani 1,095,743 hivyo nchi ilikuwa na ziada ya mchele ya tani 1,591,089.

Aidha, kwa mwaka uliopita, uzalishaji wa mchele ulishuka kwa asilimia 30.9 hadi tani 1,856,731 na mahitaji yalikuwa tani 1,065,534. Hivyo, ziada ya mchele ilishuka kwa asilimia 50.3 hadi tani 791,198.

“Tafsiri ya takwimu hizi za uzalishaji wa bidhaa za vyakula ni kwamba chakula kipo cha kutosha ndani ya Taifa letu kama takwimu zilivyoonyesha, hivyo hatuna upungufu wa chakula na Serikali inaendelea kufuatilia upatikanaji wa bidhaa za vyakula kwenye masoko yote Nchini,”alisema Dkt Kijaji.

Aliongeza kusema kuwa uzalishaji wa saruji kwa mwaka 2021/2022 uzalishaji wa saruji umeongezeka kwa asilimia 0.5 hadi tani 6,531,000 wakati uzalishaji wa nondo kwa mwaka miaka hiyo hiyo ulikuwa tani 278,000; na kwa mwaka 2021/2022 uzalishaji wa nondo uliongezeka kwa asilimia 4.7 hadi tani 291,000.

Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali wakimsikiliza Waziri wa Uwekezaji,Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji alipozungumza nao leo.

Pia, uzalishaji wa bati kwa mwaka 2020/21 ulikuwa tani 108,000; na kwa mwaka 2021/2022 uzalishaji wa bati uliongezeka kwa asilimia 5.6 hadi tani 114,000.

“ Kiuchumi tunasema soko letu la vifaa vya ujenzi linakua na hii ni dalili njema kwenye uchumi wa mtu mmoja mmoja na Uchumi jumla wa Taifa letu,” aliongeza