Mfumo wa vyama vingi vya siasa hapa
nchini ulirejeshwa miongo miwili na nusu
iliyopita, katika safari hiyo kumekuwa na
malalamiko lakini pia maboresho ili kulinda
tunu za taifa na kudumisha mshikamano na
umoja wa kitaifa.
Agosti mwaka jana Ofisi ya Msajili wa
Vyama vya Siasa ilivitaka vyama vya siasa
na vya kiraia kuwasilisha mapendekezo
kuhusu mabadiliko ya sheria mpya ya
vyama vya siasa ndani ya wiki mbili ili
mchakato wake ukamilike kabla ya
Uchaguzi Mkuu wa 2020.
Sheria hiyo mpya ambayo inakuja kuifuta
Sheria ya Vyama vya Siasa Namba 5 ya
mwaka 1992, tunasema imecheleweshwa,
lakini pengine sasa ni wakati mwafaka wa
kuangalia masilahi mapana na kuiboresha.
Katika kipindi cha hivi karibuni kumekuwapo
wimbi la wanasiasa kuhama katika vyama
vyao na kujiunga Chama Cha Mapinduzi

(CCM), wakionyesha kuunga mkono jitihada
za maendeleo zinazofanywa na Rais Dk.
John Magufuli.
Sisi hatupingi wanasiasa kupendezwa na
sera, namna ya uongozi wa chama fulani na
kuamua kuunga mkono jitihada hizo,
isipokuwa tunataka kuona kodi za wananchi
hazichezewi kupitia mgongo wa
demokrasia.
Ni wakati sahihi sasa wadau kurudi na
kukaa mezani na kuliweka jambo hilo
kisheria. Mosi, uwekwe muda kikomo wa
mwanasiasa kuhama kutoka chama ‘A’ na
kujiunga chama ‘B’ na kuruhusiwa
kugombea.
Pili, sheria iweke bayana kwamba kupitia
Uchaguzi Mkuu, mgombea fulani
akichaguliwa, tuamini kwamba chama
anachokiwakilisha ndicho kimechaguliwa,
hivyo kunapotokea kuhama hakuna hasara
kubwa itakayopatikana, maana chama
kilichoondokewa na mbunge kitapewa
nafasi ya kujaza kiti hicho.
Lakini pia sheria hiyo mpya itazame ukomo
wa kukaa madarakani kwa viongozi wa
vyama vya siasa na adhabu kwa viongozi
wanaokiuka Katiba. Hiyo itaendana na
mfumo rasmi na Katiba ya nchi, ambapo

rais anachaguliwa kila baada ya miaka
mitano katika vipindi viwili, huyo anakuwa
amemaliza ngwe yake.
Tunafahamu kwamba vyama vya siasa
katika nchi yetu bado ni vichanga na hili
lilithibitishwa na Rais mstaafu wa Awamu ya
Nne, Jakaya Kikwete, akiwa jijini
Johannesburg nchini Afrika Kusini hivi
karibuni na kuwataka viongozi wa nchi za
Afrika wasivione vyama vya upinzani kama
maadui.
Kikwete alitoa mfano wa Tanzania kwamba
mfumo wa vyama vingi ulirejeshwa mwaka
1992, hivyo bado vinahitaji kulelewa ili vikue
na kutoa matokeo chanya ya kuiwajibisha
serikali iliyo madarakani kutekeleza wajibu
wake wa kuwaletea maendeleo wananchi.
Tunakubaliana na hoja ya Kikwete kwamba
viongozi wa nchi za Afrika wanapaswa
kuviangalia vyama vya upinzani kwa
mtazamo chanya, lengo la vyama hivi ni
kuleta msukumo wa maendeleo kwa
kuwapo jicho la pili.

Mwisho

Please follow and like us:
Pin Share