Na Byarugaba Innocent, JamhuriMedia, Kibaha

Wanafalsafa wengi wamesema kuhusu elimu; Wapo waliosema elimu ni funguo wa maisha, wengine wakaongeza elimu ni Maarifa, wengine pia wakanena elimu ni Bahari.

Mjadala wa elimu ni bahari ni mpana sana ukimaanisha utajiri mkubwa unaopatikana kwenye rasilimali maji ya bahari.

Vitabu vya dini pia havipo mbali kuhusu elimu, vinatanabaisha kuwa mwanafunzi aishike sana elimu, asimwache aende zake (Mithali 4:13).

Aidha, mwanamuziki Samba Mapangala kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo aliimba pia kuhusu elimu “Somesha mtoto shule apate elimu, atafaidika kwa maisha yake.

Kwa minajili na mawanda ya Elimu, si kwamba mtoto huyo msomi anayepata elimu ananufaika peke yake, atanufaisha dunia.

Akiwa daktari atatibu wagonjwa, akiwa mwalimu atafundisha wengine maarifa mengine, akiwa rubani atarusha ndege kusafirisha watu na mizigo, akiwa mhandisi atajenga, atasanifu, ataunda vitu mbalimbali.

Aidha, akiwa mwanahabari ataandika kuelimisha, kukosoa, kuhabarisha jamii, akiwa mchumi atashauri kuhusu uchumi ama akiwa mtaalam wa hali ya hewa atashauri kuhusu vimbunga na Elnino.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ametimiza hana deni kuhusu elimu, ametenda.

Ameboresha sekta ya elimu kwa kiasi kikubwa ndani ya siku 1,095 tu madarakani kuanzia shule za awali mpaka vyuo vikuu.

Amefuta ombwe la mafundi mchundo kwa kuanzisha vyuo vya VETA na sasa wanakwenda kuwa wanufaikaji wa Bodi ya mikopo ya elimu ya juu Tanzania kwa kujiunga na Vyuo vya kati. Hii inakwenda kuongeza wasomi nchini kwa kumaliza kabisa ukame wa mafundi sanifu kwenye sekta za uhandisi magari, umeme, ujenzi, maabara na kwingineko. Mama ameupiga mwingi!

Halmashauri ya Mji Kibaha ni mnufaika kindakindaki wa mkono wa mama kwenye sekta ya elimu.

Ameufungua kwelikweli. Mazingira ya kusomea na kujifunzia ni bomba.

Tangu Machi, 2021 wakati Samia anakabidhiwa mamlaka ya kuliongoza Taifa, wakati huo nchi ikiwa kwenye majonzi makubwa ya kifo cha Rais wa Awamu ya Tano Dkt. John Pombe Magufuli bajeti ya Idara ya Elimu awali na Msingi ikuwa shilingi 13,328,507,592.00 hata hivyo kwenye utekelezaji aliiongezeka kufikia shilingi 13,408,729,500.00 sawa na 106 asilimia.

Aidha, katika mwaka fedha 2022/2023 bajeti ya idara iliongezeka kufikia shilingi 14,943,905,000.00 na kwenye matumizi yakawa asilimia 100 kwa mantiki hiyo kila kilichopangwa kilitekelezwa. Dkt. Samia na Elimu damu damu.

Kwa Mwaka wa fedha 2023/2024 tayari kiasi cha fedha kiasi cha shilingi 9,284,215,306.00 sawa na asilimia 61 kimepokelewa na kutumika.

Katika kipindi cha Rais Samia, Halmashauri ya Mji Kibaha imejenga shule mbili mpya Kanesa na Amani zilizopo kwenye Kata za Kongowe na Mbwawa pamoja na samani zake kupitia mradi wa EP4R/BOOST kwa gharama ya shilingi 1,636,581,500.00 kwa nia ya kufikisha elimu jirani na jamii pamoja na kupunguza mwendo kwa watoto waliokuwa wakitembea zaidi ya Kilometa 10 kwenda kusaka elimu kwenye shule za jirani huku kiasi cha shilingi 2,100,000,000.00 kikitumika kujenga Madarasa 109 baada ya uandikishaji kuongezeka kutokana na elimu kutolewa bure nchini.


Aidha, jumla ya matundu ya vyoo 108 yamejengwa kwa gharama ya shilingi 194,000,000.00 na nyumba mbili za walimu zenye uwezo wa kukaa walimu wanne zikijengwa kwa gharama ya shilingi 110,000,000.00 na madawati 100 yakiongezwa kwa gharama ya shilingi 1,000,000.00. Hakika Mama ametazama kotekote walimu na wanafunzi, ngoma droo!

Rais Samia amepunguza manung’uniko kwa wadau wa sekta ya elimu. Walimu, Wanafunzi na Wazazi wanampa maua yake.

Walimu wakuu na Wakuu wa Shule wanapata posho ya madaraka ambapo kiasi cha shilingi 442,800,000.00 ndani ya miaka mitatu kimelipwa.

Aidha, shilingi 160,000,000.00 kimelipa stahiki za walimu uhamisho na malipo mengine ya kusafirisha mizigo kwa wastaafu huku shilingi 309,960,000.00 kikitumika kulipa stahiki za likizo.


Hamza Duluge amekiri kuwa, Wazazi hawachangishwi tena mia mia za mitihami ya kujipima shuleni na michango mingine kama zamani. Ni marufuku bila idhini na makubaliano ya kamati shule.

Katika uongozi wake wa miaka mitatu Dkt.Samia ameidhinisha shilingi 887,131,000.00 za kuchapa na kudurufu Mitihani kwa shule za Msingi pekee na kutoa kiasi kingine cha shilingi 138,556,000.00 za ruzuku za uendeshaji. Katika kuthamini mchango mkubwa unaofanywa na walimu jumla ya shilingi 34,893,657,000.00 zimetumika kwa kuwalipa mishahara kwa wakati walimu 1,005.

Mkuu wa Idara ya Elimu awali na Msingi wa Halmashauri ya Mji Kibaha Deograticious Mapunda ametoa rai kwa Watanzania kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais Samia kwani malengo yake ni kutengeneza Taifa la wasomi, walipa kodi, wabunifu ili kunyanyua Uchumi wa Taifa kama yalivyo mataifa mengine yaliyoendelea kwenye sekta ya elimu.

Aidha, Mapunda ameeleza kuwa maboresho haya yameongeza ari ya ufundishaji kwa walimu mwamko wa kujifunza kwa Watoto hivyo kuongeza ufaulu kutoka asilimia 94.6 Mwaka 2020 mpaka kufikia 95.3 mwaka, 2023.

KWA UPANDE WA ELIMU SEKONDARI

Rais Samia ndani ya siku 1,095 amejenga shule mbili mpya za Sekondari kupitia mradi wa SEQUIP ikiwemo Viziwaziwa na Shimbo Mkuza pamoja na maabara zake kwa gharama ya shilingi 1,120,998,425. 00 sayansi inasomwa kwa vitendo. SEQUIP pia imetoa shilingi 167,000,000.00 kukamilisha miundombinu mathalani nyumba za walimu, matundu ya vyoo na madarasa.

Msisitizo mkubwa ni Wanafunzi wa Tanzania kuongeza kasi kwenye masomo ya Sayansi huku akisisitiza sana wanafunzi wa kike.
Aidha, kiasi cha shilingi 832,400,000.00 kimetumika kujenga mabweni 5, Madarasa 12 na matundu ya vyoo 16 kwenye shule za Mwanalugali na Shule ya Wasichana Kibaha na kiasi cha shilingi 200,000,000.00 kikitumika kukarabati shule ya sekondari Tumbi.

Katika kipindi hiki pia Rais Samia ameidhinisha kiasi cha shilingi 2,445,926,132.00 kuongeza madarasa 122 kupitia Kapu la Mama, UVIKO-19, Serikali Kuu na Mfuko wa Jimbo ikiwa ni jitihada za kuhakikisha wanafunzi wanakaa kwenye uwiano sahihi.

Ndani ya Kipindi cha siku 1,095, kwa halmashauri ya Mji pekee kwenye divisheni ya elimu sekondari kiasi cha shilingi 29,362,738,856.00 kimetumika. Kando ya kujenga na kuimarisha miundombinu, posho ya madaraka, likizo, uhamisho na mishahara, elimu bure, chakula kwa shule za bweni na ruzuku za uendeshaji vimetolewa kwa wakati.

Akiwasilisha bajeti ya Mwaka wa fedha 2024/2025 Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba amesadifu mapinduzi makubwa yanayofanywa na Dkt. Samia kwenye sekta ya elimu kwa kutenga kiasi cha Bilioni 832.42 kwa ajili ya Bodi ya Mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu ili kuhakikisha wale wanaomaliza kidato cha sita wanaendelea kwenye vyuo vya kati na si tu ngazi ya shahada.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Mwambisi Joseph Simba amekiri kuwa Tanzania kielimu ipo kwenye mikono salama ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani manung’uniko mengi ameyatatua hivyo ametumia fursa hii kuwaomba walimu kuchapa kazi na ilete matokeo chanya.

Afisa Elimu Sekondari Halmashauri ya Mji Kibaha Isihaka Rashid amesema kuwa maboresho yaliyofanywa na Rais kwenye sekta ya elimu yameongeza ufaulu kutoka wastani wa asilimia 92.6 mwaka 2020 mpaka asilimia 93.4 mwaka 2023 kwa kidato cha nne huku kidato cha sita ufaulu ukiongezeka kutoka asilimia 99.8 mwaka 2020 mpaka kufikia 100 mwaka, 2023.


Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha Dkt. Rogers Shemwelekwa kando ya kumpongeza na kumshukuru kwa kazi nzuri alizofanya Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan kwa kipindi kifupi cha miaka mitatu tu, amesema kazi kubwa kwa walimu ni kumsaidia Mhe. Rais kufundisha kwa weledi, ubunifu na kujituma na kwamba malengo ya halmashauri ya Mji Kibaha ni kuishia ufaulu wa Daraja 1-3 kwa Sekondari na Daraja A kwa shule za Msingi.

Halmashauri ya Mji Kibaha ina jumla ya Shule 66 za serikali zikiwemo 20 za Sekondari na 46 za Msingi. Aidha, jumla ya wanafunzi ni 59,732 wavulana wakiwa 30,183 sawa na asilimia 49.9 na Wasichana wakiwa 29,949 sawa na asilimia 50.1