DAR ES SALAAM

Na Abbas Mwalimu

Wiki iliyopita makala hii ilichambua umuhimu wa Kiswahili katika nyanja tofauti tofauti. Leo tuendelee kwa kukichambua jinsi kilivyotumika pia kama lugha ya ukombozi katika nchi za Msumbiji, Zimbabwe na Afrika Kusini (wakati wa ubaguzi wa rangi), Uganda, Rwanda, Burundi, Afrika ya Kati na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). 

Utafiti

Kiswahili pia kinatumika kama lugha ya utafiti katika vyuo vikuu mbalimbali vya Afrika, Ulaya, Asia na Marekani.

Kutokana na nafasi hiyo, taasisi mbalimbali za kimataifa husaidia tafiti katika elimu ya Kiswahili. 

Hizi ni miongoni mwa sababu zilizofanya Sekretarieti ya Umoja wa Afrika (AU) kukichagua Kiswahili kama lugha yake rasmi ya kazi (Adebayo na wenzake, 2010:65).

Tunapozungumzia utaifa na demokrasia leo hii katika Afrika tunapaswa kufahamu kuwa msingi wake ni lugha ya Kiswahili.

Katika kuthibitisha hili Muthwii na Kioko (2004) wameandika:

Lugha ni chombo muhimu katika kuhanikiza utaifa. 

Kwa msingi huo Kiswahili kina umuhimu mkubwa katika kuanzishwa kwa demokrasia ya kweli na usawa nchini Tanzania na Afrika kwa ujumla.

Mafanikio mahususi

Ongezeko la matumizi ya Kiswahili katika nchi mbalimbali za Afrika na duniani kwa ujumla kunatoa ishara ya kukua na kuimarika kwa lugha hii. 

Ushawishi wa Kiswahili katika majeshi ya Rwanda, Burundi, Uganda na DRC kunaonyesha jinsi ambavyo Kiswahili kinabeba ujumbe wa amani.

Zipo sababu kadhaa zinazoashiria mafanikio haya ya kukua kwa Kiswahili zikiwamo nchi ya Afrika Kusini kuanza kukitumia Kiswahili katika mitaala ya shule zake nchini humo katika ngazi mbalimbali. 

Kujiunga kwa nchi za Sudan Kusini na DRC katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kunaifanya lugha ya Kiswahili kuwa na nafasi kubwa ya ushawishi Afrika.

Mbali na hilo, kuwapo kwa idhaa za Kiswahili za mataifa kama Ufaransa (RFI), Marekani (VoA Kiswahili), Uingereza (BBC Swahili), Ujerumani (DW Kiswahili), China (CRI), Japan (Radio Japan Kiswahili) sambamba na redio ya UN) inayorusha matangazo kwa lugha ya Kiswahili kunaongeza kupanuka kwake. 

Mbali na nchi hizo na UN, nchi ya Urusi ina vyuo vikuu vitatu vinavyofundisha Kiswahili.

Tukiwa katika Ajenda 2063 ya AU ambayo ni mpango mkakati wa kuibadili Afrika katika miaka 50 ijayo na kuleta maendeleo endelevu, kuna haja ya kujenga misingi imara ya kukitumia Kiswahili kama nyenzo ya kupeleka ushawishi kwenye utendaji wake.

Bara la Afrika linaongozwa na dira isemayo Afrika iliyofungamana, yenye maendeleo na amani inayoendeshwa na wananchi wake na inayowakilisha kani isiyosimama katika nyanja za kimataifa. Kumbe kuna haja ya kuathiri wananchi wengi wa nchi za Afrika watumie Kiswahili kama lugha ya mawasiliano. Tunaanzia wapi? Hilo ndilo suala la msingi lakini naamini papo pa kuanzia. Tunahitaji kuanza na haya:

Kiswahili kiwe nyenzo ya 

kufikia malengo ya nchi

Kama nilivyosema awali kuwa Kiswahili kinaweza kutumika kama nyenzo ya ushawishi ambayo kwa lugha ya Kiingereza huitwa ‘soft power’, yaani  nguvu isiyo ya shuruti, ni kwa vipi?

Joseph Nye ameifafanua nguvu hii isiyo na shuruti kwa kusema kwa lugha ya Kiingereza kama ifuatavyo:

“Soft power is the ability to set the agenda in world politics through persuasion, enticing and attracting others through the force of one’s beliefs, values and ideas, and not through military or economic coercion (Nye, 1990:176).”

Kwa tafsiri yangu: “Nguvu isiyo na shuruti ni uwezo wa kujenga ajenda/hoja katika siasa za dunia kupitia ushawishi na kuwavutia wengine kupitia nguvu ya imani ya mtu, misingi na mawazo, na si kupitia majeshi au vikwazo kiuchumi.”

Kwa mantiki hiyo, tunaweza kushawishi nchi za Afrika zote zikatumia Kiswahili kama lugha ya mawasiliano katika nchi zao kama Tanzania itakuwa na mkakati madhubuti wa kuitumia lugha hii kufikia malengo.

Kama Tanzania iliweza kujenga hoja za kufanya kuwapo mabadiliko ya ibara ya 25 ya Sheria ya Kimamlaka ya Afrika (African Union Constitutive Act)  kulikosababisha kuondolewa kwa maneno ‘working languages’ na kuwekwa maneno ‘official languages’ kama ilivyoelekeza ibara ya 11, sheria ndogo ya mabadiliko katika Mkataba wa Kimamlaka wa Afrika yaani ‘Protocol on Amendments to the Constitutive Act of the African Union’ basi Tanzania inaweza kujipanga kukifanya Kiswahili iwe lugha ya kila taifa la Afrika.

Kwa kuanzia, Tanzania inaweza kuanzia kwa mabalozi waliopo nchini wanaowakilisha nchi zao hapa Tanzania.

Serikali inaweza kuandaa utaratibu wa kuhakikisha mabalozi wote wa nchi za kigeni wanapatiwa mafunzo ya Kiswahili katika Chuo cha Diplomasia (CFR) kilicho chini ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Kwa nini Chuo cha Diplomasia?

Kwa sababu CFR si chuo tu bali ni kituo chenye hadhi ya kibalozi kwa mujibu wa Sheria namba 5 ya mwaka 1986 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayohusu Upendeleo na Kinga za Mabalozi kama ilivyotoholewa kutoka katika Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961 na ule wa 1963 inayohusu Uhusiano wa Kidiplomasia na Kikonseli. Hivyo, chuo hicho kinakidhi kufundisha Kiswahili kwa mabalozi kwa sababu ya kuwa na hadhi ya kibalozi.

Pili, CFR ni sehemu ya Urithi wa Ukombozi wa Afrika inayotambuliwa na AU kwa sababu kabla ya makubaliano ya nchi za Msumbiji na Tanzania Januari 13, 1978 awali kilitumika kama Taasisi ya Elimu ya Juu ya Wapigania Uhuru wa Kusini mwa Afrika, hivyo kwa hadhi na historia ni sehemu muhimu na nzuri ya kuwafundisha mabalozi Kiswahili. 

Mbali na hilo, Tanzania inahitaji kujenga vituo vya kufundisha lugha ya Kiswahili katika nchi mkakati kama Nigeria, Misri, Senegal, DRC na Afrika Kusini na vitasaidia kueneza na kusambaza lugha hiyo katika nchi hizo na jirani.

Balozi zote za Tanzania  zinaweza kuwekewa kiunganishi (link) maalumu kwa wageni kujifunza Kiswahili katika tovuti za Balozi na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ili kuwavutia wageni kuijua luga hiyo.

Jingine la kufanyika ni kuwa na tamasha kubwa Kiswahili Afrika litakalokuwa likifanyika hapa Tanzania kila Julai 7 ya kila mwaka. 

Hili linawezekana kwa sababu tayari AU imeazimia kujenga Kituo Kikuu cha Urithi wa Ukombozi Afrika hivyo tunaweza kupenyeza ushawishi wetu kukifanya Kiswahili iwe lugha ya Waafrika wote.

Sambamba na hilo, kutokana na uwepo wa ujenzi wa kituo hicho, Tanzania inaweza kujenga kituo cha utafiti (research centre) ambacho licha ya kufanya katika masuala mbalimbali ya kisera Afrika, kitakuwa kikifanya utafiti wa lugha mbalimbali za Afrika ili kukipa Kiswahili misamiati mingi zaidi kutoka katika lugha hizo, hivyo kuongeza ushawishi zaidi na kuifanya ikubalike Afrika nzima.

Ninaamini ili kufikia dira ya Afrika mwaka 2063, Kiswahili ndiyo kiunganishi pekee ambacho ni fahari ya Waafrika. 

Ni moja ya vielelezo vya kujitawala. Aidha, kwa kiasi kikubwa ni lugha ya maendeleo ya mwafrika. 

Hivyo, mikakati madhubuti inahitajika kukifanya Kiswahili kitumike Afrika nzima nasi kama nchi tunufaike kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Mwandishi wa makala hii ni mchambuzi wa masuala ya siasa na diplomasia.

+255 719 258 484

By Jamhuri