Na Mwandiahi Wetu, JamhuriMedia, Dodooma

Ikiwa leo tarehe 05.06.2024 ni maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ambapo Kitaifa yamefanyika Jijini Dodoma, Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) imebainisha mchango mkubwa wa wadudu mbalimbali akiwemo nyuki katika Mazingira.

Akitoa elimu ya wadudu kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi NALOPA waliotembelea Makao Makuu ya TAWIRI Mtafiti Alphoncinah Mponzi amesema, wadudu wana mchamgo mkubwa katika mazingira ambapo wanasaidia uchavushaji wa mimea kwa zaidi ya asilimia 80.

“Nyuki ni mchavushaji mkuu wa kuendeleza uwepo wa mimea mbalimbali katika uhifadhi” ameeleza Mtafiti Mponzi

Aidha, Mtafiti Mponzi amesema mbali na uchavushaji wadudu wanasaidia uozeshaji wa taka na usafishaji wa mazingira pamoja na uoteshaji wa mbegu mbalimbali ambapo amebainisha mdudu (Dung beetle) anasaidia utawanyaji na uoteshaji mbegu mwituni, umeng’enyaji virutubisho vya udongo hasa vinyesi vya wanyama,(decomposition) na uongezaji mbolea kwenye udongo (soil fertilization) hivyo kufanya hivi husaidia kuwezesha makazi ya wanyama wengine.

Vilevile, alieleza kuwa uwepo wa wadudu katika uhifadhi kunasaida mzunguko wa chakula (food chain) ambapo kuna wanyama wadogo na ndege wanaotegemea wadudu kwa asilimia kubwa kama chakula chao akiwemo mnyama mhanga (Aardvark) na wanyama hawa huliwa na wanyama wengine.

Naye, Mwalimu Charles Mollel kutoka shule ya Msingi NALOPA ameishukuru TAWIRI kuanza kutoa elimu ya wadudu na nyuki kwa wanafunzi wa Darasa la Saba wa shule hiyo ambayo ina Mkakati wa kuhakikisha wanafunzi wanajifunza kwa vitendo zaidi.

Muhimu,✍️ mazingira ni pamoja na mimea ambapo kwa mujibu wa tafiti uchavushaji wa mimea mbalimbali unafanywa na wadudu kwa asilimia 80.