Kikosi cha klabu ya Simba usiku wa kuamkia leo kimeondoka kuelekea nchini Ivory Coast kwa ajili ya mchezo wa ligi ya mabingwa Afrika kundi B dhidi ya Asec Mimosas utakaochezwa Ijumaa ya Februari 23, 2024.

Simba wamesafiri na wachezaji 23, huku eneo la magolikipa wakiwa ni Aishi Manula, Hussein Abel na Ally Salim, Ayoub Lakred akiachwa Dar, jambo lililoibua gumzo kwa mashabiki wakihoji kwanini aachwe licha ya kuanza na kufanya vizuri kwenye mechi kadhaa za ligi kuu.

Afisa habari wa Simba, Ahmed Ally amesema Ayoub ameachwa kwa sababu ya kuwa na kadi tatu za njano ambazo zinamzuia kucheza mchezo huo, huku akiwataja nahodha John Bocco na Willy Onana kuachwa kwa sababu ya majeraha.

Aidha Ahmed amesema mchezo huo utakuwa mgumu sana kwa sababu licha ya kuwa wanacheza ugenini, lakini Asec ni timu bora na ndiyo inayoongoza kundi mpaka sasa hivyo watacheza bila presha na itakuwa ngumu kwao kufanya makosa yatakayowapa nafasi Simba ya kupachika mabao.

Simba wanashika nafasi ya pili katika kundi B wakiongozwa na Asec Mimosas wenye pointi 10, kwenye michuano ya ligi ya mabingwa Afrika.

By Jamhuri