Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la  Kibakwe, Mhe.George Simbachawene amewasihi wanafunzi kusoma kwa bidii na kuacha kujidanganya kuwa elimu kwa sasa haina umuhimu kwa kuwa hata waliosoma wamekosa ajira na wapo mtaani.

Mhe. Simbachawene ametoa nasaha hizo wakati wa mahafali ya 19 kwa wanafunzi wa  kidato cha nne  katika shule ya Sekondari ya Rudi iliyopo katika Kata ya Rudi, Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma.

Ameongeza kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amelenga kuboresha elimu na kuifanya elimu ya kidato cha nne  kuwa ya lazima na sio hiyari na hivyo, wananchi wa jimbo la Kibakwe wananufaika pia na maono hayo.

“Ninawaomba wananchi wote wa Jimbo la Kibakwe kupitia kwenu ninyi wazazi wa watoto hawa wanaofanya mahafali yao leo, kutambua kuwa mtu aliyemaliza kidato cha nne ana uwezo mkubwa wa kuchambua mambo kisayansi ukilinganisha na yule wa darasa la saba. Hivyo,

Elimu ni muhimu kwa kuwa inaongeza uwezo wa kufikiri na kupanua uelewa wa namna bora ya kupambana na changamoto” alisisitiza.

Aidha, amewataka wazazi kushirikiana na walimu katika kulea vijana hao wakati wote wanapokuwa shuleni kwa kuwa takwimu zinaonesha ni wanafunzi 64 tu kati ya wanafunzi 174 walioanza kidato cha nne mwaka 2020  ndio wamefanikiwa kumaliza kidato cha nne.

Kufuatia hatua hiyo Mhe.Simbachawene amewataka wazazi kuwahimiza watoto wao kutambua umuhimu wa elimu ili kuwa na jamii yenye uelewa kwa faida ya wananchi wa Kata  ya Rudi na Taifa kwa jumla.

Awali, Mkuu wa shule hiyo ya Rudi, Happy Mulio amesema licha ya shule hiyo kufanya vizuri lakini imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kutokuwa na maji ya uhakika pamoja na hosteli kwa wanafunzi wa kike hali inayowapelekea wanafunzi hao kukaa mtaani ambapo wamekuwa wakikumbana na changamoto ikiwemo kupata ujauzito.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kibakwe , Mhe. George Simbachawene akizungumza na wanafunzi na wazazi wa wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne  kwenye mahafali ya 19 ya Shule ya Sekondari ya Rudi iliyopo katika Kata ya Rudi katika Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma 
Sehemu ya Wazazi wa wanafunzi wa kidato cha nne  wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (hayupo pichani) wakati mahafali ya 19 ya Shule ya Sekondari ya Rudi iliyopo katika Kata ya Rudi katika Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma 
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akikabidhi zawadi kwa mmoja wa wahitimu waliofanya vizuri katika masomo wakati wa mahafali ya 19 ya shule ya Sekondari ya Rudi
………………………