Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema serikali yake inaendelea kulinda urithi wa hifadhi ya kimataifa ya Mji Mkongwe kwa kuzingatia kanuni na taratibu zilizowekwa.

Dk Mwinyi amesema hayo Ikulu, Zanzibar jana alipokutana na ujumbe kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kujadili kuhusu utunzwaji wa hifadhi ya kimataifa ya Mji Mkongwe.

Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imechukua hatua kutunza urithi wa Mji Mkongwe ikiwa ni pamoja na kuondoa maegesho ya vyombo vya moto kwenye maeneo yote ya Mji Mkongwe ili kuenzi na kuufanya uendelee kuwa kivutio mashuhuri cha watalii.

Dk Mwinyi amesema katika kutekeleza hatua hiyo, serikali imeamua kujenga maegesho ya vyombo vya moto eneo la darajani ikiwa ni njia mbadala ya kuondosha msongamano katika eneo la Mji Mkongwe.

Pia ameeleza mikakati ya serikali kushirikisha sekta binafsi katika kulinda urithi huo kwa kukarabati majengo chakavu kwa mujibu wa kanuni na taratibu bila kuharibu urithi wake na kuyarudisha katika uhalisia wake.

Amesema SMZ kwa kushirikiana na Serikali ya Oman wanaendelea na kusimamia ujenzi wa majengo ya Beit Al Ajaib na People’s Palace ambayo ni alama inayoitambulisha Zanzibar duniani kote.

By Jamhuri