DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu

Timu ya taifa ya soka ya wanawake ya Tanzania, Twiga Stars, imetwaa ubingwa wa Michuano ya Shirikisho la Vyama vya Soka Kusini mwa Afrika (COSAFA), baada ya kuichapa Malawi 1-0 kwenye mchezo wa fainali uliofanyika katika Uwanja wa Nelson Mandela, Port Elizabeth, Afrika Kusini Jumamosi iliyopita.

Twiga wamekwenda Afrika Kusini kushiriki michuano hiyo kama wageni waalikwa na kuwaduwaza wenyeji wao kwa kutwaa ubvingwa huo, hivyo kuwafanya akina dada wa Tanzania kukamata mataji yote yanayoandaliwa na COSAFA kwa upande wa wanawake.

Mataji hayo ni ya michuano ya COSAFA chini ya miaka 17, chini ya miaka 20 na sasa soka la wakubwa.

Timu hiyo imara ambayo sasa ina uzoefu chini ya Kocha Bakari Shime, imewaduwaza Malawi waliokuwa wakicheza fainali kwa mara ya kwanza, kwa kuwafunga bao moja katika dakika ya 64; ushindi waliostahili baada ya kuwadhibiti Wanyasa na kumiliki mpira kwa muda mrefu wa mchezo.

Bao hilo limefungwa na Enekia Lunyamila aliyepokea mpira mrefu uliowahadaa mabeki na kipa wa Malawi, kisha kuuweka wavuni.

Enekia ni mchezaji wa Alliance ya Mwanza anayetarajiwa kwenda kucheza soka la kulipwa nchini Morocco.

Zambia, waliotolewa na Twiga Stars kwa mikwaju ya penalti katika mchezo wa nusu fainali, wameshika nafasi ya tatu kwa kuwafunga Afrika Kusini; hivyo kuwaondoa mikono mitupu wenyeji hao kwa mara ya kwanza katika historia yao.

Mchezo huo uliamuliwa kwa mikwaju ya penalti 4-3 baada ya kumalizika kwa sare ya 1-1.

Kana kwamba haitoshi, nyota wa Tanzania na nahodha wa Twiga Stars, Amina Bilali, amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa michuano hiyo.

Kwa upande mwingine, wadogo zao, timu ya soka ya wanawake chini ya miaka 20, Tanzanite, wamefanikiwa kuingia raundi ya tatu ya michuano ya kuwania tiketi ya Fainali za Kombe la Dunia baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Eritrea katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, siku hiyo hiyo.

Mabao ya Tanzanite yamefungwa na Irene Kisisa na Protas Mbunda, na kufanya ushindi kuwa wa jumla ya mabao 5-0, kwa kuwa katika mchezo wa awali, walishinda 3-0 jijini Asmara, Eritrea, Septemba 25, mwaka huu.

Sasa Tanzanite watamenyana na Burundi katika mfululizo wa michuano ya kuwania tiketi ya fainali zinazotarajiwa kufanyika Costa Rica, Agosti mwakani.

370 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!