Mkurugenzi MOI amfurahisha Majaliwa

LINDI

Na Aziza Nangwa

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), Dk. Respicious Boniface, kwa kuwasogezea huduma za kibingwa wakazi wa mikoa ya kusini.

Akizungumza katika ziara yake mkoani Lindi alikotembelea Hospitali ya St. Walburg’s Nyangao, Majaliwa amesema sasa wananchi wa Lindi wanaitegemea hospitali hiyo badala ya kufuata huduma za matibabu ya mifupa Dar es Salaam.

“Wewe mkurugenzi, ninakushukuru sana. Wewe na timu yako, kwa kuona umuhimu wa kuja Nyangao na kushirikiana na madaktari wa hapa kutoa huduma za kibingwa.

“Ninawapongeza kwa maandalizi mazuri na kazi nzuri. Hata sisi tunaitegemea hospitali hii. Wewe, tutaonana Dar es Salaam,” amesema Majaliwa, akimuahidi Dk. Boniface kukutana naye Dar es Salaam.

MOI, kwa mujibu wa Waziri Mkuu, imekuwa kiungo na mfano wa kuigwa kwa kujenga ushirikiano mzuri na kusambaza matibabu ya mifupa nje ya Dar es Salaam, na kwamba serikali ipo tayari kusaidia kama kuna changamoto zozote.

Ametoa wito kwa hospitali hiyo kuendelea kuwahudumia wagonjwa ili lengo la kuboresha huduma za afya wilayani lifikiwe.

“Nimefurahishwa sana na huduma zenu. Sasa hakikisheni mnaondoa msongamano wa wagonjwa hospitalini hapa, japokuwa kila mtu anatumia muda kujieleza; mnatakiwa kuzingatia hilo ili kuondoa malalamiko,” anasema Majaliwa. 

Anasema pamoja na changamoto zinazoikabili MOI na Hospitali ya Nyangao, bado wataalamu hawa wamejitahidi kutoa huduma bora kwa uaminifu, ukarimu na upendo kwa wagonjwa na ndiyo maana watu wengi wanakwenda kutibiwa hapo.  

Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Lindi, Bruno Ngonyani, anasema amefurahishwa na ujio wa waziri mkuu hospitalini hapo.

“Ujio huu unathibitisha uhusiano mzuri uliopo kati ya serikali na taasisi za dini. Hili ni jema, kwa kuwa linatoa fursa kwa serikali kujionea upungufu uliopo hospitalini hapa na kusaidia,” anasema Askofu Ngonyani.

Anasema: “Waziri Mkuu, hapa tuna madaktari ‘interns’ (wanafunzi). Tunaomba muwaangalie sana kwani hawa wanasaidia kupunguza kazi na msongamano wa wagonjwa wanaokuja kutibiwa hapa,” anasema Askofu Ngonyani. 

Anasema uwepo wa Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk. Boniface pamoja na ujio wa waziri mkuu katika hospitali hiyo ni ishara kuwa huduma zataboreka katika hospitali hiyo.

Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Masanja Kasoga, anasema kitendo cha waziri mkuu kutembelea hospitali hiyo na kumpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, kumewapa uhakika wa kudumu kwa uhusiano na utoaji wa matibababu ya kibingwa katika Hospitali ya St. Walburg’s Nyangao. 

“Uhusiano huu ni kusogeza huduma za kibingwa za matibabu ya mifupa kwa watu wa kusini, na sasa waziri mkuu ameahidi kuendelea kutusaidia wataalamu na vifaa vya matibabu ya mifupa. Tunashukuru sana,” anasema Dk. Kasoga.

Anasema kwa sasa wana mpango wa kuongeza huduma za matibabu ya ubongo na mishipa ya fahamu ili kuwasaidia wagonjwa kutosafiri umbali mrefu hadi Muhimbili kufuata huduma hizo.

Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk. Respicious Boniface, anasema taasisi kusogezwa kwa huduma kusini kunalenga kuwaondolea wananchi gharama kubwa ya kusafirisha wagonjwa hadi Dar es Salaam.

“Tumeleta huduma hii huku ili kutanua wigo wa matibabu ya kibingwa ukanda wa kusini. Kila baada ya wiki mbili, madaktari wetu bingwa huja Nyangao na Ndanda kusaidiana na madaktari wa hospitali hizo kutoa huduma kwa wananchi,” anasema Dk. Boniface.

Dk. Boniface anaongeza: “Leo (Oktoba 5, 2021), tumeshuhudia kwa jinsi gani serikali kupitia waziri mkuu, wanavyothamini huduma zetu za kibingwa tunazozitoa katika Hospitali ya Nyangao.

“Kama Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, nimefarijika sana kwani nilipata bahati hata ya kumweleza waziri mkuu kwamba huduma tunazozitoa hapa ni kwa ajili ya kupunguza wimbi la wagonjwa wanaotoka mikoa ya kusini.”

Anasema pia amemweleza changamoto na matarajio yao katika kutanua huduma kwenye hospitali hiyo kwa kuwapeleka wataalamu wa ubongo na mishipa ya fahamu. 

Dk. Boniface ameishukuru serikali kwa kushirikiana nao katika kuboresha huduma za kibingwa ili ziwe endelevu.