Bei yake kwa Sasa Yatajwa ni Mara 10 Zaidi ya Tanzanite

Na Wizara ya Madini – Bangkok

Imeelezwa kuwa Madini ya Vito aina ya Spinel yanayochimbwa Mahenge Tanzania ni miongoni mwa bidhaa inayotafutwa kwa kiasi kikubwa na Wanunuzi na Wauzaji Wakubwa wa Madini ya Vito na Usonara wanaoshiriki na kutembelea katika Maonesho ya 68 ya Vito na Usonara yanayoendelea katika jiji la Bangkok eneo la Queen Sirikit nchini Thailand.

Hayo yamebainishwa Septemba 9, 2023 na Mkurugenzi wa Kampuni ya Ruby International Limited Mhe. Salim Hasham ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ulanga, Mahenge Mkoa wa Morogoro ambaye kampuni yake inashiriki katika maonesho hayo. Kampuni hiyo inajishughulisha na uuzaji, uchimbaji na ununuzi wa madini mbalimbali ya vito yakiwemo ya Spinel, Tanzanite, Garnet na mengine.

Akizungumza katika mahojiano maalum, baada ya ujumbe wa Wizara kutembelea banda lake, Mhe. Salim amesema kwamba Spinel ni miongoni mwa madini yanayotafutwa zaidi katika soko la dunia yakiwemo madini ya Tanzanite ambayo yanayozalishwa Tanzania pekee ulimwenguni kote katika eneo la Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara.

Kufuatia mahitaji ya madini hayo kwenye soko la dunia, Mhe. Salim amewataka wachimbaji nchini kuinuka na kutumia maonesho makubwa ya madini yanayofanyika katika maeneo mbalimbali duniani kujitangaza, kutafuta masoko na kujenga mahusiano ya kibiashara na kusisitiza kuyaongeza thamani madini yao kwa lengo la kupandisha thamani yake na hatimaye waweze kunufaika zaidi kupitia rasilimali madini, kuongeza mapato ya Serikali na mchango wa Sekta ya Madini kwenye maendeleo ya nchi.

‘’Spinel inatafutwa sana hapa, kila anayekuja anauliza Mahenge Spinel? Ni madini yanayotakiwa sana kwenye soko la dunia. Isitoshe madini yanayozalishwa Tanzania ni maarufu sana duniani. Ni kwetu sisi watanzania tuamue, tuamke na tufanye wenyewe kwa kuwa tumeamua kufanya,’’ amesisitiza Mhe.Salim.

Ameongeza kwamba, Tanzania ni mzalishaji mkubwa wa madini ya Spinel, ikifuatiwa na nchi za Vietnam na Myanmar ( zamani Burma) na kuongeza kuwa, madini ya Tanzania katika soko la dunia yanachangia zaidi ya asilimia 15.

Akizungumza kuhusu thamani ya madini Spinel, Mthamini Mkuu wa Serikali kutoka Wizara ya Madini Archard Kalugendo amesema Spinel ni miongoni mwa madini yenye thamani kubwa duniani na kueleza kuwa, hivi sasa bei yake ni mara 10 zaidi ya Tanzanite.

Maonesho ya Bangkok ni moja ya maonesho makubwa na maarufu sana Barani Asia na sasa yana takribani miaka 40 tangu kuanzishwa kwake. Serikali ya Tanzania inayatumia maonesho hayo kujitangaza, kutafuta masoko, ushirikiano, teknolojia mpya pamoja na kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu Sekta ya Madini hususan katika eneo la madini ya Vito na usonara ambapo nchi ya Thailand imepiga hatua kubwa katika uendelezaji wa madini hayo.

By Jamhuri