Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Lindi

Shirika la Madini la Taifa (Stamico) limesema litaendelea kutoa elimu, vifaa na kuboresha mazingira ya uchimbaji hapa nchini ili rasilimali za Taifa ziweze kusaidia wengi zaidi.

Miongoni mwa mafanikio wanayojivunia ni ushirikiano na makubaliano waliyoingia na benki nne kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wachimbaji wadogo nchini.

Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa saba wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Ofisa uhusiano wa shirika hilo, Bibiana Ndumbaro alipokuwa akiwasiliana mada katika Mkutano Mkuu wa saba wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) uliofanyika mkoani Lindi.

Amesema fursa hiyo ya kutoa na kupokea mikopo inalenga kuwawezesha wachimbaji kununua vifaa vya kisasa na kukuza biashara zao, ajira na uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa.

Bibiana amesema makubaliano waliyoingia na benki hizo nne yatawawezesha wachimbaji wadogo kuomba mikopo kwenye taasisi hizo na wao (Stamico) wanapoombwa taarifa wachimbaji hao huzitoa ili wahusika wapate mikopo waliyoomba.

“Kimsingi hapa tunazungumzia benki za NMB, KCB CRDB na Azania ambazo zipo kusaidia wachimbaji wadogo kufikia malengo yao, rasilimali zetu ni vema zitakatusaidia kupiga hatua kiuchumi” amesema .

Bibiana amesema Stamico imedhamiria kuleta suluhisho la kudumu la upatikanaji wa mikopo kwa wachimbaji wadogo kwa kuhakikisha inasimamia kuanzishwa kwa Benki ya Wachimbaji ambapo taratibu za uanzishwaje wake umeanza.

Amesema kuwa Stamico imeboresha uendeshaji wa miradi yake na kuifanya kuwa sehemu ya kukusanya mapato na sio matumizi jambo lililosababisha kuongezeka kwa mapato yake.

“Tumeboresha mradi wetu wa kuzalisha nishati mbadala ya kupikia kwa kuleta mitambo mikubwa miwili yenye uwezo wa kuzalisha tani 20 kwa saa kila mmoja ili kuongeza uzalishaji wa nishati hiyo kuweza kuwafiki wananchi wengi. Mitambo hii itafungwa mkoani Pwani na Songwe” amesema.

Bibiana amesema kuwa Stamico imechagiza kuanzishwa kwa kiwanda cha kusafisha dhahabu cha Mwanza ambacho kimechochea ongezeko la thamani ya madini hivyo kuchochea ukuaji wa ajira na teknolojia kwa Watanzania.

Ameongeza kuwa kupitia miradi ya ubia Stamico inahakikisha miradi hiyo inarithisha teknolojia na kutoa ajira kwa Watanzania.

Amebainisha kuwa wameendelea kutoa elimu ya teknolojia kwa vitendo kwa wachimbaji wadogo na kuongeza kituo cha mfano kwa ajili ya wachimbaji wa chumvi mkoani Lindi ili kuhakikisha wanazalisha chumvi yenye ubora kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi