Tabora

Na MoshyKiyungi

Hoja kwamba ulemavu si tija na kwamba mlemavu akipewa nafasi anaweza, huenda ikachukuliwa kama mpya miongoni mwa jamii.

Wapo walemavu kadhaa waliofanikiwa kimaisha na kuwa mfano wa kuigwa kwa jamii katika fani mbalimbali, ikiwamo muziki.

Mmoja wapo ni Stevland Hardaway Morris, anayefahamika zaidi kama Stevie Wonder.

Huyu ni mwanamuziki tajiri mwenye ulemavu wa macho ambaye pia ni mwanaharakati wa haki za binadamu.

Mkongwe huyu raia wa Marekani, Stevie Wonder, mbali na kuimba, pia ni mtayarishaji wa muziki mwenye uwezo wa kupiga ngoma, piano, gitaa na ala karibu zote za muziki.

Sauti yake nzuri anapoimba hufikisha ujumbe mahususi autakao na siku zote huvaa miwani myeusi, kichwani akiwa na ‘rasta’.

Kwa hakika muziki humtoa na kumtendea haki Stevie Wonder, aliyezaliwa Mei 13, 1950 katika Jimbo la Michigan, Marekani.

Muziki wake unatambulika na kukubalika katika kila kona ya dunia.

Stevie Wonder ni miongoni mwa wanamuziki wakubwa wenye mafanikio, wanaojulikana sana katika studio maarufu ya kurekodi muziki, Motown, na katika maisha yake amekwisha kurekodi zaidi ya albamu 23; miongoni mwao akiwashirikisha au akishirikiana na wanamuziki wengine maarufu na wenye sifa kubwa.

Miongoni mwa misukosuko aliyopitia ni pamoja na Serikali ya Afrika Kusini kupiga marufuku nyimbo zake Machi 26, 1985.

Uamuzi huo ulifikiwa kutokana na kauli aliyoitoa wakati akipokea tuzo ya Oscar mwaka huo, aliposema: 

“Tuzo hii ninaipokea kwa jina la Nelson Mandela.”

Ikumbukwe kuwa wakati huo Mandela alikuwa gerezani akitumikia kifungo cha maisha kwa makosa ya uhaini.

Ni wazi kuwa Stevie Wonder alikuwa mmoja wa watu waliokuwa wakimpenda na kumuunga mkono Mandela hata kabla hajawa Rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini.

Mwaka 1963 Wonder alitoka na sehemu ya pili ya wimbo ‘Fingertips’, mwaka 1966 aliachia nyimbo za ‘Uptight (Everything’s Alright)’, ‘Blowing in the Wind’ na‘A Place in the Sun’ ambapo mwaka 1967 akaja na wimbo wa ‘I Was Made to Love Her’.

Nguli huyo ametunga na kuimba nyimbo nyingi, baadhi ya nyimbo hizo ni ‘From the Bottom of My Heart’, ‘Shelter In The Rain’, na ‘So What The Fuss’ zikiwa ni sehemu ya juhudi za Umoja wa Mataifa (UN) kwa kuwashirikisha wanamuziki wa kimataifa.

Katika kusisitiza umuhimu wa furaha katika maisha ya kila siku, mkongwe huyu amewahi kuzindua kampeni kwa wimbo au muziki unaoweza kuleta tabasamu kwa kila mtu, uliolenga kuhamasisha matumaini bora duniani.

Katibu Mkuu wa UN wakati huo, Ban Kin Moon, aliuteua wimbo wenye ujumbe wa amani wa Stevie Wonder ambao kwake ulisikika kama sauti za furaha katika uwepo wa makubaliano mapya juu ya malengo ya maendeleo endelevu katika ajenda za viongozi wa kimataifa zilizoandaliwa kujadiliwa.

Mmarekani huyo alishiriki kutunga na kuimba wimbo maarufu uliowajumuisha magwiji wengi wa muziki uliopewa jina la ‘We are The World’.

Hivi karibuni, mkongwe huyo amepata mtoto wa tisa baada ya mpenzi wake, Tomeeka Bracy, kujifungua mtoto wa kike na kumpa jina la Nia.

Na sasa Wonder ni baba wa familia ya watoto tisa kwa wanawake aliowahi kuwa nao katika vipindi tofauti.

Wonder bado anapiga muziki huko Marekani. Mungu amzidishie maisha marefu.

Makala hii imeandaliwa kwa msaada wa vyanzo mbalimbali.

Mwandaaji anapatikana kwa namba 0784331200, 0713331200, 0736331200 na 0767331200.

By Jamhuri