Limejizatiti katika viwanda

Limejikita katika miradi ya kimkakati





Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. John Pombe Magufuli akizindua kituo Cha Uwekezaji cha JWTZ    kilichopo Mgulani JKT jijini Dar Es Salaam.

Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMAJKT), linaanzisha viwanda vipya na kuboresha viwanda lilivyonavyo ili kuzalisha kwa tija, lengo likiwa ni kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli ambayo imedhamiria kuifanya Tanzania yenye uchumi wa kati unaojengwa na viwanda ifikapo mwaka 2025.

Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa ambaye pia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa SUMAJKT, Brigedia Jenerali Charles Mbuge ameeleza kuwa, Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli anatimiza miaka minne katika uongozi wake tangu alipoapishwa rasmi tarehe 5, mwezi Novemba, mwaka 2015, katika muda huo wa uongozi wake, SUMAJKT limepata mafanikio mbalimbali ikiwemo:

Kiwanda cha Ushonaji (The National Service Garments Factory)

Kiwanda hiki kipo katika kituo cha uwekezaji cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Mgulani JKT jijini Dar es Salaam, kinashona mavazi ya aina mbalimbali zikiwemo nguo za watu binafsi, sare za vyombo vya ulinzi na usalama, shule, makampuni na taasisi mbalimbali.

Kiwanda cha maji ya kunywa ‘SUMAJKT Bottling Plant’

Hiki ni kiwanda kingine kilichoanzishwa, nacho kipo katika kituo cha uwekezaji cha JWTZ kilichopo Mgulani JKT ambacho kinatumia mitambo ya kisasa kuzalisha maji ya kunywa yajulikanayo kwa jina la ‘Uhuru Peak’ na kinasambaza na kuuza maji yake katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Kiwanda cha kutengeneza bidhaa za ngozi

Shirika limeanzisha kiwanda cha kutengeneza bidhaa za ngozi kwa majaribio, ambapo kimeanza kwa kutengeneza viatu vya aina mbalimbali zikiwemo buti za vyombo vya ulinzi na usalama, viatu vya shule, viatu vya watoto na watu wazima.

Kiwanda cha kuchakata nafaka Mlale

Kiwanda kinachakata mahindi na kutengeneza unga safi wa sembe ujulikanao kwa jina la ‘SUMAJKT Mlale Sembe’. Kiwanda hiki ni cha ubia kati ya Shirika na Kikosi cha Mlale JKT.

Kiwanda cha taa (SUMAJKT SKYZONE)

Hiki ni kiwanda cha ubia kati ya SUMAJKT na Kampuni ya Everlight Skyzone ya nchini China ambacho kinajihusisha na utengenezaji wa taa za kisasa za barabarani na mitaani, ujenzi wa kiwanda hicho unaendelea katika eneo la Makao Makuu ya JKT Mlalakuwa, jijini Dar es Salaam.

Kiwanda cha samani Chang’ombe

Kiwanda kipo eneo la Chang’ombe, jijini Dar es Salaam. Ni moja ya kiwanda ambacho kimeboreshwa zaidi kwa kununua mashine za kisasa, hali ambayo imeongeza ufanisi katika utengenezaji wa samani za kisasa kwa matumizi ya nyumbani na maofisini.

Kiwanda cha kubangua korosho

Shirika limo kwenye mchakato wa kupata mitambo ya kisasa ili kukiwezesha kiwanda cha kubangua korosho cha ‘SUMAJKT Cashew Nuts Industry’ kilichopo Lindi kufanya ubanguaji wenye tija. Hii inatokana na uamuzi wa Serikali kuliamini Jeshi kupitia SUMAJKT na kulikabidhi shirika kuendesha kiwanda hicho ambacho awali kilifahamika kwa jina la BUCO.

Brigedia Jenerali Mbuge amefafanua kuwa SUMAJKT pamoja na kujiimarisha katika sekta ya viwanda, pia limejikita katika miradi ya kimkakati kuhakikisha shirika linafanya biashara kwa tija ili kuongeza pato la shirika na taifa kwa ujumla katika maeneo yafuatayo:

SUMAJKT Recreation and Catering Services

Inatoa huduma za kumbi ambazo ni Uhuru unaochukua watu 1,000 na Umoja watu 500, kwa ajili ya shughuli mbalimbali zikiwemo harusi, mikutano, semina na warsha, pia inatoa huduma ya chakula na vinywaji. Kumbi hizo zipo eneo la Mwenge jijini Dar es Salaam.

SUMAJKT Auction Mart

Ni kampuni inayoshughulika na minada, ukusanyaji madeni, ushuru, kodi na kukaza hukumu za mahakama.

SUMAJKT Guard Limited

 Kampuni hii imepanua wigo wake zaidi wa kutoa huduma ya ulinzi binafsi katika mashirika ya umma, taasisi na watu binafsi nchi nzima hadi sasa imefanikiwa kutoa ajira kwa vijana 9,000, pia imeanzisha huduma ya usafi na umwagiliaji dawa kwa shule, vyuo, hospitali, taasisi za umma na mashirika pamoja na watu binafsi kupitia mradi wake wa ‘SUMAJKT Cleaning and Fumigation’.

SUMAJKT Insurance Broker

Kampuni hii inatoa Bima ya Maisha na Bima zisizo za Maisha, mfano bima ya afya, magari, nyumba, safari na nyinginezo.

SUMAJKT Port Services

Kampuni hii inasimamia huduma za vibarua wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), katika Bandari ya Dar es Salaam na Maziwa Makuu.

SUMAJKT Construction Company Limited (SUMAJKTCCL)

Katika kuboresha huduma, shirika limebadilisha jina la kampuni yake ya ujenzi ambayo awali ilifahamika kwa jina la National Service Construction Department (NSCD) na kuwa ‘SUMAJKT Construction Company Limited’.

Kampuni hii imefanikiwa kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi yenye masilahi kwa taifa ikiwemo, ujenzi wa ukuta unaozunguka mgodi wa madini ya tanzanite Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, wizara sita katika Mji wa Serikali jijini Dodoma na nyumba 41 za wasaidizi wa Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli.

SUMAJKT Tower

Katika kutekeleza azima ya Serikali  ya Awamu ya Tano ya kuhamia Dodoma, SUMAJKT linaendelea na ujenzi wa jengo la  Makao yake Makuu katika eneo la Medeli East, Manispaa ya Dodoma lenye ghorofa tano ambalo linafahamika kwa jina la ‘SUMAJKT Tower’, pia litakuwa na ofisi  kwa ajili ya kupangisha taasisi mbalimbali.

Afisa Mtendaji Mkuu  wa SUMAJKT pia amebainisha kuwa shirika limefanikiwa kutoa gawio kwa Serikali, na kuchangia Pato la Taifa kupitia faida linayoipata kutoka katika miradi na kampuni zake mbalimbali.

Vilevile shirika limefanikiwa kuzalisha ajira kwa vijana wa Kitanzania katika miradi, kampuni na viwanda vyake.

Afisa Mtendaji Mkuu, Brigedia Jenerali Mbuge, kwa niaba ya menejimenti na watendaji wa SUMAJKT anampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mheshimiwa Dk. John Pombe Magufuli kwa kutimiza miaka minne ya uongozi wake ambao umeifanya SUMAJKT kuongeza kasi katika utekelezaji wa majukumu yake na kuweza kuanzisha viwanda na miradi mipya.

By Jamhuri