Binadamu huogozwa na hulka, dhamiri na nafsi aliyonayo. Hulka ni tabia ya kujifunza kutoka katika jamaa na jamii yake anamoishi. Dhamiri na akili vinamwezesha kutofautisha mambo ya kutenda na kutotendwa na nafsi inampatia hali ya kujijua kuwa ni binadamu na kuwajua watu wengine kwamba nao ni binadamu.

Mambo matatu haya kwa pamoja humwezesha binadamu kuishi pamoja, kufanya kazi pamoja na kuelewana katika kuendeleza maisha yao, utamaduni wao, uchumi wao na hata ulinzi na usalama wao. Mambo haya huwa mwongozo na dira katika maisha yao.    

Chini ya misingi ya tabia ya kujifunza, akili ya kumwezesha kutofautisha na hali ya kujijua ni binadamu, mtu huyu hujikuta katika mfumo unaomchakatua kuelewa mapema au kuchelewa kufahamu au kutomaizi daima jambo lililo mbele yake. Huu ni mchakato muhimu kwa binadamu yeyote. 

Kuelewa mapema, kuchelewa kufahamu na kutomaizi daima ni hali zinazomfanya binadamu kuonekana ima anatambua au hatambui mambo. Hizi ni changamoto kati ya mtu na mtu katika kuchagua na kupanga mustakabali wa maendeleo yake na ya jamii yake. 

Mwezi Oktoba 2019, Rais Dk. John Magufuli alifanya ziara ya siku tatu mkoani Songwe kukagua shughuli za serikali, miradi ya maendeleo na kutoa shukrani kwa wananchi waliomchagua kuwa rais wa nchi. Katika ziara hii, tumeona mambo mengi yamefanikishwa na machache yamekwamishwa. 

Kutekelezwa au kukwama kwa miradi ya maji, afya, elimu, barabara na mingineyo kwa kiasi kikubwa kunatokana na mifumo inayochakata viwango vya uelewa kwa mtu mmoja mmoja au watu wengi pamoja, katika kufasili maelezo na maelekezo yatolewayo kuhusu miradi hiyo. Hili ni tatizo linalohitaji tiba ya haraka. 

Katika ziara hiyo, rais alizihutubia hadhira nyingi mbalimbali akiwa njiani na kwenye vituo vilivyoratibiwa kwa mikutano ya hadhara. Alisisitiza kuimarishwa umoja wa kitaifa na kufanya kazi kuleta maendeleo ya nchi. Aidha, aliwasihi Watanzania wasiruhusu vitendo vya rushwa, ufisadi na utovu wa nidhamu kulelewa katika jamii yetu. “Lazima tujenge taifa lenye nidhamu.”

Kutokana na maelezo haya ya utangulizi, hebu soma na tafakari dondoo zifuatazo nilizozinukuu na kuzisanifu kutoka katika hotuba moja wapo ya Rais Magufuli alipozungumza na wananchi wa Mkoa wa Songwe.

“Tuliwekewa mawazo sisi ni maskini. Sisi ni tajiri na tajiri hakopikopi. Tusisubiri wafadhili, tujifadhili wenyewe, hela ziko hapa hapa (Tanzania). Fedha zilikuwa zinaliwa na mafisadi. Ndugu zangu ninawaambia ukweli, sisemi uongo.

“Mlinichagua bure ndugu zangu, ni lazima niyatoe haya bure. Na hiyo ndiyo sadaka yangu kwenu. Jeuri hii niliyonayo ni kwa sababu yenu. Hili lote ni kutekeleza lengo la Baba wa Taifa (Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ) la kuondoa umaskini.

“Nataka Watanzania muelewe, hakuna mtu anaweza akafurahi nyinyi mnajenga Stiegler’s Gorge kwa fedha yenu bilioni 6.5. Walitakiwa wawakopeshe, mjenge kwa trilioni 20, mfe na madeni na kila siku muwe mnachangia kwa miaka yote.

“Ninawaambia ndugu zangu, ninawaomba Watanzania wezangu angalau mnielewe. Mnielewe basi kwa kipindi hiki ninachokuwa rais. Nikishaondoka basi msinielewe. Ili  kusudi hizi ninazowasaidia Watanzania mpate kuwepo kama ukumbusho. Ninawaambia ndugu zangu kwa dhati kabisa.

“Ni lazima Watanzania na nchi za Afrika tuanze kujitambua na kusema kwa nini? Watanzania na Waafrika tujiulize, kwa nini nchi tajiri kama DRC zenye madhahabu na maalmasi magomvi makubwa hayaishi huko?”

Je, Mtanzania na Mwafrika mwenzangu, dondoo hizi za Rais Magufuli umezielewa au bado haujazifahamu au ndiyo huwezi kuzimaizi? Nakushauri tu tafadhali jitambue, badilika na acha mazoea ya kukubali mbinu za mabeberu za kutishwa tishwa ili uendelee kunyonywa na kudhulumiwa. 

654 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!