Na Stella Aron, JamhuriMedia

Dunia kwa sasa inakabiliwa na mabadiliko yua tabia nchi na kuwepo kwa madhara ambayo tayari kwa Bara la Afrika yamenza kuonekana.

Ulimwengu umeingia rasmi katika kipindi cha El Nino, kulingana na Shirika la Sayansi la Marekani (NOAA), Shirika la Hali ya Hewa Ulimwenguni (WMO) na Umoja wa Mataifa ambapo zimetoa taarifa ya tukio la asili la El Nino kufuatia kuanza kwa mvua za msimu.

Kila nchi kupitia Mamlaka zake za Hali ya Hewa zimetoa taarifa ya tukio hili la asili linalotokea kila baada ya miaka kadhaa baada ya kuonekana kwenye mifumo ya hali ya hewa. Nchini Tanzania Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) nayo ilithibitisha uwepo wa El Nino.

Lakini kawaida El Nino huathari hali ya hewa duniani, kuanzia joto kali, mvua nyingi na katika baadhi ya maeneo husababisha ukame. Julai 19, 2023 Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), ilitoa taarifa ya uwepo wa El Nino katika kipindi cha msimu wa vuli zilizoanza.

EL NINO MAANA NI NINI

Ni hali ya uwepo wa ongezeko la joto la bahari ya katika eneo la kati ya kitropiki la Bahari ya Pasiki, hali hii inapokuwepo kunakuwa na madhara mbalimbali katika maeneo tofauti ya dunia.

El Nino ni sehemu ya tukio la asili la hali ya hewa linaloitwa El Nino Southern Oscillation (ENSO). ENSO ina asili mbili zinazokinzana: El Nino na La Nina ambazo zote zinabadilisha hali ya hewa duniani kwa kiasi kikubwa.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), El Nino ni mfumo wa hali ya hewa unaosababishwa na uwepo wa joto la bahari la juu ya wastani katika eneo la kati la kitropiki katika Bahari ya Pasifiki. Hali hii kwa kawaida huambatana na vipindi vya mvua kubwa vinavyoweza kusababisha mafuriko.

Tukio la El Nino kwa kawaida huthibitishwa wakati ambapo halijoto ya uso wa bahari katika eneo la tropiki ya Pasifiki ya Mashariki inapopanda hadi angalau 0.5C juu ya wastani wa kawaida na kwa muda mrefu.

La Nina ambayo si maarufu sana ni kinyume chake, Wakati halijoto ya uso wa bahari inaposhuka kwa karibu nyuzi joto 3-5, La Nina hutangazwa. Hii inasababisha hali ya hewa ya baridi na kavu kwa wastani katika sehemu za Bahari ya Pasifiki, kati ya Amerika Kusini na Australia.

Tukio la El Nino inahusiana na joto la maji ya bahari ya Pasifiki ambalo hutokea kila baada ya miaka mitatu au nane na hudumu kwa miezi 9-12, kwa mujibu wa wataalamu.

Inaelezwa tangu mwaka 1900 kumekuwa na angalau matukio 30 ya El Nino duniani huku El Nino ya mwaka 1982-1983, 1997-1998 na 2014-2016 ni miongoni mwa matukio yaliyoweka rekodi na kuleta madhara makubwa.

Katika miaka ya 2000, matukio ya El Nino yamejitokeza mwaka wa 2002–2003, 2004–2005, 2006–2007, 2009–2010, 2014–2016, 2018–2019, na sasa mwaka 2023 limeanza ambapo kilele chake kinatarajiwa kuwa Februari 2024.

Mbali na mvua kubwa wataalamu wa hali ya hewa wameonya kuwa huenda El Nino ya mwaka huu ikasababisha mwaka 2024 kuwa mwaka wa joto kali zaidi duniani.

RAIS SAMIA AGUSWA NA UTABIRI HUO

Rais Samia Suluhu Hassan

Kutokana na tahadhari hiyo, Rais Samia Suluhu Hassan aliwataka viongozi wa miji mikubwa nchini, kuchukua jithada za makusudi katika kuandaa mikakati ya kukabiliana na athari za mvua kubwa maarufu kama El Nino.

“Ningepeda kusisitiza juu ya tahadhari ya kuwepo mvua za El Nino wakati wa msimu Vuli hususani Kanda ya Ziwa na Pwani. Mmlaka ya Hali ya Hewa imetabiri kuhusu uwezekano huo.

“Sasa ukipita miji mikubwa hauoni tahadhari iliyochukuliwa bado mitaro ya maji imejaa takataka badala ya kusafisha ili mvua zinaponyesha maji yapite kwa haraka. Wasimamizi wa miji himizeni usafi wa maeneo yenu ili mvua zinapokuja zisilete madhara.

“Tunasali ili mvua hizi ziwe za kawaida ili zilete neema na baraka nchini, lakini ikimpendeza Mungu zikawe nyingi basi zisituletee athari.” anasema Rais Samia.

Dkt. Samia ametoa rai hiyo wakati akipokelewa na mamia ya wakazi wa Mkoa wa Singida eneo la Sagara akiwa katika ziara ya kikazi ambapo akiwa mkoani humo alifungua shule 302 zilizojengwa kwa mradi wa Boost na Sequi.

MAJALIWA ATOA MAELEKEZO

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa anasema Serikali itaendelea kuchukua hatua stahiki kukabiliana na mvua za El-Nino ambapo ameziagiza wizara, mikoa na taasisi za Serikali kuainisha na kuandaa rasilimali za kujiandaa, kuzuia na kukabiliana na maafa.

Majaliwa ameitaka wizara, mikoa na taasisi za Serikali kuelimisha namna ya kuwahamisha wananchi kwenye maeneo hatarishi na kuchukua tahadhari ili kuokoa maisha na mali.

Amezitaka idara na taasisi zinazohusika na mazingira na miundombinu kuhakikisha barabara zinapitika wakati wote, mitaro na makalavati yanazibuliwa, kuimarishwa na kusafishwa ili kuruhusu maji kupitika kwa urahisi.

Pia anazitaka sekta za maji, umeme na mawasiliano kuweka mipango ya kuzuia madhara, lakini pia kushirikisha wadau wa maafa wakiwemo wananchi , taasisi za umma na sekta binafsi katika mipango ya usimamizi wa maafa.

“Kamati zote za maafa katika ngazi za kijiji, wilaya, mkoa na taifa, zianze kujipanga kikamilifu kukabiliana na changamoto za El-Nino endapo zitajitokeza kwenye maeneo yetu.” anasema Majaliwa.

Sambamba na hilo anazitaka wizara, idara na taasisi, mikoa na halmashauri kuandaa mipango ya utekelezaji katika maeneo yao kwa kuzingatia mpango wa taifa wa dharura kukabiliana na El-Nino.

BITEKO ATOA MAELEKEZO KUKABILIANA NA MADHARA YA EL NINO

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko ametoa maelekezo mbalimbali yatakayoboresha ufanisi katika utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Dharura wa Kuzuia na Kukabiliana na Madhara ya El Nino kama ilivyotabiriwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).

Akizindua mpango huo na kuugawa kwa Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu pamoja na viongozi wa baadhi ya Taasisi za Serikali kwa ajili ya kuanza utekelezaji wake anasema mpango huo umeandaliwa ili kuhakikisha kuwa Serikali, wadau na jamii wanachukua hatua stahiki za kuzuia na kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na El Nino na kujiandaa kukabiliana na kurejesha hali ya madhara yatakayojitokeza.

“Ili kuwa na ufanisi katika kutekeleza mpango huu, nazielekeza sekta zote kuchukua hatua kuainisha na kuandaa rasilimali za kuzuia na kujiandaa kukabiliana na maafa endapo yatatokea kwa kila sekta kushiriki kikamilifu katika eneo lake.

“Kutambua maeneo hatarishi yenye viashiria vya kuathirika na maafa na kuandaa mpango wa kuzuia madhara na kukabiliana na maafa, kuelimisha wananchi na kuwahimiza kuhama kwenye maeneo hatarishi, umuhimu wa kuweka akiba ya chakula na kulima mazao yanayohitaji maji mengi pamoja na hatua za kuchukua tahadhari ili kuokoa maisha yao na mali”, anasema Biteko.

Maelekezo mengine ni kuandaa na kutekeleza mipango ya kuzuia milipuko ya magonjwa kwa binadamu, wanyama na mimea, Idara ya Taasisi zinazohusika na mazingira, miundombinu, kuhakikisha barabara zinapitika wakati wote, kuimarisha na kusafisha mitaro na makalavati, sekta za maji, umeme na mawasiliano ziweke mipango ya kuzuia madhara na kuhakikisha uharibifu katika huduma hizo unapewa ufumbuzi mapema, kutoa taarifa haraka kwa Mamlaka husika pale inapotokea maafa kwenye sekta na kuimarisha upatikanaji wa vifaa vya maokozi na huduma za dharura pamoja na kutoa elimu kwa Watendaji katika ngazi zote ili wachukue hatua stahiki za kuzuia na kupunguza madhara ya El Nino yanayoweza kujitokeza.

Vilevile, amezitaka sekta kuimarisha na kusafisha njia za maji ya mvua na maji taka pamoja na usimamizi wa taka ngumu na uwepo wa madampo, kuimarisha madaraja na kingo za mito na mabwawa katika maeneo yote ya kimkakati, kusimamia matumizi sahihi ya mitaro na njia za maji kwa kuzuia viwanda kutiririsha uchafu katika maeneo ya makazi na sehemu za kuzalishia maji, Wizara, Idara, Taasisi, Mikoa na Halmashauri zote ziandae mipango ya utekelezaji katika maeneo yao kwa kuzingatia mpango huu ulioandaliwa na kuhakikisha mvua hizi zinatumika kwa shughuli za maendeleo.

Pia, kufuatilia na kutekeleza maelekezo ya kitaalam pamoja na taarifa za utabiri wa hali ya hewa unaotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini na kuweka utaratibu wa kuandaa ujumbe mfupi na kuusambaza kwa njia ya simu.

Aidha, ametoa msisitizo kuwa wizara zichukue wajibu wake wa kuandaa kukutana na wadau na watu walio chini yenu kuwapa maelekezo hayo na kwenye matangazo na hotuba zao kutenga eneo la kuweka ujumbe unaohusiana na kuwatahadharisha Watanzania madhara ya El Nino.

SABABU YA TMA KUTEMBEA KIFUA MBELE

Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania TMA Dkt. Ladislaus Chang’a akifungua mafunzo ya waandishi wa habari kuhusu utabiri wa Hali ya hewa yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Kibaha Conference Center mjini Kibaha mkoani Pwani Leo.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Ladislaus Chang’a, anasema kuwa uwekezaji mkubwa uliofanyika katika kuimarisha huduma za hali ya hewa nchini na Serikali umechangia kuongeza ufanisi katika utendajikazi kwa TMA na sasa kutembea kifua mbele.

Anasema kuwa Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imefanya jambo kubwa sana la uwekezaji kwa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), ambapo matunda yake ni kufanyakazi yenye uhakika ambapo pia yamesaidia kushirikiana na nchi mbalimbali duniani na Tanzania kupata manufaa.

“Kuna mengi ambayo Serikali imechangia TMA kujipambanua kutokana na uwekezaji katika nyanya mbalimbali kwa TMA, hivyo ni vyema kuishukuru Serikali kwa juhudi kubwa iliyofanya na kuchangia tabiri zetu kuwa zenye uhakika kabisa mbali ya uwekezaji pia wafanyakazi walikwenda kupata mafunzo ya kuongeza ujuzi kutoka katika nchi mbalimbali zilizoendelea,” anasema.

Hata hivyo anasema kuwa matukio ya hali mbaya ya hewa ambayo yanendelea kuongezeka ni pamoja na mvua kubwa za muda mfupi, joto kali, upepo mkali na vimbunga ambapo tathmini ya karibuni inaonesha matukio ya El Nino yataongezeka kwa idadi na ukubwa kadri ambavyo joto la dunia linaendelea kuongezeka.

“Mwelekeo wa mvua za vuli kwa mwaka 2023 unaonesha msimu wa mvua za vuli utachagizwa na uwepo wa El Nino, tunaendelea kufanya kazi masaa 24 kufuatilia mabadiliko katika bahari zote ambapo tunachokiona kwa sasa ni ukubwa wa El Nino kuwa katika nyuzi joto 1.2 ambao ni ukubwa wa wastani, na tunatarajia mvua hizo zitaenda mpaka Januari mwakani.” anasema Dkt. Chang’a.

NENO KWA MENEJIMENTI ZA MAAFA NCHINI

Kaimu Mkurugenzi TMA, Dkt Chang’a, anasema kuwa mvua za Juu ya Wastani hadi Wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, kusini mwa mkoa wa Simiyu, kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma, Dar es Salaam, Tanga, Pwani (ikiwemo visiwa vya Mafia), kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro na pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba katika msimu wa mvua za Vuli, 2023.

Aidha, maeneo ya mikoa ya Mara, kaskazini mwa Mkoa wa Simiyu, Arusha, Manyara na Kilimanjaro yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani na katika kuhakikisha kuwa taarifa hizo zinazingatia, TMA imezitataka Idara na Menejimenti ya maafa nchini, kuendelea kuratibu utekelezaji wa mipango itakayosadia kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza kipindi cha mvua.

Chang’a anazitaka mamlaka husika katika mikoa, wilaya kata na vijiji kutoa elimu na miongozo, itakayohamasisha kuzuia au kupunguza madhara yatokanayo na mvua.

Pia wamezita sekta zinazotumia Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini kama wakulima, wafugaji, wavuvi mamlaka za wanyamapori na wadau kufuatilia taarifa za TMA mara kwa mara ili kupata taarifa mahsusi za utabiri wa msimu ili kukidhi mahitaji katika sekta zao.

Anasema TMA inatoa taarifa ya uchambuzi wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa mvua za msimu, kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua mwaka (kanda ya magharibi kati, Nyanda za Juu Kusini Magharibi , Kusini mwa nchi Ukanda wa Pwani ya kusini pamoja na maeneo yaliopo kusini mwa Mkoa wa Morogoro) katika kipindi cha Novemba na Aprili 2024.

Anasema kipindi cha nusu ya kwanza ya msimu wa Novemba 2023 mpaka Januari 2024 ,kinatarajiwa kuwa na mvua nyingi, ikilinganishwa na nusu ya pili Februari – Aprili 2024 uwepo wa El-Nino unatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika mvua za msimu.

ATHARI SHUGHULI ZA KILIMO, WAFUGAJI

Anasema kuwa athali na ushuri katka shughuli za kilimo zinatarajiwa kuendelea kama kawaida,katika maeneo mengi hata hivyo vipindi vya unyevu wa kuzidi kiasi ,pamoja na mafuriko vinaweza kujitokeza na kuathiri ukuaji wa mazao na miundombinu ya kilimo kina cha maji katika mito, mabwawa kinatarajiwa kuongezeka.

Mamlaka inawashauri wadau mbalimbali kuzingatia matumizi endelevu ya uhifadhi wa rasilimali maji mwenendo wa msimu wa mvua za vuli.

Kutokana na uwepo wa mvua kubwa zinazoweza kuleta mafuriko magonjwa ya milipuko kwa mifugo na mazao kwa Mkoa wa Mbeya kukiwa na wastani wa mvua milimita 1,000 mpaka 1,520 kwa kipindi cha Novemba mwaka huu mpaka Aprili 2024, Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na Magharibi imetoa tahadhari kwa wakulima na wafugaji kutumia mbinu bora za kudhibiti miundombinu sambamba na mmomonyoko wa udongo kwenye mashamba yenye rutuba.

WAKULIMA MBEYA WAKUMBUSHWA

Kaimu Meneja TMA Kanda ya Mbeya, Abel Nyamende anasema kuwa wakulima wanapaswa kufuatilia taarifa za hali ya hewa kwa kuandaa mashamba, kupalilia na kupanda mbegu zinazostahilimi maji mengi.

“Tumetoa tahadhari kwa wakulima na wafugaji kwani kuna uwekano mkubwa mvua zikaleta madhara ikiwepo wadudu waharibifu wa mazao na mifugo na magonjwa ya milipuko yatakayo sababishwa na mafuriko,”anasema.

Nyamende anasema ni wakati sasa wakulima kutumia taarifa za TMA kila wakati ili kwenda na kalenda na kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza endapo wakazalisha kwa mazoea na kupanda mbegu kiholela pamoja na tahadhari ya kudhibiti mmonyoko ardhini.

“Wingi wa maji unaweza kusababisha madhara mbalimbali sambamba na mafuriko, udongo wenye rutuba kusombwa na maji sambamba na wafugaji wa samaki kuhimarisha miundombinu ya mabwawa,”anasema.

Pamoja na kuwepo kwa mvua hizo anawataka wafugaji kutumia fursa ya mvua za msimu huu kuotesha nyasi na kuvuna maji ya mvua ambayo yatakuja kuwa msaada hapo baadaye kunywesha mifugo unapojitokeza ukame.

Pia, anashauri wananchi wanaoishi maeneo ya mabondeni kuchukua tahadhari ya kuondoka kwa kuzingatia utabiri wa hali ya hewa ya kuwepo kwa mvua nyingi nchini.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera anawataka wananchi wanaoishi kwenye maeneo ya hatarishi na mabondeni kuhama kabla ya majanga ya mafuriko kuwakumba kwani utabiri wa TMA unaonyesha uwepo wa mvua.

RC PWANI AZUNGUMZA NA WANAOISHI MAENEO HATARISHI

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge ,ametembelea Maeneo yenye viashiria vya kutokea athari za mvua za El Nino, ikiwemo eneo Mohoro na kuwaasa wakazi wa eneo hilo kuhama.

Akizungumza na wananchi wa Muhoro Kunenge anawataka ,kuzingatia maelekezo ya Serikali ya kuhama eneo hilo kwani mwaka 2021 eneo hilo liliathirika na mvua kubwa na Serikali kulazimika kutafuta eneo mbadala kwa ajili ya wananchi hao.

Anasema ,Serikali imeona ianze kujipanga na kudhibiti maafa yanayotokana na mafuriko pindi mvua zinaponyesha kwa kuhakikisha wananchi wanawekwa katika mazingira salama.

Kunenge,anasema kuwa wananchi hao wamepewa viwanja bure bila kulipia gharama yoyote na kwamba kila mmoja anapaswa kufanya maandalizi mapema ya kuanzisha makazi katika eneo hilo ambalo litakuwa limeondoa kero ya mafuriko yaliyokuwa yakitokea muda mrefu.

”Leo tumefika hapa kwa ajili ya kufanya maandalizi ya tahadhali juu ya mvua za El Nino ambazo zimekuwa zikileta maafa kwa wananchi wetu na ukizingatia Mkoa wa Pwani umezungukwa na Bahari ya Hindi ambayo imekuwa ikijaa maji wakati wa mvua na hivyo kuleta athari kwa wananch”, anaema Kunenge.

Kunenge alieleza,hupatikanaji wa viwanja hivyo imetokana na juhudi za Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ambaye ndiye aliyeridhia kugawa eneo hilo kwa wananchi wake na kwamba hakuna budi ya kumshukuru kwa hatua hiyo kubwa.

“Niwaombe wananchi wa Mohoro muungeni mkono Rais Samia kwa hatua hii kubwa aliyoifanya kwa kuhakikisha wote tunahamia katika maeneo tuliyopangiwa na sisi leo tumekuja kuwahamasisha ili muweze kuhama mapema,” anasema Kunenge

Katika hatua nyingine Kunenge , alifafanua mbali na hatua ya kugawa viwanja bure lakini pia tayari Serikali ipo katika mpango wa kujenga daraja jipya la Mohoro ambalo mara nyingi wakati wa mvua hujaa maji na hivyo kuleta maafa.

Walieleza,hatua hii ni njema kuchukua ,kufanya maandalizi juu ya kuwasaidia wananchi kuepukana na maafa yanayotokana na mvua za Elnino kama ambavyo imetangazwa na TMA.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Bw. Hemed Magaro anasema kuwa ni vyema sasa kufanyiakazi utabiri wa TMA kwani imeelezwa kuwa mikoa 14 kupata mvua kubwa.

Magaro anasema katika kuhakikisha wanakabiliana na janga hilo wameweka mikakati mbalimbali itakayosaidia kutekeleza usimamizi wa maafa ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kupitia njia mbalimbali ili jamii iweze kupata uelewa wa nini kinaweza kutokea na namna ya kujiokoa.

Vilevile amesema mikakati mingine waliyoweka kwa pamoja wameazimia kuhakikisha kunakuwepo na vifaa vya kutosha vya uokoaji sambamba na rasilimali watu, kuandaa bajeti ya dharura ya maafa, kutoa njia za mawasiliano, kujua idadi ya watu wanaoishi katika maeneo hatarishi n.k

Hata hivyo Magaro ameagiza idara ya afya kuhakikisha kunakuwa na akiba dawa za kutosha hasa kipindi hiki tunachotarajia mvua za El Nino kuanza kunyesha. Pia amesisitiza vyombo vya usafiri majini na nchi kavu kukarabatiwa na viwe tayari wakati wowote kuanzia sasa.

Mbali na hayo, Mwenyekiti Magaro ameagiza idara ya kilimo kuandaa mbegu za mazao ya muda mfupi kutumika kupunguza changamoto ya chakula baada ya mafuriko kutokea kwani kitaalamu maeneo yanayopitiwa na mafuriko hustawisha sana chakula katika ukanda wa bonde la mto Rufiji.

DAR ES SALAAM ILIVYOJIPANGA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Uratibu na Bunge, Jenista Muhagama

Mkoa wa Dar es Salaam umejipanga katika kuhakikisha inatoa huduma katika kipindi cha mvua kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali pamoja na zile zinazohusika na huduma ya utafutaji na maokozi, usalama wa wananchi, afya na makazi ya muda na huduma zingine za kijamii zimejipanga katika kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma pindi yanapotokea mafuriko kutokana na mvua za El Nino.

Taasisi zinazohusika kutoa huduma wezeshi au saidizi pamoja na kuimarisha mifumo kama vile usafiri, mawasiliano, nishati na maji zinakumbushwa kujiimarisha ili kuhakikisha shughuli za kijamii na kiuchumi haziathiriki wakati wa maafa.

Taasisi saidizi zina wajibu wa kuwezesha taasisi zenye jukumu ongozi katika kuokoa maisha na mali ili zitekeleze majukumu kwa ufanisi pamoja na kupunguza athari kwa jamii.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Uratibu na Bunge, Jenista Muhagama anawataka viongozi kujipanga na kujiandaa kukabiliana na EL-Nino endapo itatokea, ni lazima kujiratibu na kuwa na vifaa na rasilimali zingine zinazoweza kutumika wakati wa kulikabili janga hilo.

Waziri ameutaka mkoa huo kuimarisha kingo, kuainisha maeneo ambayo mara nyingi yana athari kipindi cha mvua nyingi, kusimamia matumizi sahihi ya mitaro na mifereji ya maji taka pia kujipanga kuzuia athari na kutengeneza mipango ya kuzuia madhara pamoja na kushirikisha jamii katika ulinzi wa mito isiharibiwe.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila anasema Rais Dkt Samia Suluhu Hassan hataki kuona wananchi wanapata athari za EL-Nino ndio maana ametoa maelekezo mahususi ya kujiandaa, kujipanga au kuweka mikakati ya kuzuia athari zinazoweka kutokea endapo mvua hizo zitanyesha.

Mkoa wa Dar es Salaam tayari umeshafanya maandalizi ya kukabiliana na EL-Nino ambapo tayari umeshaainisha maeneo hatarishi na kusafisha mito kwa mfano mto Msimbazi vilevile kazi inaelea kusafisha mitaro na mifereji pia kuendelea kutoa elimu kwa Umma” anasema Chalamila.

Chalamila anaeleza kuwa wameweka mikakati ya kukabiliana na mvua za El Nino ambapo anasema mvua hizo ni moja wapo ya sifa ya mabadiliko ya tabianchi kubwa au pungufu.

“Ulimwengu unakuwa hauna usawa kwas ababu vitu ambavyo vinaleta usawa ya ulimwengu vinakuwa vimeharibiwa na shughuli za binadamu na mabadiliko ya tabianchi yanapotokea kuna mambo mengi.

“Tunafikiri ni nini kinaweza kutokea kama mkoa wetu utakuwa na mvua nyingi? kwanza italeta uharibifu wa barabara, pili uharibifu wa miundombinu nyingine ikiwemo umeme ,maji na mingine kama majengo.

Chalamila anasema kuwa mvua nyingi pia zinasabababisha mafuriko na kujaa kwa mito ambayo mwisho wa siku maji yataenda kwenye makazi ya watu kwa hiyo kama hayo yakitokea wanasema hizo ni athari.
Ila athari zaidi anaeleza kuwa ni pale ambapo hayo yanapelekea vifo,kuharibika kwa majengo,kukatika kwa madaraja na mengine.

ELIMU KWA WANANCHI

Jambo la kwanza ambalo Chalamila analianisha ni kutoa elimu kwa umma kuhusu uwepo wa mvua nyingi ili kina mmoja kwa namna alivyo aweze kuhakiki nyumba yake bati,matofali na miundombinu nyingine ili mengine wananchi wanajiandaa.

Chalamila anasema pia kuna maandalizi ya kisaikolojia ambapo lazima mtu ajue kwamba kama kutakuwa na mvua atunze chakula kiasi gani.

Pia wamehakikisha kwamba wanatayarisha mapito ya maji yasiwe na mkwamo kama kuzibua mitaro pamoja na kuhakikisha maji yote yanaelekezwa mahali ambapo hayataleta athari kubwa ambapo mito imesafishwa,kuzibua mitaro na mengine.

“Tumebomoa baadhi ya majengo yaliyojengwa katika baadhi ya miundombinu inayopeleka maji mtoni kwa hiyo hizi jitihada zote tumefanya ili kupunguza maji ambayo ni mengi yasiweze kuleta athari,”anasema.

Pamoja na hayo ujenzi wa madaraja na barabara umekuwa ule wa viwango ili kukabiliana na majanga ambapo muundo wa sasa zinastahimili mafuriko.

“Lakini pia na hali itokanayo na majanga mengine tumekuwa na muundo mzuri wa madaraja yanayoweza kuwa na uwezo mkubwa wa kubeba maji yanayoweza kuleta madhara kulingana na mabadiliko ya tabia nchi,”anasisitiza.

TAHADHARI ZA ZILIZOCHUKULIWA

Chalamila anatoa tahadhari wakati huu wa mvua nyingi watu kuepuka kuvuka sehemu za maji mengi bila uangalifu hasa kwa watu ambao wamelewa kwani watasombwa na maji.

“Kuna waendesha magari anaona maji mengi na anatavuka kumbe maji yamekata daraja ,watoto wamezoea kuona maji na kuogelea kumbe ndo wanasombwa kwahiyo tunawapa elimu endelevu kwa makundi ya watu wanaopenda pombe,watoto wadogo ,kinamama,madereva na mengine wachukue tahadhari,”anasisitiza.

Aidha anasisitiza kuwa wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi yanayoweza kukumbwa na mafuriko waweze kutoka na kuhamia maeneo salama kwao.

“Watu wote wanaoishi katika maeneoa hayo mfano bonde la mto Msimbazi,karibu na bonde la mto Mpiji, Mlalakuwa , bonde la mto Tegeta, mto Ngombe wote hawa tumeshakaa kuwahamasisha kwamba maeneo hayo ni hatarishi sasa ni muda mwafaka wa kufanya makazi yao mahali pengine ambapo hapana mafuriko,”anaeleza Chalamila.

“Swali ni je wanamtaji kwa nyumba zao kuvunjwa? na kwenda kujenga maneo mengine? Ninachojua elimu hii hatujaanza kutoa leo ni muda mrefu na utakumbuka eneo la Hananasifu kuja magomeni huu upande wote la mto Msimbazi tayari zamani kulishakuwa na watu wamejenga na tayari kulishabomolewa mpaka Jangwani nyumba zilishaondelewa,” anasema.

Chalamila anasema wananchi wanaokaa kuanzia Tegeta ndevu ,kibaoni,Kibo na Bunju mwisho eneo lote hilo linapokea maji kutoka milima ya Chasimba na chatembo ambayo milima inayokinga kiwanda cha Twiga simenti wamepatiwa elimu na fedha zimetolewa kuhakikisha kuna miundombinu mikubwa ya kutengeneza miferi mikubwa maji yanayotoka katika milima hiyo.

Anabainisha kuwa hiyo ni pamoja na kuwaelekeza wananchi wote waliojenga kwenye mapitio ya maji kuanza kuruhusu njia ya maji haraka iwezekanayo.Aidha tahadhari zingine ni wananchi kufuatilia utabili wa Hali ya Hewa unaotolewa na mamlaka husika saa 24 siku 5, Siku 10 na Siku 30 na kuzingatia ushauri unaotolewa.

JIJI LA MWANZA

Wananchi wakizibua daraja la Mto Mirongo katika barabara ya Uhuru lililoziba kutokana na bidhaa na takataka zilizobebwa na mafuriko yalitosababishwa na Mvua kubwa zinazoendelea kunyesha jijini Mwanza .

Prudence Costantine, Mkurugenzi wa Maafa kutoka Idara ya Menejimenti ya maafa-Ofisi ya Waziri Mkuu anasema Serikali kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa ilitoa utabiri ulioonesha kwamba kutakua na Mvua za wastani na juu ya wastani (El Nino) kwa mikoa kadhaa nchini ukiwemo Mkoa wa Mwanza hivyo ni lazima wadau wajiandae kukabiliana nazo.

“Tunaweza tukapata maafa kama magonjwa na vinginevyo kutokana na mvua hizo na ndio maana ofisi ya Waziri Mkuu ikaona ije na mpango wa kukabiliana na maafa hayo na hadi sasa wataalamu mbalimbali wamesambaa kwenye mikoa mbalimbali kuketi pamoja na kamati za maafa za mkoa.

“Tunashauri wananchi kufuiatilia utabiri wa hali ya hewa na kuchukua hatua na wananchi wanaoishi maeneo hatarishi ni vyema wakaondoka maeneo hayo ili kuepuka madhara,’ anasema.

ARUSHA WATATUA CHANGAMOTO ZA MIUNDOMBINU

Mkuu wa Wilaya ya Karatu Dadi Kolimba, amewataka Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini ( TARURA) Mkoa wa Arusha kutatua changamoto za Miundombinu kwa kuzingatia tahadhari ya mvua za El Nino.

Anasema taarifa za mamlaka ya hali ya hewa nchini kuwepo kwa mvua hizo wanapaswa kujipanga kutatua changamoto kabla na baada ya mvua hizo. Anasma kuwa kuna shughuli ambazo zinatakiwa kufanyika kabla ya maafa lakini kunashughuli zinatakiwa kufanyika wakati wa maafa.

“Maeneo ambayo yamekuwa na changamoto mkayaweke vizuri kwa kuzibua mitaro kuweka makaravati kabla ya athari Kubwa haijatokea kwa kuhakikisha tunaisimamia vizuri ili mvua zinapokuja zisiwe na madhara makubwa” anasema.

Aidha anasema wote wana jukumu kubwa la kuhakikisha barabara zote za vijijini na mijini zimekaa vizuri ili kusaidia kusitokee maafa makubwa kupitia kamati za wataalamu kuanzia ngazi za kata wilaya hadi Mmoa ,lakini pia endapo yatatokea maafa watahakikisha wanatumia vizuri elimu zetu kuokoa ili kusije kukatokea maafa makubwa.

Hata hivyo amesema kwa Sasa wanakazi zilizofanyika na kwamba wamepokea tahadhari hizo tokea mwezi wa 7 na Kazi ya kwanza ilikuwa ni Madaraja na vivuko vyote ambapo baadhi ya changamoto wameshaanza kuchukuwa hatua kwa kutenga baadhi ya rasilimali ambazo zilikuwa watumie katika Kazi za kawaida hivyo itakapotokea wataendelea kukabiliana ili kupunguza athari.

“Mara nyingi bajeti zetu tumekuwa tunapanga kulingana na kufungua barabara mpya kutokana na vyanzo vya mfuko wa Jimbo na tozo kwa kipaumbele cha kwanza kuwa maeneo ya uzalishaji kwa kuongeza nguvu hivyo ni lazima tuwe na vipaumbele vya ujenzi ili kuondoa migogoro ambapo tumekuwa tukitoa Elimu kwa wananchi na madiwani “Alisema Mhandisi Kyando

SERIKALI YAZIELEKEZA KAMATI ZA MAAFA

Kutokana na ubairi wa TMA, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Jenista Mhagama, amezungumza na kamati za maafa katika mikoa ambayo mvua za El Nino inatarajia kunyesha na kuweka mikakati itakayosaidia kupungua madhara yatokanayo na mvua.

Mhama anawataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya mvua kubwa, baada ya Mamlaka ya Hali hewa nchini (TMA) kutoa utabiri wa mwelekeo wa mvua za msimu wa Vuli ili kunusuru maisha na mali zao ambao umeonesha uwepo wa El-Nino itakayosababisha vipindi vya mvua kubwa.

“Tunaona madhara kadhaa yanayoweza kutokea katika baaadhi ya sekta kutokana na uwepo huo wa El-Nino utakaosababishwa na mvua kubwa katika kipindi hicho ambacho kimesemwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini ni kama vile, mafuriko yatakayoleta uharibifu wa miundombinu, madhara ya kiafya, kiuchumi, kijamii na upotevu wa mali na maporomoko ya ardhi kuathiri makazi” anafafanua Waziri Mhagama

Anaongeza kusema kuwa madhara mengine yanaweza kutokea katika sekta ya mazingira ikiwa ni pamoja na uharibifu wa mashamba, miundombinu ya usafiri na shughuli zingine hususani uchimbaji madini pamoja na magonjwa ya milipuko kwa binadamu, wanyama na kuongezeka kwa wadudu waharibifu wa mazao na mimea.

Sambamba na hilo, Waziri Mhagama anasema Serikali inaelekeza kamati za usimamizi wa maafa na sekta, kushirikiana na umma kuchukua baadhi ya hatua kama vile kutambua maeneo hatarishi na yenye viashiria vya kuathirika na maafa na kuandaa mipango ya kuzuia madhara na kukabiliana na maafa endapo yatatokea pamoja na kuainisha na kuandaa rasilimali za usimamizi wa maafa kwa kila sekta kushiriki kikamilifu katika eneo lake.

Waziri Mhagama amezikumbusha kamati hizo kuchukua hatua kwa kuzingatia utabiri wa Hali ya Hewa kwa kuelimisha wananchi kwenye maeneo yao juu ya hatua za tahadhari za kuchukua ili kuokoa maisha pale ambapo jambo lolote litatokea na kukoa mali na kutoa taarifa kwa haraka sana kwa mamlaka Husika kuhusu dalili zozote za kutokea Maafa.

KAULI ZA WAKAZI WAISHIO MAENEO HATARISHI

Mto Msimbazi ulipo jijini Dar es Salaam

Khalifan Ngeyena (61), mkazi wa Jangwani jijini Dar es Salaam, anasema kuwa ni mfanyabiashara wa nazi Kariakoo kwa muda mrefu ameishi maeneo ya Jangwani tangu mwaka 1973 na kipindi hichp kulikuwa hakuna mafuriko.

Anasema kuwa miaka ya nyuma mto Msimbazi ulikuwa mdogo lakini kadri siku inavyokwenda mto huo huzidi kutanuka kiasi kwamba nyumba yake ilikuwa mbali na mto lakini sasa ipo karibu na mto jambo lililomfanya ashindwe cha kufanya licha ya kutakiwa kuhama eneo hilo.

“Hapa mimi nimeishi tangu nikiwa mvulana mdogo na wazazi wangu walitangulia mbele ya haki, lakini miaka hiyo hakukuwa na maji ambayo yalikuwa yakifika eneo hili lakini kadri miaka inavyokwenda mti unazidi kupanuka hadi nyumba ninayoishi ipo karibi na maji.

“Kuhama napenda lakini sina uwezo wa kunua kiwanja wala kujenga na ndio maana nashindwa pa kuki bilia mimi na familia yangu ingawa viongozi wa mtaa wametutaka kuhama kutokana na mvua kubwa za El Nino ili kuepuka kupoteza mali na maisha.

“Tumesikia taarifa za TMA kuhusiana na mvua kubwa na tangu nisikie na mvua kuanza kunyesha usiku silali kwani nailinda familia yangu, mfano mzuri Jumapili ya Novemba 12, 2023 mvua kubwa ilinyesha kuanzia saa 7 usiku hadi saa 7 mchana kiasi kwamba maji yalijaa na familia yangu nilihamishia gesti maeneo ya Magomeni.

“Nilichukua chumba cha gesti kimoja na familia yangu nikaimamishia huko na mimi nikabaki hapa kulinda mali kwani siku na sehemu ya kuwapeleka, hivyo naiomba Serikali ituangalie watu kama sisi ya namna ya kutupa viwanja maeneo mengine kwani tupo tayari kuhama maeneo hatarishi,” anasema Khalifan.

Naye Mwanaheri Shabani mkazi wa Kinondoni Mkwajuni (66), anasema kuwa katika kipindi cha mvua maji hujaa na kuingia ndani kwake kila mara. Anasema kuwa inapotokea mvua hupata na shida kutokana na vitu kuharibika kwa kuwa nyumba ipo bondeni hapa Mkwajuni.

“Mimi nimeishi maeneo haya muda mrefu na kiwanja nikilinunuliwa kwa bei ya sh.35,000 na wazazi wangu ambapo kipindi cha nyuma kulikuwa hakuna maji mengi na hii imetokana na mifereji kujaa takataka na kauchangia maji kushindwa kupita kirahisi na pia vitendo vya uchotaji michanga navyo vimekuwa kikwazo kikubwa,” anasema Mwanaheri.

Naye Majuto Suleiman mkazi wa Bagamoyo kijiji cha Mohoro anasema kuwa eneo hilo ni hatarishi lakini wanaishukuru Serikali kwa kuamua kuwapa viwanja ili kuhama maeneo hayo ambayo maji hujaa na kusababisha madhara kwa wakazi.

Naye Said Hamisi , anaishukuru Serikali kwa hatua kubwa ya kuwahamisha katika eneo hilo ambalo ni hatarishi na kuwapa viwanja bure ambapo amesema wataitumia nafasi hiyo vizuri kwa ajili kujenga makazi yao ya kuishi.

Hamisi anasema katika jambo kubwa ambalo Serikali imefanikiwa ni kuwatengenezea wananchi mazingira mazuri ya kuishi kwani walikuwa wanapata shida kubwa ya kupoteza ndugu zao, watoto na kupoteza mali zao wakati mafuriko yakitokea.

“Taarifa za hali ya hewa kweli tulizipata na wanakijiji wa eneo la Mhororo tulikutana na kujadiliana ya namna ya kushirikiana pindi tunapoona mvua kubwa na kuondokana maeneo haya kwenda kwa ndugu na marafiki ikiwa ni pamoja na kuhamisha mali.

“Lakini tuliwaza je utaratibu wa kuhamisha mali utakuwa endelevu na je gharama ni kubwa hivyo uongozi ukalipeleka suala hili ngazi za juu ambapo Rais Samia alisikia kilio chetu na kutoa maeneo ambayo tunatakiwa kuhamia huko,” anasema.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mongolandege, Kata ya Ukonga, Jimbo la Ukonga, jijini Dar es Salaam, Rajabu Tego, anasema kuwa baada ya kusikia taarifa za mvua za El Nino kutoka TMA alikutana na wajumbe wa nyumba kumi ambapo walianza kazi ya kutoa elimu kwa wakazi wanaoshi pembezoni mwa mto Msimbazi.

“Kuna wakazi wengi wanaishi pembezoni mwa mto Msimbazi na kila mwaka mafuriko huwakuta ambapo mvua ya mwaka juzi nyumba nyingi zilizolewa na maji na pia kulikuwa na vifo hivyo tukawashauri wakazi hao kuhama ambapo baadhi walihamia kwa ndugu na jamaa na wengine wamebaki na kueleza kuwa hawana mahala pa kwenda,” anasema.

Tego anasema kuwa kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Ukonga, Jery Silaa ambaye ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, walitoa elimu kwa wakazi hao kuhusiana na mvua za El Nino ikiwa ni pamoja na kuwapa ushauri wa namna ya kutafuta maeneo mengine ili kuondokana na athari mbalimbali.

“Kuna timu iliundwa kwa ajili ya kutoa elimuwa kwa wakazi hao baadhi walielewa na kuhama lakini wapo ambao walikaidi hivyo bado elimu inahitajika zaidi kwa wakazi waishio pembezoni mwa mto Msimbazi ambao hivi sasa unazidi kutanuka na kufika kwenye makazi ya watu.

“Tunachofikia mvua kubwa ikinyesha usiku na wakazi wakiwa wamelala hapa itakuwa shida sana kujiokoa na ndio maana tumewaelimisha kuhama maeneo hayo kutokana na utabiri wa TMA kwani vyema kuzingatia utabiri na kupunguza madhara,” anasema.

AGIZO LA SHIRIKA LA AFYA DUNIANI

Shirika la afya duniani limezitaka nchi zijiandae na athari zifuatazo za kiafya:

Uhaba wa chakula na kuongezeka kwa utapiamlo wa wastani na wa hali ya juu hasa miongoni mwa walio hatarini zaidi na Kuongezeka kwa magonjwa yatokanayo na maji kama vile kipindupindu kutokana na uhaba wa maji au mafuriko na miundombinu ya vyoo.

Athari zingine ni ongezeko la milipuko ya magonjwa yanayoenezwa na mbu kama vile malaria katika maeneo ya nyanda za juu ambayo kwa kawaida ni baridi sana, ongezeko la hatari ya Homa ya Bonde la Ufa na Kuongezeka kwa idadi ya watu walioathiriwa na magonjwa ya kuambukiza kama vile surua na uti wa mgongo

Kukatizwa kwa huduma za afya kutokana na ukosefu wa maji katika hali ya ukame au uharibifu wa miundombinu ya afya kutokana na mafuriko na vimbunga, Joto kali na ongezeko la hatari ya kutokea kwa moto wa mwituni katika baadhi ya maeneo yatakayokumbwa na ukame ni miongoni mwa athari zinazotarajiwa.

Mifumo ya hali ya hewa hali ya joto la bahari katika eneo la kati la kitropiki la Bahari ya Pacific, linatarajiwa kuendelea kuwa la juu ya wastani katika kipindi cha Novemba 2023 hadi April 2024.
Hali hii inashiria kuendelea kuwepo kwa hali ya El-Nino hata hivyo inatarajiwa kupunguza nguvu kadri tunavyoelekea mwisho wa msimu wa mvua.

Kwa upande wa Bahari ya Hindi hali ya joto la bahari la juu ya wastani inatarajiwa kuwepo upande wa magharibi mwa bahari kwa msimu wote wa mvua za Novemba hadi april 2024.

Hali kadhalika joto la bahari la chini ya wastani hadi wastani linatarajiwa kuendelea kuwepo upande wa mashariki mwa Bahari ya Hindi, hususani katika kipindi cha nusu ya kwanza ya msimu hali hii inashiria kuendelea kuwepo kwa kwa hali inayotambulika kama Positive Indian Ocen Dipole ( od ) katika nusu ya kwanza ya msimu wa mvua na baadae kupungua nguvu katika nusu ya pili ya msimu Februari hadi April 2024.

El Nino husababisha ukame pia katika baadhi ya maeneo

By Jamhuri