Na Daniel Limbe, JamhuriMedia, Geita

“Kulemaa viungo siyo kulemaa akili” Maneno haya yana akisi wazi kuwa unaweza kuwa na udhaifu wa viungo au kukosekana kwa baadhi ya viungo vya mwili wako lakini bado ukawa na akili ya kukusadia kuyafikia malengo yako kiuchumi.

Licha ya kwamba tatizo la ulemavu lipo duniani kote, vile vile nchini kwetu tunao watu wenye ulemavu wa aina mbali mbali ikiwemo ule wa Viungo, wasioona, wasio sikia,mabubu,walemavu wa ngozi(Albino),wenye changamoto ya akili, na ulemavu mwingine.

Hata hivyo jamii yetu kwa muda mrefu imekuwa ikiamini kuwa mlemavu ni mtu asiyeweza kutimiza majukumu yake kikamilifu kutokana na changamoto zake za kimaumbile hivyo kusababisha kundi hilo kuonekana kutokuwa na mchango wowote katika jamii.

Imani hiyo potofu inachangiwa na Mila na desturi mbovu ambazo zimekuwa kichocheo cha watu hao kubaguliwa kwa namna mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutopata elimu,chakula bora,afya,malazi na hata kutopewa fursa kubwa ya kutoa maoni yao.

Sababu hizo na nyingine nyingi zinatajwa kuwa sehemu ya unyanyapaa unaofanywa kwa baadhi ya walemavu wa viungo,hivyo kusababisha kundi hilo kukata tamaa na kubaki nyuma kimaendeleo.

Ni ukweli usio na mashaka kwamba bidii na maarifa katika kazi yoyote ndiyo njia kuu ya kuyafikia malengo tazamiwa, kuliko kukata tamaa na kuendelea kuwa tegemezi kwa ndugu,jamaa,marafiki, taasisi wadau na serikali kwa ujumla.

Licha ya kwamba yapo makundi mbali mbali ya ulemavu, Makala hii inajikita kuzungumzia zaidi watu wenye ulemavu wa viungo jinsi wanavyoweza kujikwamua na lindi la umaskini wa vipato na kuchangia uchumi wa Taifa iwapo utawekwa mkakati madhubuti wa kuwakwamua.

Nikutokana na msukumo wenye dhamira ya kweli katika kulithamini kundi hilo ikiwa ni pamoja na kuwapa fursa zote zinazoweza kuwakomboa ki uchumi, kisiasa na kijamii kwa kuwa kila aliye mzima sasa huenda ndiye mlemavu mtarajiwa.

Mwandishi wa Makala hii amezungumza na mlemavu wa viungo, Hamis Hamza (48) mkazi wa kijiji cha Mkuyuni wilayani Chato mkoani Geita, ambaye amepooza kwa zaidi ya miaka 30 na kwamba hawezi kusimama,kuchuchumaa wala kugeuza ubavu wake.

Anasema alipata ulemavu huo mwaka 1991 baada kuugua mguu wa kushoto kisha viungo vingine kuanza kupooza akiwa mwanafunzi wa darasa la tatu kwenye shule ya msingi Chato, hali iliyosababisha kukatisha ndoto zake za kupata elimu.

Hata hivyo haikuwa rahisi sana kuikubali hali yake,lakini kutokana na ushauri mbalimbali aliopata kwa ndugu na jamaa alilazimika kujikubali na kuendelea na maisha ya kawaida.

Pamoja na changamoto hiyo, haikuwa kikwazo kwake kuyatafuta mafanikio kwa njia nyingine kingali akiwa mgonjwa kitandani ambapo alianza kuagiza asali,na kuni kutoka vijijini kisha kuwauzia wahitaji, kabla ya kuanza shughuli ya kilimo cha mpunga kazi anayoendelea kuifanya hadi sasa.

Hamza anasema walemavu wakiwezeshwa hakika wana uwezo mkubwa wa kufanya kazi na kuinua uchumi wa familia na taifa kwa ujumla,kwa sababu siyo kila kazi inamlazimu mtu kutembea kwa miguu yake.

Anatoa mfano wa kazi za kilimo ambazo zinaweza kufanyika kwa kuajili watu wengine kuandaa shamba,kupanda mbegu hadi kuvuna mazao, kufanya biashara ya usafirishaji wa pikipiki za magurudumu mawili na zile za matatu (Bajaji).

Zingine ni ufugaji wa kisasa, uvuvi na biashara mbalimbali kulingana na fursa zilizopo kwa kila eneo walipo walemavu.

Anasema binadamu yoyote aliye hai na mwenye akili timamu, iwapo akipewa elimu ya kuzitambua fursa zinazo mzunguka maeneo yake, anaweza kuyafikia mafanikio ya kiuchumi na kuwezesha wengine.

Aidha anapingana vikali na imani potofu kwamba walemavu wa viungo hawawezi kujikwamua na lindi la umaskini huku akitolea mfano kwake kuwa mpaka sasa anategemewa na ndugu zake zaidi ya 10 ambao siyo walemavu na wengine anasomesha watoto wao.

“Mimi pamoja na ulemavu wangu kwa zaidi ya miaka 30 nikiwa kitandani na nisiyeweza hata kujigeuza nimepambana kwa bidii na maarifa yangu na sasa nina miliki nyumba, gari la kusadia shughuli zangu za shamba,nina mke pamoja na baadhi ya vitega uchumi vingine”.

Mbali na mafanikio yake,anaiomba serikali kutekeleza kwa vitendo utoaji wa mikopo kwa walemavu ili kuwaondoa kwenye lindi la umaskini uliokithiri ikiwa ni pamoja na taasisi za umma kuwatembelea na kusikiliza changamoto zao badala ya kukaa maofsini pekee.

Elizabeth Kengele (mlemavu) mkazi wa kijiji cha Kalema anasema kulemaa viungo siyo kulemaa akili, na kwamba iwapo wakithaminiwa na kuwezeshwa mitaji wanauwezo mkubwa wa kuchangia katika pato la taifa.

Anasema kila mwanadamu ameumbwa kwa kusudi maalumu la mwenyezi Mungu na amegawiwa karama kwa kadri ilivyompendeza Muumba, lakini suala la maendeleo ya kiuchumi linatokana na kuwepo kwa mazingira wezeshi,kufanya kazi kwa bidii na maarifa,muda na akili.

“Ni muhimu itambulike kuwa kulemaa viungo siyo kulemaa akili…sisi walemavu wa viungo hatujapewa fursa za kutosha katika masuala ya uzalishaji mali…mbali na kuwa na ulemavu wangu huu nimefanikiwa kujenga nyumba,ninayo familia ya watoto saba na ninaendelea kuwasomesha mwenyewe”.

“Mimi kila kukicha nawahi mwaloni kununua samaki kwa wavuvi, baadaye naingia mitaani na hiki kibaiskeli changu naanza kuwauzia wateja…faida nayoipata inanisaidia kuendesha familia yangu ikiwa ni pamoja kusaidia ndugu zangu kijijini” amesema Kengele.

Vile vile anasema kutokana na hali yake ya ulemavu na ugumu wa maisha ulisababisha ndugu zake kumzuia kuzaa ili asiteseke zaidi,lakini kutokana na kutambua kuwa hatandelea kuishi kwa kutegemea misaada ya ndugu na wasamalia wema,alilazimika kujiondoa nyumbani kwao na kuanza kuyasaka maisha yake mwenyewe.

Anamshukuru sana Mungu kwa hatua aliyonayo kiuchumi kwa kuwa hategemei tena kukaa mitaani kuomba omba misaada huku akiwasihi walemavu wengine kuacha kubweteka badala yake wajishughulishe ili kujikwamua na lindi la umaskini wa vipato.

“Wito wangu kwa walemavu waache kubweteka kwa kutegemea huruma za misaada kutoka kwa ndugu na jamaa…kikubwa wasaidiwe mitaji na waonyeshwe fursa za kiuchumi…naamini wasioweza kujiondolea umaskini wa vipato ni walemavu wa akili pekee…lakini wengine wakiwezeshwa wanaweza”amesema Kengele.

CHAMA CHA WALEMAVU

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa chama cha walemavu wilaya ya Chato,Justine Lupande, wilaya hiyo ina jumla ya watu wenye ulemavu 3,330 wakiwemo wasiosikia,wasioona,mabubu,wenye ulemavu wa akili,walemavu wa ngozi na wale wenye tatizo la viungo.

Anaitaka jamii kuachana na imani potofu kuwa walemavu wa viungo hawawezi kukuza pato la familia na taifa badala yake wasaidie kupatikana kwa mitaji itakayowainua kiuchumi watu hao.

Anasema yapo mabadiliko makubwa kwa kundi la walemavu ambapo vikundi viwili wilayani humo vyenye jumla ya watu 10 vimefanikiwa kupata mkopo kutoka halmashauri ya wilaya ya Chato,ambapo kimoja chenye watu watano kinafuga nguruwe kwenye kijiji cha Mpogoloni na kingine wamefungua studio ya kurekodi Muziki kwenye kijiji cha Katemwa Muganza.

Anatumia fursa hiyo kuiomba serikali kuongeza kiwango cha mikopo kwa walemavu kutoka aslimia mbili inayotengwa kwa kila halmashauri nchini na badala yake itengwe aslimia nne,jambo analoamini itawasaidia kubuni miradi inayoweza kuwapa tija haraka ukilinganisha na kiwango cha sasa kinachotolewa.

Baadhi ya wananchi wanasema watu wenye ulemavu ni miongoni mwa watu maskini sana katika jamii,kutokana na maisha yao kuambatana na vikwazo vya kimaumbile,kisiasa,kiafya na kielimu ambapo wengi wao hasa waliopo vijijini hufichwa ndani na kunyimwa fursa za uzalishaji mali.

Rehema Hassan,anasema serikali za mitaa haziwashirikishi walemavu katika mipango ya maendeleo kutokana na kuwachukulia kama watu wabishi na wanaopenda kuhoji kila jambo.

Sellina Magembe,anasema angalau yapo mabadiliko kidogo kwa jamii kuhusiana na watu wenye ulemavu ukilinganisha na miaka ya nyuma,ambapo ilionekana kuzaliwa kwao ni mkosi na ndiyo ilikuwa sababu kubwa ya kuwaficha ili wasijulikane kwa jamii.

Mitazamo hiyo iliambatana na kutowapa fursa za ushiriki wa kujadili mambo yao,kutokuwa na watu sahihi wa kuwasemea kwenye vyombo vya maamuzi hivyo kusababisha kundi hilo kuendelea kuwa maskini wa kutupwa ukilinganisha na hali ilivyo sasa.

Jeremiah Masambu,mkazi wa kijiji cha Kitela Chato anasema kupungukiwa viungo vya mwili au viungo kukosa nguvu siyo sababu ya mtu kuwa maskini wa kipato ispokuwa ni mtazamo hasi uliojengeka kwenye jamii,jambo linalopaswa kuepukwa kabisa.

“Ukitazama Hamisi ni mlemavu wa viungo,na ni mtu ambaye karibu maisha yake yote yupo kitandani hajiwezi lakini anayo maendeleo makubwa kutuzidi hata sisi wazima…kwangu mimi huyu ni mfano wa kuigwa kwa walemavu wengine”.

“Ni muhimu watambue kwamba hawahitaji kukaa ndani kusubiri misaada na huruma bali wanapaswa kuingia vitani kupigania ugali wa kila siku na raha zingine za Dunia” anasema Masambu.

Pendo William,mkazi wa kijiji cha Chato kati,anasema kundi la walemavu limenyimwa fursa za uwezeshwaji kiuchumi licha ya kwamba wanao uwezo wa kupambania maisha yao kimaendeleo.

“Binafsi siwachukulii walemavu kama watu wanaopaswa kuonewa huruma ili waonyeshe vipawa vyao…kikubwa wanahitaji wawezeshwe na kuelimishwa namna ya kutumia vipawa hivyo sambamba na kupewa elimu ya namna bora ya kuzitambua fursa za kiuchumi zilizopo kwenye maeneo yao”.

“Huu ni muda wa walemavu kuamka na kutambua kuwa mafanikio yanatokana na utashi na bidii ya mtu mwenyewe badala ya kujikatia tamaa na kusubiri huruma za jamii” anasema William.

“Kumbuka hata zamani wanawake walikuwa wanaonekana ni watu wa kuonewa huruma…lakini leo si unaona tuna rais mwanamke…naamini tukiondoa mitazamo isiyofaa kwa walemavu utafika wakati nao wataonekana watu pasipo huruma wala kuwekwa kwenye kundi maalumu”.

MKAKATI WA WILAYA

Ofisa maendeleo wilaya ya Chato,Vicent Bushaija,anasema mwitikio wa walemavu wa viungo kuchangamkia fursa ya mikopo ya halmashauri siyo mkubwa sana licha ya kutengwa fedha kwaajili yao.

Anasema mkakati wa halmashauri hiyo ni kuendelea kutoa elimu kwa makundi ya Wanawake,Vijana na Walemavu kujitokeza ili kupata mikopo ambayo itawasaidia kuinua pato la familia na kujiondolea umaskini.

Kadhalika kutoa kipaumbele cha mikopo kwa walemavu wanaokopa na kulejesha kwa wakati.

Kuwatembelea na kuwapa ushauri bora wa kujishughulisha na kazi ndogo ndogo badala ya kukaa nyumbani na kuwa tegemezi kwa wengine.

Kuhamasisha jamii kutowafungia ndani watoto wenye ulemavu na kwamba wanapaswa kuwapeleka shule ili wakapate elimu kama watoto wengine.

Mwenyekiti wa jumuiya ya walemavu mkoa wa Geita, Robert Kasunzu, anasema umefika wakati wa kuwathamini walemavu kwa vitendo,badala ya mipango isiyo kuwa na utekelezaji.

“Kumekuwepo na mipango mingi isiyokuwa na utekelezaji kwa watu wenye ulemavu…tunahitaji kuona kwa vitendo namna tunavyoweza kuthaminiwa ikiwa ni pamoja na kupewa ruzuku itakayotusaidia kuanzisha mitaji isiyokuwa na masharti magumu kama zilivyo pesa za mikopo kutoka halmashauri” anasema

Kutowathamini kwa vitendo ni kuendelea kuwapa unyonge kutokana na hali zao kimaumbile na kiuchumi, na kwamba serikali na wadau wengine maendeleo wanapaswa kutoa fursa muhimu kwa maslahi mapana ya walemavu na taifa kwa ujumla.

Itakumbukwa mwaka 2018 aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda,alitoa agizo kwa wenye viwanda kuguswa na maisha ya wenye ulemavu kwa kuwapa ajira ili waweze kufurahia maisha yao kama ilivyo kwa watu wengine.

Kauli hiyo aliitoa kwenye uzinduzi wa Taasisi ya kusaidia watu wenye ulemavu ya “Dr. Reginald Mengi Parsons with Disabilities Foundation”,ambapo aliyekuwa mkurugenzi wa makampuni ya IPP marehemu Dkt. Mengi aliahidi kutoa shilingi bilioni 5 ili kuunga mkono jitihada za mkuu wa mkoa huo kutaka kuanzisha kiwanda kitakacho ajili watu wenye ulemavu.

SERA YA TAIFA

Kwa mujibu wa sera ya taifa ya Maendeleo na huduma kwa watu wenye ulemavu( National Disability Policy) iliyoidhinishwa na Baraza la Mawaziri mwezi julai 2004,inasisitiza utoaji fursa sawa kwa watu wenye ulemavu.

Kauli mbiu katika sera hiyo ni Maendeleo na watu wenye ulemavu, ikiwa na lengo la kuhimza utolewaji wa huduma bora kwa kuzingatia usawa kwa walemavu.

Pia inahimiza ushiriki wa watu wenye ulemavu kwenye maendeleo ya nchi hususani katika mipango ya kupunguza umaskini katika ngazi zote.

Sera na sheria mbali mbali zinazohusu wenye ulemavu zitasaidia kuboresha fursa za ajira,kupiga vita ubaguzi na kuwawezesha watu hao kuishi maisha yenye hadhi.

Sambamba na hilo,itawawezesha kushiriki katika shughuli za kiuchumi,kijamii na kisiasa kama ilivyo kwa watu wengine.

NINI KIFANYIKE

Jamii iache kuwatia unyonge walemavu kuwa wao hawawezi na wanastahili huruma na misaada au kwenda barabarani kuombaomba.

Walemavu watambue wanao uwezo wa kupambania maendeleo yao ili kujiondolea umaskini wa vipato.

Maofisa maendeleo ya jamii kuanzia ngazi ya kata wawafikie watu wenye ulemavu na kuwaelimisha kuzitambua fursa za kiuchumi zilizopo maeneo yao.

Ndugu na jamaa za watu wenye ulemavu wasiwafiche ndani walemavu badala yake wawatie moyo wa kupambana kuyatafuta maendeleo.

Serikali iwekeze mitaji kwa watu wenye ulemavu jambo litakalosaidia kuwaondolea unyonge walionao.

Mipango ya maendeleo kuanzia ngazi ya kitongoji,kijiji,kata,tarafa,wilaya,mkoa na taifa kwa ujumla iwape kipaumbe walemavu kama ilivyo kwa kundi la wanawake.

Mbali na kuwa haki za watu wenye ulemavu zinatambuliwa vizuri katika sera,ni muda muafaka vitendo vionekane badala ya kuwa na mipango isiyokuwa na utekelezaji.

Jamii itambue kila aliyemzima leo huenda ndiye mlemavu mtarajiwa.

             

By Jamhuri