Na Suzy Butondo, JamhuriMedia, Shinyanga

Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa mkoani Shinyanga, Donasian Kessy amewataka wananchi kujihadhali na wimbi la matapeli lililoibuka hivi karibuni,ambalo limekuwa likitapeli watu kwa kutumia simu za mkononi.

Tahadhali hiyo ameitoa leo wakati akitoa taarifa ya kipindi cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2023/2024 kwa vyombo vya habari leo Februari 7,2024, ambapo amewataka wananchi kuwa makini na matapeli wanaopiga simu za mkononi na kudai wao ni maafisa wa serikali na kudai wasaidiwe kuwa wamepatwa na changamoto mbalimbali wakiwa kazini.

Donasian amesema matapeli hao wamekuwa wakiwapigia simu watu mbalimbali kwa kudai wamefiwa,ama wameharibikiwa na gari wakiwa kazini, hivyo amewaomba watu wanaopigiwa simu hizo watoe taarifa katika ofisi za TAKUKURU ili waweze kufuatiliwa na wachukuliwe hatua za kisheria.

“Hivi karibuni mtu mmoja amenipigiasimu anadai yeye ni afisa wa serikali hapa Shinyanga kwamba ameharibikiwa na gari wakati akitokea Dodoma tumtumie shilingi laki moja, baada ya kutaja jina nilishtuka maana aliyemtaja kwa wakati huo nilimuacha ofisini,hivyo nikawaambia hatuna afisa kama huyo.

“Hivyo namba za tapeli huyo tunazo tunazifuatilia ili kufahamu huyu mtu yuko sehemu gani na ninani anayefanya utapeli huu na akibainika atachukuliwa hatua za kisheria, pia tuwaombe wananchi wote, pale wanapogundua miradi ya maendeleo haiko vizuri watoe taarifa katika ofisi za Takukuru”ameongeza Kessy.

Aidha Takukuru Mkoa wa Shinyanga ilifanya ufuatiliaji wa miradi ya SEQUIP (Mpango wa Uboreshaji wa elimu ya Sekondari) ili kuona kama miradi inatekelezwa kwa wakati na katika ubora na viwango vinavyotakiwa, ambapo ilionekana miradi hiyo imetekelezwa kwa ufanisi na ubora.

“Katika mwaka wa fedha 2022/2023 Mkoa wa Shinyanga ulipokea shilingi Bilioni 5.2 fedha hizi zilikuwa ni kwa ajili ya ujenzi wa miradi 13 ambayo ni shule mpya sita za sekondari, ujenzi wa nyumba sita 2 in 1 za walimu na ujenzi wa shule ya wasichana ya mkoa ambapo ilifatilia na kukuta miradi hiyo ikiwa imetekelezwa kwa ufanisi na ubora ”,amesema Kessy.

Aidha amesema walifuatilia miradi miwili ya sekta ya afya inayotekelezwa katika halmashauri ya wilaya ya Msalala yenye thamani ya shilingi Milioni 700 ambapo dosari ndogo ndogo zilibainika kwenye miradi na ushauri ulitolewa wa kutatua dosari hizo.

Hata hivyo Takukuru ilifanya chambuzi tano za mfumo wa matumizi ya fedha za Tasaf, utoaji wa huduma katika sekta ya ardhi kupitia mabaraza ya ardhi na nyumba, matumizi ya stakabadhi za EFD kwa wazabuni wanaofanya biashara na halmashauri, katika halmashauri ya za Kahama, Shinyanga na Kishapu ambapo walikuta changamoto ndogo ndogo zinaendele kufanyiwa kazi.