*Watumia taarifa walizopewa na JAMHURI kutaka kuuzima ukweli

*Kamanda wa TAKUKURU Arusha amchuuza Mhariri, amlengesha

*Ashiriki ubambikiaji kesi huku mtuhumiwa akitamba kuiweka mfukoni Serikali

*Naibu Mkurugenzi Mkuu bila kusikiliza asema kesi iendelee, ni jinai

ARUSHA

Na Mwandishi Wetu

Katika hali ya kusikitisha, Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Arusha, James Ruge, ametumia dhamana aliyopewa na taifa kushiriki kukandamiza haki za wanyonge, JAMHURI limebaini.

Tukio hilo limetokea Desemba 26, mwaka jana wakati JAMHURI likifuatilia sakata la ujangili unaodaiwa kufanywa na mfanyabiashara wa uwindaji wa kitalii mwenye asili ya Kiarabu, Saleh Salim Al Amry, mkazi wa Arusha.

Al Amry anadaiwa kuwaingiza nchini watalii wa uwindaji kutoka Saud Arabia mwaka 2019, ambao pamoja naye, waliwinda na kuua wanyama na ndege ambao hawamo kwenye orodha ya ‘wanyama wanaoruhusiwa kuwindwa’ kisheria, huku wakipiga picha zaidi ya 100.

Wakati wa kufuatilia taarifa hizo, JAMHURI lilimtafuta Al Amry kwa njia ya simu kwa wiki kadhaa kupata kauli yake kuhusu tuhuma zinazomkabili bila mafanikio, ila kwa alichokijua moyoni mwake, akaomba mwandishi wa JAMHURI akutane naye ofisini kwake Arusha, badala ya kutoa majibu kwenye simu.

Ijumaa ya Desemba 24, 2021 Al Amry alipopokea simu kwa mara ya kwanza na kuzungumza na mwandishi wa JAMHURI jijini Arusha, Hyasinti Mchau, alimuomba kabla ya kujibu maswali atumiwe picha hizo.

Maswali ya JAMHURI kwa Al Amry yalikuwa kwanza kutaka kufahamu iwapo anazitambua picha tulizonazo; pili, kama wakati wa uwindaji huo walikuwa na leseni za kuua nyati na simba; tatu, kufahamu ni mwindaji mahiri yupi (Professional Hunter – PH) aliyekuwa naye wakati wa uwindaji na swali la mwisho lilikuwa ni ukweli kuhusu kuhojiwa kwake kwa kukutwa na kiwango kikubwa cha madini ya tanzanite na dhahabu.

Dakika chache baadaye Al Amry alitumiwa picha, na Mchau anasema: “Alipopokea picha akanipigia simu akitaka tukutane ofisini kwake Jumapili asubuhi (Desemba 26, 2021).”

Baada ya hapo Mchau akapiga simu ofisi za JAMHURI, Dar es Salaam kuomba uchapaji wa habari kuhusu ujangili unaodaiwa kufanywa na Al Amry kusubiri hadi watakapokutana kupata maelezo ya upande wake na kupata majibu kama sehemu ya haki ya asili ya mtu anayetuhumiwa kwa lolote, JAMHURI kitaaluma lilisitisha kwa muda habari hiyo.

Kwa kutambua unyeti wa mkutano kati ya Mchau na Al Amry pamoja na mustakabali wa masuala ya ujangili nchini, JAMHURI likaona ni vema taasisi nyeti za serikali zikashirikishwa. Hii ilikuwa ni baada ya kupata taarifa za ujahili wa Al Amry kuwa hutumia baadhi ya watu ndani ya vyombo vya dola kubambikia wananchi kesi.

JAMHURI liliamua kuishirikisha TAKUKURU Mkoa wa Arusha inayoongozwa na Kamanda Ruge kwa kuwasiliana naye. Katika kuweka kumbukumbu, JAMHURI liliamua kutumia WhatsApp, Ruge akatumiwa ujumbe unaosomeka hivi:

“Salamu Kamanda. Nakusalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania… Taarifa;

Kuna Mwarabu anajulikana kwa jina la Saleh Salim Al Amry. Background ya huyu mtu ni mwanajeshi aliyepigana vita ya pili ya Saddam Hussein upande wa United Arab Emirates (UAE) akitokea jeshi la Yemen.

“Huyu mtu amehamia Tanzania na anaishi Arusha. Amekuwa mwiba kwa serikali na nchi, akihujumu uchumi kwa njia ya ujangili akiwa amewaweka viongozi wengi kwenye ‘payroll’ yake.

“Huyu mtu ameua wanyama wengi sana ambao hawaruhusiwi kuwindwa. Tumekuwa tukitoa taarifa zake kwa kuandika, lakini haguswi!

“Tunazo taarifa za ujangili alioufanya za kuua wanyama na ndege aina ya ‘kori bustard’, majike ya swala, simba wadogo, nyati na nyumbu Desemba 2019. Nakutumia picha.

“Gazeti la JAMHURI limemhoji kuhusu hizo picha. Amemwita mwandishi [wetu] ofisini kwake Jumamosi saa tatu asubuhi [baadaye ikasogezwa mbele hadi Jumapili saa tatu asubuhi].

“Angalizo tu, ndiyo maana ninakupa taarifa asije kumfanyia mchezo mchafu, kumbambika rushwa kwa nguvu kwa kupitia TAKUKURU. Tuna taarifa huyu Mwarabu anawatafuta maofisa kutoka ofisini kwako ili mwandishi atakapofika, wampachikie kesi kinguvu.

“Nimekupa taarifa tu ‘in advance’ lakini huyu mwandishi ni lazima aende siku hiyo kwa kuwa Jumanne lazima tuiambie serikali mali za nchi zinavyomalizwa.”

Ruge akajibu kwa kifupi: “Nikushukuru sana ndugu yangu kwa taarifa hii.”

Ruge abadilika ghafla

Mkutano kati ya Al Amry na Mchau ulimalizika kwa muda mfupi baada ya maofisa wa TAKUKURU kuingia ofisini kwa Al Amry na kumkamata Mchau kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa (kesi ipo mahakamani).

Baada ya tukio hilo ambalo JAMHURI ililitarajia na siku mbili kabla kumpa taarifa Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Arusha, Ruge, Mchau akapelekwa ofisini na kuhojiwa kwa muda mrefu.

Ruge alipotafutwa na Mhariri wa JAMHURI kuomba aingilie kati suala hilo kwani analifahamu kwa kuwa alijulishwa mapema, mazungumzo yalikuwa hivi:

Ruge: Mimi niko Namanga, nje ya ofisi kikazi. Kwa kawaida sisi tukitoka nje ya ofisi tunakaimisha kila kitu. Kwa hiyo, wasiliana na ofisi watakusaidia.

Mhariri: Nimewasiliana nao na wanasema wanasubiri kauli yako tu, wamuachie kwa dhamana hadi kesho.

Ruge: Ni nani anasema hivyo?

Mhariri: Ofisa mmoja anaitwa Rama (aliyeshiriki kumkamata Mchau).

Ruge: Nimekwambia kwa utaratibu wetu (TAKUKURU) nikiwa nje ya ofisi siwezi kutoa maelekezo hayo. Wapo maofisa pale ofisini wanaoweza kukusaidia.

Mhariri: Mimi nadhani hutaki tu kutusaidia. Umeamua kututesa. Lakini tulifahamu tangu awali kwamba mwandishi angeshikishwa rushwa!

Ruge: Kama ulifahamu ni hatua gani ulichukua kuzuia kitendo hicho kisitokee?

Mhariri: Hatua niliyochukua ni kukutaarifu wewe! Sasa ni nani mwenye dhamana ya kuzuia na kupambana na rushwa zaidi yako? Tulikutaarifu lakini sasa umeamua kututesa. Ninaamini kuna sehemu haki haijatendeka. 

Ruge: Hebu tusubiri hadi kesho.

Hata hivyo, wakati Ruge akidai kuwa Namanga, JAMHURI linafahamu kuwa ni yeye ndiye aliyeelekeza kukamatwa kwa Mchau bila kujali ‘tahadhari’ aliyopewa na JAMHURI awali.

JAMHURI linafahamu pia kwamba wakati maofisa wa TAKUKURU waliokuwa na Mchau kwenye gari dogo wakifuatana na Al Amry aliyekuwa na gari namba T 438 DSS aina ya Arphard wakiwasili ofisi za TAKUKURU, Ruge alikuwapo!

“Wakati mahojiano yakiendelea Ruge alikuwapo. Nilimuona,” anasema Mchau.

Akizungumzia kitendo alichokifanya Ruge, mwanasheria mkazi wa Morogoro na wakili wa kujitegemea, Everist Mnyele anasema:

“Ni kitendo kibaya kabisa kufanywa na ofisa aliyepewa dhamana na mamlaka ya kuzuia rushwa. Haya ni matumizi mabaya ya madaraka (ofisi). Kwa nini amkamate mtoa taarifa? 

“Makosa ya matumizi mabaya ya madaraka ni mabaya kwa kuwa yanawaumiza wanyonge na ndiyo maana huwa hayamo kwenye msamaha wa Rais. Sasa ninyi waandishi mnapo pa kusemea, mtu wa kawaida atafanya nini kama aliyepaswa kumlinda amemgeuka?”

Mwindaji Mahiri (PH) anayemfahamu vizuri Al Amry ameliambia JAMHURI kuwa ilikuwa ni hatari sana mwandishi kwenda ofisini kwake.

“Huyu jamaa ni ‘mafia’. Ningefahamu mapema ningemkataza Mchau asiende. Ni hatari sana. Halafu fedha zake huwa kama zina mashetani. Akimpa mtu anakuwa kama zezeta. Anafanya chochote bila hata kutumia busara ya kawaida,” anasema PH huyo ambaye ni mtu wa karibu na Al Amry.

JAMHURI limemtafuta Kamanda wa TAKUKURU, Kamishna Salum Hamduni, likamtumia picha za wanyama na ndege waliouawa na majibu ya Kamanda Ruge, yeye akasema: “Nipo likizo, mtafute Naibu Kamanda.”

Kamishna Hamduni, alimtumia Mhariri wa JAMHURI namba ya Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Neema Mpembe Mwakalyelye, aliyemwachia ofisi. 

Mhariri wa JAMHURI alipompigia simu Naibu Mkurugenzi wa TAKUKURU, Neema, alipokea simu akamsikiliza huku akisikika akizungumza na kuwajibu watu wengine (waliokuwa ofisini kwake), baadaye bila hata kulipa uzito suala aliloelezwa akasema: “Hiyo ni jinai, hatuwezi kufuta kesi, acha kesi iendelee na ushahidi utamtoa ikiwa hana hatia.”

Alitoa majibu hayo baada ya awali kumuuliza Mhariri: “Wewe ulikuwapo?” Mhariri alimweleza kuwa mbali na Mchau aliyebambikiwa kesi, kulikuwapo mtu wa pili aliyeshuhudia unyama huo. Akasema yeye hawezi kuingilia suala ambalo ni jinai.

Baada ya majibu hayo, Mhariri wa JAMHURI alimwambia Neema: “Naibu Mkurugenzi, kwanza naomba ufahamu kuwa mbali na uandishi mimi ni Mwanasheria. Unafahamu kwa nini sheria iliweka mkondo wa ‘Administrative Law’? 

“Hivi kweli mwandishi wetu amebambikiwa kesi, unataka ahangaike mahakamani miaka mitatu hadi mitano, kisha ithibitike kuwa hakuwa na kosa?

“Lakini pia, ndiyo maana ninyi viongozi mpo. Hivi kweli nakueleza kuwa watu wenu Arusha wametenda kinyume cha maadili na sheria za kazi, bila kunisikiliza unanipa majibu mepesi tu, na kutetea watu walioko ofisini wanaofanya uhalifu wakati ninyi TAKUKURU mnapaswa kuchunguza kila taarifa mnayopewa kwa mujibu wa sheria?”

Baada ya kumwambia hivyo, sauti yake ikabadilika kidogo akawa mpole, ila akasema: “Basi, fuata utaratibu wa kuwasilisha malalamiko dhidi ya hao maofisa nasi tutafuatilia kama yatakuwa na mashiko.” 

Baada ya hapo, Mhariri alikata simu kwa masikitiko juu ya usikivu wa ofisi hii ya umma.

Taarifa zilizolifikia JAMHURI zinasema, Al Amry yupo anatamba kuwa yeye ameiweka mfukoni serikali na anaweza kuingia ofisi yoyote akafanya lolote bila kuchukuliwa hatua yoyote hapa nchini. 

Mmoja wa watu waliokuwa wamekaa naye juzi, amemkariri akisema: “Mimi nakwambia hata huyo Ruge nikitaka kumwondoa hapa Arusha namwondoa. Acha kumwondoa, hata nikitaka kumfunga namfunga, sembuse hawa waandishi wa magazeti! Watapiga kelele sana na hakuna kitakachobadilika zaidi ya wao kuumia.” 

JAMHURI linaendelea kufuatilia katika vyombo vya dola na watendaji wa serikali kushuhudia mwisho wa upatikanaji wa haki Tanzania na ulinzi wa rasilimali za umma iwapo wanalindwa wenye mali au watetezi wa haki.

Ujangili Simanjiro walaaniwa

Taarifa zinadai kwamba mauaji ya kikatili kwa wanyamapori yaliyofanyika mwanzoni mwa Desemba 2019, siku chache kabla ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti, kushinikizwa na Al Amry kuunda kamati ya uchunguzi, kamati hiyo iliyoundwa kinyume cha sheria na utaratibu wa utawala bora Desemba 6, 2019, ililenga kuficha uovu wa Al Amry na genge lake na kuelekeza lawama kwa Kampuni ya HSK Safaris inayomiliki Pori Tengefu la Simanjiro mkoani Manyara.

Genge linalodaiwa kufanya ujangili chini ya Al Amry hufadhiliwa na tajiri kutoka Saudia anayefahamika kwa jina la Al Rajhi.

“Vitendo viovu vya Al Amry ni vingi sana, lakini yeye ni bingwa wa kuvifukia kwa kutumia kila anachokiita ‘pesa ndogo ndogo’,” anasema mkazi wa Kata ya Emboret, Simanjiro anayehofia usalama wake na familia iwapo jina lake litatajwa gazetini.

Anasema maeneo ya mashambani huko Emboret ni sawa na ‘uwanja wa mapambano’ kati ya wanyamapori na genge la Al Amry na tajiri wake Al Rajhi ambapo wanyama husumbuliwa na kuuawa hovyo bila leseni wala kufuata utaratibu. 

“Safari moja tu ya uwindaji wa kinyemela wanaua mamia ya wanyama na ndege. Unadhani serikali hupoteza kiasi gani cha mapato?

“Tukilalamika serikalini (hasa TAWA), uchunguzi unaanza kwa nguvu lakini unaisha ghafla tu. Hii inauma sana kwa kuwa mwanakijiji akikamatwa na digidigi mmoja wa kitoweo, anashushiwa balaa kubwa wakati hawa jamaa wanaachwa tu. Hii ndiyo Tanzania aliyoiacha Nyerere kweli?

“Waarabu wanaokuja kuwinda Tanzania ni matajiri, wana uwezo mkubwa wa kifedha. Lakini wanataka au wanasaidiwa kuwinda wanyama na akina Al Amry bila kulipia.

“Hivi yupo Mtanzania anayeweza kwenda kuiba mafuta Uarabuni? Hawa Waarabu wenyewe kwao hawawezi kufanya wanayoyafanya huku. Watanyongwa asubuhi kabisa,” anasema mwananchi huyo akilaani ujangili huo.

Pamoja na habari hizi, zinaambatanishwa picha mbalimbali za wanyama na ndege alioua, huku akiwatesa wanaojaribu kuanika habari zake.

By Jamhuri