TAKUKURU watakiwa kuifanyia kazi ripoti ya CAG

Na Kija Elias,JamhuriMedia,Moshi

NAIBU Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Deogratius Ndejembi, amewataka maafisa wa Takukuru nchini kuhakikisha kwamba ripoti ya ukaguzi iliyofanywa na CAG na kukabidhiwa kwao inafanyiwa kazi haraka iwezekanavyo.

Kauli hiyo ameitoa jana mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, wakati akifunga mafunzo ya awali ya maafisa uchunguzi 553 wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), yaliyofanyika katika shule ya Polisi Tanzania Moshi.

Ndejembi amesema Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali CAG, amekwisha kutoa ripoti yake kwa Makamanda wa Takukuru, hivyo akawataka maafisa hao kwenda kuziangalia ripoti hizo na kuzifanyia kazi kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha wanaokoa fedha za Watanzania ambazo zimekuwa zikipigwa na baadhi ya watendaji wasio waaminifu kupitia manunuzi ya vitu mbalimbali kupitia zabuni wanazotitangaza.

“Ninyi wahitimu wa mafunzo ya awali kwa watumishi waajiriwa wapya kwa mwaka 2022 mnawajibika kwenda kuhakikisha mnasimamia masuala haya yote ya matumizi ya fedha za miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali kupitia taasisi yenu ya Takukuru,”amesema.

Aidha Ndejembi amewataka maafisa uchunguzi na maafisa uchunguzi wasaidizi kulinda heshima ya taasisi hiyo katika misingi ya maadili na uzalendo na kwamba hatarajii kusikia mtumishi aliyeletwa kwenye halmashauri na wilaya, analewa pombe kupindukia na kurudi nyumbani alfajiri.

“Tunawataka mkawe kioo kwenye jamii ambayo mtakuwa mkiishi huko, nendeni mkawe mabalozi wazuri wa taasisi yenu,”amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa (TAKUKURU) CP Salum Hamduni, amesema Rushwa ni tishio kubwa la kiusalama, rushwa ina matokea hasi kwa usalama wa nchi, kama itaachiwa kuendelea kufanyika.

Amesema kutokana na mafunzo ambayo wameyapata na maafisa hao na mengine ambayo wataendelea kuyapata yatasaidia sana katika kuimarisha nguvu katika kupambana na rushwa nchini.

“Serikali imekuwa ikisisitiza sana ukusanyaji wa mapato lakini kuna mianya mingi ya uvujaji na upotevu wa mapato ya serikali, vitendo vya ubadhilifu, wizi wa fedha na mali za umma, niwatake maafisa hawa nendeni mkalisimamia hili hakikisheni mnakwenda kusimamia kikamilifu fedha hizo,”amesema CP Hamduni.

Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu amesema mkoa umepokea kiasi cha Sh bilioni 350 na kati ya fedha hizo Sh bilioni 78 ni fedha za miradi ya maendeleo na kuwataka maofisa watakaopangiwa katika mkoa huo kuhakikish miradi inayojengwa inaendana na thamani ya fedha hizo.

Mafunzo ya awali ya uchunguzi kwa watumishi waajiriwa wapya kwa mwaka 2022 yamehitimishwa ambapo jumla ya maafisa uchunguzi wa Takukuru 553 wamehitimu mafunzo hayo na kati yao wanaume wakiwa 376 na wanawake 178.