Chama cha Waandishi wa Habari wanawake Tanzania (Tamwa) wameandaa soko la wazi litakalofanyika Dunga katika viwanja vya ofisi za Halmashauri, Jumamosi Septemba Mosi kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 11 jioni.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari leo Agosti 30 na Mkurugenzi wa TAMWA Zanzibar, Mzuri Issa imesema soko hilo la wazi ni la tatu na litakuwa likifanyika kila mwisho wa mwezi.

“Litakuwa soko la wazi la tatu linalofanyika kila mwisho wa mwezi ili kuwahamasisha wajasiriamali wadogo kutengeneza bidhaa zenye ubora na kupata masoko,” imesema taarifa yake.

Mzuri amesema Soko la mwanzo lilifanyika  Juni 23 mwaka huu eneo la Chwaka wilaya ya Kati, la pili lilifanyika Dunga  Julai 28 na hili ni la tatu.

“Katika maonyesho ya Dunga, Septemba Mosi vikundi 4 vya wajasiriamali wanawake vitashiriki na kuonyesha bidhaa za kilimo; mbogamboga, mbolea na miche ya mazao aina mbalimbali,” imesema.

Imesema kwa upande wa ufugaji kutakuwa na bidhaa zitakanazo na ng’ombe kama vile maziwa safi, ya mgando na samli.

“Huu ni mwendelezo wa dhamira ya kuwawezesha wanawake kiuchumi ya mradi unaosimamiwa na TAMWA Zanzibar kwa udhamini wa Zanzibar Milele Foundation (WEZA II) ambao umewafikia wanavikundi wanawake takriban 7,000 kati ya hao 4,000 wako Unguja na miongoni mwao 1,600 wanatoka Wilaya ya Kati Unguja,” imesema taarifa hiyo

Please follow and like us:
Pin Share