Arusha

Na Mwandishi Wetu Jamhuri Media Arusha

Fedha zilizotolewa na serikali kupambana na athari zilizoletwa na ugonjwa wa virusi vya korona (Uviko – 19) nchini kwa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), zimesababisha ongezeko la idadi ya watalii.

Mwaka jana, Serikali ilitoa Sh bilioni 90 kwa Wizara ya Maliasili na Utalii, ambapo wizara hiyo ikapeleka Sh bilioni 49 TANAPA kusaidia kuboresha miundombinu ya hifadhi iliyoathiriwa na UVIKO – 19 mwaka 2020/21.

Na sasa imeelezwa kuwa fedha hizo zimeleta neema ya ongezeko la watalii kufikia 1,617,796 na kuingiza mapato ya zaidi ya Sh bilioni 324; ikiwa ni zaidi ya mara sita ya fedha zilizotolewa.

UVIKO – 19, ugonjwa ulioitikisa dunia, ulisababisha anguko la idadi ya watalii Tanzania na kuathiri kwa kiasi kikubwa shughuli za uhifadhi na utalii nchini.

Fedha zilizotolewa na serikali sasa zimeiwezesha TANAPA kuboresha miundombinu mbalimbali ndani ya hifadhi na matunda yake sasa yanaonekana.

Manufaa hayo yamekwenda sanjari na mwaka mmoja baada ya uzinduzi wa filamu ya Royal Tour kwa ajili ya kutangaza duniani vivutio vya utalii vya Tanzania; filamu ambayo pia imesaidia kuleta watalii.

Filamu ya Royal Tour ‘iliyochezwa’ na na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan mapema mwaka 2022 na kuonyeshwa ndani na nje ya nchi, imeongeza chachu katika sekta ya uhifadhi na utalii.

Akizungumza jijini Arusha hivi karibuni, Kamishna Mkuu (CC) Uhifadhi TANAPA, William Mwakilema, amesema ndani ya mwaka mmoja tangu kuzinduliwa filamu ya Royal Tour, idadi ya watalii waliotembelea hifadhi za taifa nchini imeongezeka.

“Tumepokea watalii 1,617,796 huku shirika likiingiza mapato ya zaidi ya Sh bilioni 324. Hii ni baada ya uboreshwaji wa miundombinu mbalimbali ndani ya hifadhi zetu,” amesema Mwakilema.

Kamishna Mwakilema amesema kabla ya kupokea fedha za Uviko-19, miundombinu ndani ya hifadhi kadhaa ilikuwa imeharabika kwa sababu mbalimbali ikiwemo mvua kubwa zilizonyesha katika maeneo ya hifadhi.

“Miundombinu iliyoboreshwa ni pamoja na mawasiliano ya barabara, viwanja ya ndege, malango ya kupokelea wageni wanapowasili na kuondoka, nyumba za watumishi, mitambo ya kujenga barabara, magari na maeneo maalumu ya uokozi inapotokea dharura au ajali,” amesema.

Hifadhi zilizonufaika na fedha hizo ni Tarangire, Mkomazi na Saadani ambazo zimeboreshewa viwanja vya ndege na malango ya kupokelea watalii.

Miundombinu iliyoboreshwa katika hifadhi za Katavi, Nyerere, Mkomazi, Saadani, Serengeti na Mlima Kilimanjaro ni barabara pamoja na nyumba za watumishi.

“Nichukue fursa hii kwa niaba ya TANAPA kumshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea fedha za Uviko – 19 kwa kutambua mchango wa sekta ya uhifadhi na utalii ambayo ni moja ya sekta nyeti kwa Taifa letu,” anasema Kamishna Mwakilema.

Ongezeko la Watalii na Mapato

Akitoa mchanganuo kuhusu ongezeko la watalii na mapato katika kipindi cha mwaka mmoja, Kamishna Mwakilema amesema Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA) imepokea watalii 259,789 walioingiza Sh bilioni 78.273.

“Pia katika kipindi hicho, Hifadhi ya Serengeti ilipokea watalii 491,375 ambao waliingiza mapato ya Sh bilioni 156.964,” amesema Kamishna Mwakilema.

Amesema hifadhi nyingine zilizobaki ambazo miundombinu yake iliboreshwa kwa fedha za UVIKO-19 zilipokea watalii 866,632 ambao waliziingizia hifadhi hizo kiasi cha Sh bilioni 89.533.

Kauli za Wadau

Akizungumzia ongezeko la watalii nchini, Mtendeji Mkuu wa Chama cha Mawakala wa Utalii Tanzania, Sirili Akko, anasema wadau wa utalii wanatambua kazi kubwa iliyofanywa na serikali ya Rais Samia na

taasisi zake kuweka mazingira rafiki kwao kufanya biashara ya kuwahudumia watalii kwa ufanisi na ubora unaotakiwa.

“Na filamu maarufu ya Royal Tour imekuwa chachu muhimu sana ya ongezeko la watalii na biashara ya bidhaa za utalii kurudi kwa kasi kufuatia ongezeko la watalii,” amesema Akko.

Kwa upande wake, Mshauri wa Masuala ya Mazingira, Uhifadhi na Utalii, Dk. Victor Runyoro, ametoa angalizo kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia taasisi zake ifanye utafiti wa kitaalamu kujua jinsi watalii wanavyopata taarifa ya vivutio vya utalii na kabla ya kufanya uamuzi wa kuvitembelea.

“Matokeo ya utafiti huo yatasadia kujua ni kwa njia gani taarifa za vivutio vyetu vya utalii huwafikia watalii kutoka nchi mbalimbali ili nguvu ya kutafuta masoko ipelekwe eneo husika na kupunguza gharama za kutafuta masoko,” amesema mtaalamu huyo mbobezi.

Utalii ndiyo sekta inayoongoza kwa kuliingizia taifa fedha za kigeni na ni ya pili katika mchango wa pato la taifa (GDP) kwa asilimia 17. Pia imetoa ajira rasmi na zisizo rasmi kwa zaidi ya Watanzania 2,000,000.

By Jamhuri