Na Stella Aron,JamhuriMedia

Kutokana na ukame unaoikumba nchi, mabwawa ya kuzalisha umeme ya Hale, Kihansi, Nyumba ya Mungu na Pangani yenye uwezo wa kuzalisha megawati 266 za umeme yamepungua uwezo wake na kwa sasa yanazalisha megawati 34 za umeme tu hivyo kuathiri upatikanaji wa umeme wa kutosha katika sehemu mbalimbali za nchi hususani mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Tanga.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kurugenzi na mahusiano kwa umma TANESCO imesema kuwa kutokana na ukame huu mkubwa mikoa hii inalazimika kupata umeme wake kutoka katika vituo vya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia vilivyopo Dar es Salaam.

Aidha kutokana na kuongezeka kwa kasi kwa shughuli za uchumi na viwanda katika mikoa hiyo njia za kusafirishia umeme kutoka Dar es Salaam kwenda kwenye mikoa hiyo zimezidiwa na hivyo kusababisha umeme unaopatikana katika mikoa hiyo kutokidhi mahitaji.

Ili kutatua kadhia hii shirika linachukua hatua kujenga njia mpya kutoka kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Luguruni ili kuhudumia maeneo yote ya Luguruni mpaka Chalinze na hivyo kutoa nafasi ya umeme mwingi zaidi kufika katika mikoa yta Arusha, Kilimanjaro na Tanga.

Hii itasaidia kupunguza mzigo wa umeme katika njia sasa inayotoka Ubungo hadi Chalinze na hivyo kuruhusu umeme mwingi kwenda katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Tanga.

Pia kujenga njia moja kutoka kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Lemugrul kilichopo Kisongo Jijini Arusha.

Hatua hii itapunguza mzigo wa umeme unaopita kwenye kituo cha Njiro hivyo kuongeza kiasi kingine cha umeme kufika katika mikoa Kilimanjaro na Tanga kupitia Arusha na kutafuta tatizo la sasa la Arusha ambapo kituo cha Njirio kinapitisha mahitaji katika Mkoa wa Arusha.

Hali ya ukame mkubwa ilitabiriwa kutokea mwaka huu na shirika limechukua hatua za kuongeza uzalishahi wa umeme vituo vyake vya gesi, kazi katika upanuzi wa kituo cha Kinyerezi 1 imefikia ukingoni na inategemewa kuikamilika kabla ya mwisho wa mwaka huu ili kuingiza megawati nyingine 185 katika gridi ya Taifa.Megawati 90 kati ya hizo zipo kwenye majaribio hivi sasa. Hatua hii itaimarisha uwezo wa kukabiliana na upungufu wa maji ambao unategemewea kuendelea.

Pamoja na kazi zote hivi kuendelea kufanyika, ofisi zetu za mikoa TANESCO itaendelea kutoa ratiba ya upungufu wa umeme kwenye maeneo yote yanayoathirika na wateja watapewa taarifa kwa njia mbalimbali zikiwemo pamoja na ujumbe mfupi wa maneno kwenda kwa mhusika wa eneo litakaloathirika.