Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia, Iringa

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Iringa vijijini (UVCCM), Elia kidavile amewataka wanafunzi wanaohitimu darasa na saba kukataa kwenda kufanyakazi za ndani pindi wanapohitimu elimu ya msingi.

Akizungumza kwenye mahafali ya darasa la saba katika shule ya msingi Mlolo,Elia kidavile, amesema kuwa kumekuwa na wimbi kubwa la madalali kuwarubuni wanafunzi kwenda kufanya kazi za ndani pindi tu wanapomaliza elimu msingi jambo ambalo limekuwa likikatisha ndoto za watoto wengi.

Mwenyekiti wa UVCCM wilaya ya Iringa Elia Kidavile akitoa vyeti kwa wahitimu wa shule ya msingi Mlolo wakati wa mahafali ya 59 toka kuanzishwa kwa shule hiyo.

Kidavile amewataka wazazi kukataa kabisa jambo hilo ambalo halina afya kwa maendeleo ya wananchi wa wilaya ya Iringa vijijini pamoja na Taifa kwa ujumla.

Amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inatoa elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi sekondari hivyo hakuna haja ya wazazi kuwapeleka watoto wao kwenda kufanya kazi za ndani pindi wanapohitimu elimu ya msingi.

Kidavile amesema kuwa mzazi yoyote yule anakayekutwa amempeleka mtoto wake kufanya kazi za ndani basi sheria zitachukua mkondo wake na UVCCM wilaya ya Iringa vijijini haikubaliani kabisa na wazazi wanaowapeleka watoto kufanya kazi za ndani,hivyo wazazi wanatakiwa kuwapeleka sekondari mara baada ya matokeo kutoka.

Alisisitiza kwa jamii ya wananchi wa Kijiji cha Mlolo kutoa taarifa kwa viongozi wa Kijiji,kata,tarafa na wilaya iwapo kuna mzazi amempeleka mtoto wake kufanya kazi za ndani au mtoto ametoroka kwenda kufanya kazi za ndani ili sheria ichukue mkondo wake.

Aidha mwenyekiti wa UVCCM wilaya ya Iringa vijijini Elia kidavile alichangia kiasi cha shilingi laki mbili kwa ajili ya kukarabati sakafu za shule ya msingi Mlolo ambao imeharibika ili kuwawezesha walimu kutoa elimu bora bila kuwa na hofu ya miundombini ya darasa.

Awali akizungumza mbele ya mgeni rasmi,mwalimu mkuu wa shule ya msingi Mlolo Salum Mtewa amesema kuwa shule hiyo inakabiriwa na changamoto za ukosefu wa kompyuta,photokopi mashine, upungufu wa madawati, upungufu wa walimu na upungufu wa vifaa vya michezo kwa wanafunzi.

Mwalimu Mtewa amesema kuwa anashukuru mchango alioutoa mwenyekiti wa UVCCM wilaya ya Iringa vijijini Mheshimiwa Elia kidavile katika shule hiyo ya msingi Mlolo.

By Jamhuri