Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Lindi

Huenda Adha ya usafiri na usafirishaji bidhaa inayowakabili wananchi wanaotumia barabara ya Kiranjeranje kwenda Ruangwa ikafikia tamati baada ya Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Lindi kutangaza kutia kambi eneo hilo ili kuhakikisha njia inapitika.

kambi hiyo inalenga kuondoa taabu wanayokutana nayo wananchi kwa sasa katika usafirishaji wa bidhaa wanazozalisha na hata wasizozalisha kutokana na kulazimika kutumia bodaboda kwani hakuna gari inayoweza kupita.

Hayo yamewekwa bayana na Meneja wa Tanroads mlMkoa wa Lindi, Emil Zengo alipokuwa akieleza mikakati waliyonayo katika urejeshaji wa mawasiliano yote yaliyokatika ndani ya mkoa.

Zengo amesema barabara hiyo ina umuhimu mkubwa kwa watu wa Ruangwa na maeneo jirani ikiwemo Nanjirinji kwani ni wakulima wazuri wa ufuta, mbaazi na hata uchimbaji wa madini mbalimbali.

Barabara hiyo ni miongoni mwa zilizoathiriwa na mvua kubwa zilizonyesha nchini za El-Nino zilizofuatiwa na mvua zilizosababishwa na Kimbunga Hidaya.

“Mvua za El- Nino zilibeba daraja katika mto Ngurukuru na kukata mawasiliano kati ya Namichiga na Kilanjelanje,” amesema Zengo.

Amesema kambi watakayoiweka itakuwa kubwa huku wakiomba Serikali kuwaongeza nguvu ili waweze kuhakikisha barabara zote zinapitika muda wote.

“Kwa sasa barabara hii ina maeneo ambayo mvua zinaponyesha yanajaa maji kwa wingi na kuna maeneo ambayo yanahitaji kujengwa madaraja, bajeti ya Serikali itakaporuhusu kama TANROADS tuko tayari kwa muda wowote utakaohitajika kujenga miundombinu ya makaravati na madaraja ili barabara hii iweze kutumika muda wote,” amesema Zengo.

Kufanya hivyo kutasaidia kuunganisha wilaya ya Kilwa Masoko na Ruangwa na kuwawezesha wananchi kusafirisha mazao yao na kupata chakula ambacho hawawezi kulima

“Pia waweze kusafirisha madini mbalimbali ambayo yanapatikana kwa wingi sana katika eneo hili, kwa kuzingatia umuhimu wa eneo hili, sisi kama Wakala wa barabara Tanroads Lindi tuko tayari kusimamia matengenezo ya muda mfupi na muda mrefu yanayohutajika,” amesema Zengo.

By Jamhuri