Na Mwandishi Wetu, Dodoma
WAKALA wa Barabara Tanzania (TANROADS) umeendelea kutekeleza kazi kubwa ya kurejesha miundombinu ya barabara na madaraja iliyoharibiwa na mvua za El-Nino pamoja na Kimbunga Hidaya, hatua iliyosaidia kurejesha mawasiliano na shughuli za kijamii na kiuchumi katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumza kuhusu utekelezaji wa kazi hizo Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega alisema , kupitia TANROADS, ilipanga kufanya matengenezo ya barabara kuu na barabara za mikoa yaliyohusisha matengenezo ya kawaida kwa kilometa 35,311.01, matengenezo ya muda maalum kwa kilometa 2,994.31, matengenezo ya sehemu korofi kilometa 305.17 pamoja na matengenezo ya madaraja 2,865 katika mwaka wa fedha 2025/2026.
Ulega alisema ,katika kipindi cha Julai 2025 hadi Aprili 2026, Serikali imefanikiwa kufanya matengenezo ya kawaida ya barabara zenye urefu wa kilometa 16,782.58, matengenezo ya muda maalum kwa kilometa 1,101.12, matengenezo ya sehemu korofi kwa kilometa 147.13 pamoja na matengenezo ya madaraja 1,383.
“Lengo la matengenezo hayo ni kuhakikisha miundombinu inayojengwa inalindwa, inadumu kwa muda mrefu na kuwa salama kwa watumiaji wakati wote.”alisema Ulega
Aidha, mvua za El-Nino na Kimbunga Hidaya vilivyoikumba nchi mwishoni mwa mwaka 2023 vilisababisha mafuriko makubwa yaliyoathiri mtandao wa barabara, hususan zile zilizojengwa kwa kiwango cha changarawe.
Kwa mujibu wa tathmini ya uharibifu wa miundombinu uliofanywa baada ya majanga hayo, madaraja 63, kilometa 827 za barabara, mitaro yenye urefu wa kilometa 84 pamoja na makalavati 225 katika wilaya 139 za Tanzania Bara viliharibika.
Alisema miongoni mwa barabara zilizoathirika zaidi ni barabara ya Dar es Salaam–Lindi, ambapo hali hiyo ilisababisha sehemu ya fedha zilizokuwa zimepangwa kwa ajili ya matengenezo na ujenzi wa barabara kuelekezwa katika kushughulikia dharura zilizojitokeza.
Alisema utokana na hali hiyo, Serikali kupitia Programu ya Contingent Emergency Response Component (CERC) ilitekeleza jumla ya miradi 81 ya dharura ya ujenzi wa madaraja yaliyoathiriwa na mvua za El-Nino na Kimbunga Hidaya katika mikoa 22 ya Tanzania Bara kwa gharama ya Sh bilioni 556.93.
“Kati ya miradi hiyo, miradi 70 yenye thamani ya Sh bilioni 414.481 inatekelezwa na wakandarasi wa ndani, huku miradi 11 yenye thamani ya Sh bilioni 142.447 ikitekelezwa na wakandarasi wa kigeni.”alisema
Serikali ilieleza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo umefikia asilimia 97.6, ambapo miradi 78 imekamilika na taratibu za kuipokea zinaendelea, huku miradi mitatu ikiwa katika hatua za mwisho za ukamilishaji.
Aidha, utekelezaji wa miradi hiyo umeondoa changamoto za usafiri na mawasiliano zilizokuwa zikiwakabili wananchi katika maeneo mbalimbali na kurejesha matumaini kwa wananchi waliokuwa wameathirika na uharibifu wa miundombinu hiyo.


