Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia, Dar es Salaam

MAMLAKA ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) imepokea vifaa mbalimbali vyenye thamani ya zaidi ya sh bilioni 1 kutoka kwa Mamlaka ya biashara ya Korea Kusini kwa ajili ya kuboresha Utendaji kazi.

Vifaa hivyo ni vibanda 500 vya kuoneshea maonesho, komputa mpakato 10, komputa za kawaida 30, scanner 30 pamoja na jenereta la KVT 60.

Akizungumza katika hafla hiyo ya kupokea vifaa hivyo leo Machi 19, 2024 ,Mkurugenzi Mkuu wa Tantrade, Latifa Khamis amesema vifaa hivyo ni muhimu na vya thamani kwa mamlaka hiyo kwasababu vitaongeza mapato na kuleta ufanisi katika maonesho ya Biashara ya kimataifa (sabasaba).

Amesema katika kuboresha zaidi Maonesho ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) Tanrade iliuomba ubalozi wa Korea Kusini kupata vifaa ikiwemo vibanda ambavyo vitasaidia katika kuboresha maonesho kwenda vizuri.

“Kama mnavyoshuhudia kila siku zinavyokwenda wadau wamekuwa wakiitaji kushiriki maonesho lakini wamekuwa wakikosa nafasi hivyo kupitia vibanda hivi tutaongeza washiriki na ufanisi pamoja na mapato Kwa nchi na hatimaye uchumi wa Nchi kupitia tantrade utaweza kuongezeka,”amesema Latifa.

Amesema mahusiano hayo baina ya ubalozi na Korea kusini ni mazuri na ya aina yake na yaliolenga kusaidia bila masharti yoyote.

Mbali na msaada huo pia amesema wako katika mazungumzo baina ya tantrade na Ubalozi wa Korea kusini yanayolenga zaidi kuboresha Utendaji kazi.

“Hawa ni ndugu zetu ambao wanaimalisha mahusiano yetu si tu kwa Tan trade pia katika maeneo mengine,”alisisitiza Latifa.

Mkurugenzi Mkuu huyo alitoa wito kwa wadau na washiriki wa maonesho kujitokeza kushiriki kwani uwezo wa Tantrade kuwahudumia umeongezeka.

Pia aliwahidi kuwa maonesho ya kimataifa ya Biashara ya 48 ya mwaka huu yataimarika na yatakuwa yenye mvuto zaidi.

Kwa upande wake Balozi wa Korea kusini, Kim Sun Pyo amesema wataendelea kushirikiana katika maeneo mbalimbali .

Balozi Sun Pyo amesema ipo haja ya kuwahimiza wananchi na watanzania wasafarishe sana bidhaa zao ili kwenda kuuza Korea kusini.

Vile vile amesema licha ya watanzania kuhimizwa umuhimu wa kuwahamasisha wananchi wa Korea kusini waweze kununua bidhaa kutoka Tanzania.

“Tunaitajika kuamasisha uhusiano wa pande zote mbili katika masuala haya,”amesema Balozi Sun Pyo.

By Jamhuri