Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Morogoro

Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro imemuhukumu John Mwasikili kutumikia kifungo cha miaka 25 gerezani baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi zenye ujazo wa kilo 107.29.

Aidha Mahakama imeamuru gari namba T 895 CQR ambalo lilikuwa na bangi hiyo litaifishwe na kielelezo ambacho ni dawa za kulevya aina ya bangi kiteketezwe.

Hukumu hiyo imesomwa na Jaji Monica Otaru wa mahakama hiyo ya Morogoro baada ya kuridhika na vielelezo 15 na ushahidi uliotolewa na mashahidi 16 wa upande wa Jamuhuri ulioweza kuthibitisha pasipo kuacha shaka kuwa mshtakiwa ametenda kosa hilo.

Akisoma hukumu hiyo Jaji Otaru amesema kuwa amemtia hatiani mshtakiwa huyo baada ya kujiridhisha kuwa ni kweli mshtakiwa alikamatwa na dawa ya kulevya aina ya bangi yenye uzito wa kilogram 107.29 iliyokuwa ndani ya gari aina ya Toyota Kluger namba T.895 CQR kwenye mifuko nane ya sulphate.

Mshitakiwa Mwasikili alikamatwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya na kufikisha katika Mahakama kuu kanda ya Morogoro Machi 15, 2024.

Inadaiwa kuwa mwaka 2022 huko Morogoro lilikamatwa gari aina ya Toyota Kluger lenye namba za usajili T.985 ambalo ndani yake lilikutwa na mifuko nane ya sulphate ikiwa na dawa za kulevya aina ya bangi.

Katika kesi hiyo upande wa Jamuhuri uliwasilisha vielelezo 15 na mashahidi 16 huku mshtakiwa alipeleka mashahidi 11.

By Jamhuri