Na Wilson Malima, JAMHURI MEDIA

Kwa mujibu wa takwimu kutoka Benki ya Tanzania (BoT) na Wizara ya Kilimo, Tanzania imeongeza mauzo ya nje ya chakula mwaka hadi mwaka, huku chakula hicho kikiuzwa nchi za Afrika Mashariki, Kusini mwa Afrika, Pembe ya Afrika (Horn of Africa) na sehemu nyingine mbalimbali duniani.

Takwimu hizo zinaonesha kuwa Tanzania iliuza mboga mboga zenye thamani ya Dola za Marekani Bilioni 1.01 sawa na Sh. trilioni 2.4 katika kipindi cha miaka mitano kati ya mwaka 2018 hadi 2022.

Tanzania pia iliuza mazao ya nafaka (zaidi mchele na mahindi) yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 999 sawa na Sh. trilioni 2.3 katika kipindi hicho cha miaka mitano iliyopita.

Mauzo ya nje ya nchi ya samaki na bidhaa za samaki yalifikia Dola za Marekani milioni 800 sawa na Sh trilioni 1.9, wakati matunda yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 71.4 sawa na Sh.Bilioni 170 kati ya 2018 na 2022.

Takwimu hizo zinaonesha kuwa Tanzania ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa watano wa mchele kwenye bara zima la Afrika na ndiyo mzalishaji mkubwa zaidi wa mchele Afrika Mashariki.

Katika msimu wa 2020/21, Tanzania ilizalisha tani milioni 1.85 za mchele, wakati mahitaji ya nchi kwa mwaka ni takribani tani milioni 1. Maana yake ni kuwa mchele wa ziada ulikua tani 850,000.

Katika msimu huo huo, Tanzania ilizalisha tani milioni 6.5 za mahindi, ukilinganisha na nahitaji ya taifa ya tani milioni 6 kwa mwaka.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan Ikulu akifuatilia na kuandika mambo kadhaa wakati Waziriwa Kilimo  Hussein Bashe (Hayupo pichani) akitoa hotuba yake leo kwenye uzinduzi huo uliofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam leo Ijumaa 17,2023.

Takwimu hizi zinaibuka huku Rais Samia Suluhu Hassan leo akizindua maandalizi ya mkutano mkubwa wa Kilimo wa Afrika (Africa Food Systems Forum) ambao unatarajiwa kufanyika Tanzania Septemba 5-8, mwaka huu.

Uzinduzi huo umefanyika Ikulu, Dar es Salaam.

Tangu aingie madarakani mwezi Machi 2021, Rais Samia ameongeza bajeti ya serikali kwenye kilimo maradufu kwa viwango ambavyo havijawahi kuonekana tangu Tanzania ipate uhuru mwaka 1961.

Serikali ya Samia imewekeza kwenye ruzuku ya mgbegu, ruzuku ya mbolea, uzalishaji mbegu na kilimo cha umwagiliaji.

By Jamhuri