Serikali imetangaza utayari wake wa kuandaa mkubwa mkubwa wa Mtandao wa Wasimamizi wa Rasilimali Watu katika Sekta ya Umma Barani Afrika unaotarajiwa kufanyika Zanzibar utakaojadili matumizi ya Akili Unde (AI) na mikakati ya kuboresha utendaji wa taasisi mbalimbali.
Mkutano huo utafanyika kuanzia Novemba 10 hadi 13 mwaka huu ukizihusisha nchi zote 54 wanachama za Afrika.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete akizungumza na waandishi wa habari Unguja, Visiwani Zanzibar Oktoba 10, 2026 kuhusu maandalizi ya Mkutano huo mkubwa unaotarajiwa kukutanisha zaidi ya wataalamu 800 wa rasilimali watu.
“Mkutano huo utaongozwa na kaulimbiu kuu inayosema “kuwezesha mabadiliko ya kimkakati ya rasilimali watu katika utumishi wa umma barani Afrika kwa kutumia akiliunde.
“Lengo la kukutanisha wataalamu hao ni kujadili jinsi ya kukabiliana na mabadiliko ya akili unde (AI) na kuondoa hofu kwamba teknolojia hiyo inaweza kuchukua nafasi ya mameneja wa rasilimali watu badala ya kutumia kama fursa ya kuleta maendeleo katika nchi za Afrika,” Amesema Kikwete.
Katika mkutano huo, Waziri Kikwete amesema zitawasilisha mada zisizopungua tano, huku mtoa mada mkuu akiwa Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu, Balozi Ombeni Sefue.
Amesema hadi sasa nchi 11 zimethibitisha kushiriki zikiwemo Kenya, Uganda, Somalia, Nigeria, Sierra Leone, Cote D’Ivoire, Ghana, Namibia, Lesotho, Zimbabwe na Tanzania.
Waziri Kikwete ametoa wito kwa Watanzania na wataalamu wote wa rasilimali watu ndani na nje ya nchi kuendelea kujiandikisha kwa wingi ili wasikose fursa hii ya kipekee ya kujenga uwezo na kwenda sambamba na mabadiliko ya kiutendaji.
Mbali na mijadala ya kitaaluma, mkutano huo unatajwa kuwa fursa ya kutangaza mafanikio ya kitalii na kiuchumi ya Zanzibar yaliyofikiwa.
Wajumbe watakaohudhuria watapata fursa ta kujionea sura mpya ya Zanzibar ikiwemo uwekezaji katika uchumi wa buluu.
“Ujio wa wageni hao unaotarajiwa kuchochea ukuaji wa uchumi na biashara nchini wakati wa siku hizo za mkutano,” Amesema Kikwete.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Mhe. Haroun Ali Suleiman amebainisha kuwa kupewa fursa ya kuandaa mkutano huo mkubwa wa kimataifa ni heshima kwa Tanzania na ishara ya amani na utulivu uliopo nchini.
Amesisitiza kuwa nchi zenye migogoro haziwezi kuaminiwa kuandaa mikutano ya kiwango hicho cha kimataifa.


