Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ipo katika hatua za mwisho kukamilisha mapitio ya Kanuni za Utangazaji kuruhusu matumizi ya teknolojia mpya ya utangazaji wa redio kidijitali maarufu kama ‘Digital Sound Broadcasting (DSB)’.

Akifungua Mkutano wa mwaka wa vyombo vya utangazaji jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew ameeleza kuwa teknolojia hiyo itapunguza changamoto ya ukosefu wa masafa ya redio, hasa katika maeneo ya miji mikubwa nchini hivyo kuongeza wigo mpana zaidi wa ufikishaji wa maudhui ya redio kwa wananchi wengi zaidi yakiwemo maeneo ya mipakani.

Wakati taifa likijiandaa na uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu, Mhandisi Kundo aliitaka sekta ya utangazaji kutoa maudhui bora za shughuli hizo muhimu za demokrasia.

Kuhusu maboresho ya sekta ya utangazaji, Mhandisi Kundo alisema kuwa tayari Serikali imeagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kufanya upembuzi yakinifu wa sekta yote ya utangazaji.

Mchakato huo utamulika mageuzi ya kiteknolojia, vyanzo vya mapato, gharama za uendeshaji, soko la utangazaji, utandawazi, na maudhui ya utangazaji na athari zake ili kuona uwezekano wa kutatua changamoto za utangazaji zikiwemo zinazohusu uwezo wa vituo vya Utangazaji kujiendesha kimapato.

DSB ni teknolojia inayotumia miundombinu ya kidijitali kama vile mkongo wa mawasiliano ili kufikisha maudhui kwa jamii ikiwa badala ya kutegemea masafa ya redio pekee.

Akifafanua zaidi juu ya DSB, meneja wa huduma za utangazaji wa Mamlaka ya Usimamizi wa Mawasiliano nchini (TCRA), Mhandisi Andrew Kisaka alisema kuwa teknolojia hiyo itawawezesha wadau wa utangazaji kutoa kuwafikia wananchi wengi zaidi.

Mhandisi Kundo aliwaasa wadau wa sekta ya utangazaji kushiriki kikamilifu katika mchakato huo wa kuboresha sekta na kutoa maoni yao kwa kushirikiana na mshauri mwelekezi atakapokuwa akitekeleza majukumu yake chini ya usimamizi wa TCRA.

Mkutano wa vyombo vya utangazaji, uliowakutanisha watoa huduma mbalimbali wa utangazaji nchini, ulihitimishwa na azimio la kuunganisha jitihada za pamoja kuhakikisha vyombo vya utangazaji vinazingatia maadili na kuondoa maudhui yanayokiuka viwango vya utangazaji.

By Jamhuri