Tanzania inakabiliwa na upungufu wa walimu wa somo la hisabati katika ngazi zote hali inayochangia kuendelea kuwepo kwa ufaulu mdogo katika somo hilo.

Hayo yamesemwa jijini Arusha na Mwenyekiti wa Chama cha Hisabati Tanzania (CHAHITA), Betinasia Manyama wakati akizungumza katika mkutano mkuu wa chama hicho ulioenda sambamba na mafunzo endelevu ya walimu kazini ya 58 kitaifa kwa walimu wa hisabati kutoka mikoa yote Tanzania inayofanyika katika chuo cha uhasibu Arusha.

Amesema somo la hesabu limekuwa ni changamoto kubwa kwa wanafunzi kutokana na ufaulu mdogo unaosababishwa na kuwepo kwa upungufu wa walimu katika somo hilo.

Manyama amesema walimu hao wamekuwa na vipindi vingi sana kutokana na walimu waliokuwepo wengi wao kustaafu na wengine kuhamishwa vituo hivyo kuiomba serikali kuangalia namna ya kusaidia walimu hao wa hisabati.

Mwenyekiti wa Chama cha Hisabati Tanzania (CHAHITA) ,Betinasia Manyama akizungumza katika mkutano huo jijini Arusha

“Tunaomba sana serikali ituangalie kwa jicho la pekee kwani tupo wachache sana na tunalemewa tunaomba tuongezewe walimu wengine kwani imekuwa ni changamoto na tunashindwa kutoa hata motisha kwa wanafunzi kutokana na uchache uliopo.”amesema.

Aidha ameiomba serikali kutoa motisha kwa walimu wa somo la hisabati waliopo hivi sasa ili waweze kufanya vizuri zaidi kwani wamekuwa na mzigo mkubwa kwa kuwa na vipindi 30 huku kwa walimu wa kiswahili wakiwa na vipindi 8 tu,kwani utofauti ni mkubwa sana.

“Tunaomba walimu wa somo la hisabati wapunguze tabia ya ukali na kuingia na viboko darasani hali ambayo inawachanganya wanafunzi na kuwatoa kwenye uwepo ,naombeni sana walimu mjitahidi kuongeza bidii na mbinu katika ufundishaji wa somo la hesabu ili kupata wanafunzi wengi watakaolipenda somo hilo na kuongeza kiwango cha ufaulu.”amesema.

Naye Afisa elimu sekondari mkoa wa Arusha ,Abel Ntupwa akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala wa mkoa wa Arusha , aliwataka walimu hao kuimarisha klabu za hisabati katika shule mbalimbali ili kukuza kiwango cha ufaulu katika somo hilo na kuwafanya wanafunzi kupenda zaidi somo hilo.

Ntupwa aliwataka walimu hao kuepukana na kujilimbikiza mikopo ambayo wamekuwa wakikopa kila mahali hali ambayo inawapelekea kuwa na mawazo ,huku maarifa yakiendelea kupungua na kuishia kuingia madarasani wakiwa na mawazo na kushindwa kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wanafunzi.

Aidha aliwataka walimu hao kubeba maono kwani wengi hawana maono badala yake wanatumia uzoefu walionao ambapo amewataka kubadilika mara moja ili tasnia hiyo iendelee kuheshimika zaidi.

“Nawaombeni sana muwe na ujasiri na udhubutu wa kutumia ndoto tulizo nazo ili tuwe msaada kwa jamii , familia na nchi kwa ujumla na tuhakikishe tunaacha tabia za kufedhehesha somo la hisabati bali tutafute namna ya kutoka ili chama hiki kiweze kuwa mfano wa kuigwa”amesema Ntupwa.

Ameomba Serikali kuongeza fedha kwa ajili ya walimu wa somo la hisabati kwani wanafanya kazi kubwa ambayo inahitaji motisha ili kuzidi kuongeza hari ya ufaulu katika somo la hisabati mashuleni.

Walimu wa somo la hisabati  kutoka Mikoa yote Tanzania wakiwa katika Mkutano huo unaofanyika katika Chuo cha Uhasibu Arusha.

By Jamhuri