Na Mwandishi Wetu

MHADHIRI wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Profesa Goodluck Urassa amesema ili shule ziweze kufanya vizuri kitaaluma, walimu wanapaswa kufanya kazi yao kama sehemu ya biashara, na kuongeza ubunifu.

Profesa Urassa, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, alipokuwa akiwajengea uwezo walimu wa shule za Kimataifa za St Mary’s, ili waweze kuongeza ubunifu na ufanisi katika ufanyaji kazi wao.

Alisema lengo la semina hiyo ni kuwapiga msasa walimu hao, katika mambo mengi ikiwamo elimu ya ujasiriamali, ubunifu, na namna ya kuongeza ufaulu katika shule zao kwaajili ya kuzikuza kitaifa.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Profesa Goodluck Urassa akizungumza jana jijini Dar es Salaam, alipokuwa akiwajengea uwezo walimu wa shule za Kimataifa za St Mary’s, ili waweze kuongeza ubunifu na ufanisi katika ufanyaji kazi wao.

“Nimewapiga msasa namna ya kufanya kazi kwa viwango vya juu, jinsi ya kuhudumia wateja, kuendesha shule zao kibiashara na kijasiriamali” alisema Profesa Urassa 

Pia, aliwataka walimu kujenga utamaduni wa kuwa na mpango, wa kufanya kazi kuanzia mwanzo wa mwaka hadi mwisho wa mwaka, pamoja na ule wa kila siku kwenye kutimiza majukumu yao ya kitaaluma.

“Shule nyingi, zinaathirika kwa kutojenga vizuri mipango yao, na kukosa rasilimiari za kujiendesha ndiyo maana tunawajengea walimu na viongozi uwezo ili wakawarithishe na wanafunzi wao ili tuje kupata viongozi bora wa baadaye” alisema

Vilevile, alizisihi taasisi za elimu kukumbuka umuhimu wa kutoa semina kwa watumishi wa serikali, ili waweze kukumbuka majukumu yao, muhimu wa kazi yao na kuongeza ufanisi katika kazi akisema kuwa njia hiyo itasaidia kupata matokeo chanya kwenye sekta.

Mkurugenzi wa shule hizo Tanzania, Dk Rose Rwakatale, alisema lengo la semina hiyo ilikuwa kuwainua wafanyakazi wao, na kuwaongeza elimu ili waweze kutimiza majukumu yao kulingana na mabadiliko ya teknolojia.

Alisema semina hiyo iliwakutanisha walimu kutoka shule 14 zilizopo Dar es Salaam na mikoa mingine kwa lengo la kusikiliza, kuchambua kwa kina na hatimaye kwenda kufanyia kazi Ili kuongeza ufanisi kwenye shule zao.

Mkuu shule ya St Mary’S Tabata, Thomas Samsoni alisifu semina hiyo akisema imewafungua kwa kiasi kikubwa kwani wamefundishwa namna ya kuwahudumia wateja, majukumu ya viongozi katika taasisi. 

“Baada ya semina hii matokeo yatakuwa makubwa, tumefundishwa vitu vingi, tumeongeza maarifa na ujuzi, imekuwa siku nzuri kwetu kujifunza kutoka kwa Profesa mbobezi tunategemea kuhamishia maarifa haya kwenye maeneo yetu ya kazi” alisema.

Aliushukuru uongozi wa shule hizo kwa kuandaa semina hiyo, aliyoita elimishi akiomba liwe jambo endelevu.

Walimu wa shule za St Mary’s wakimsikiliza Mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Profesa Goodluck Urassa alipokuwa akiwajengea uwezo walimu wa shule hizo za  Kimataifa za St Mary’s, ili waweze kuongeza ubunifu na ufanisi katika ufanyaji kazi wao.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Profesa Goodluck Urassa akizungumza jana jijini Dar es Salaam, alipokuwa akiwajengea uwezo walimu wa shule za Kimataifa za St Mary’s, ili waweze kuongeza ubunifu na ufanisi katika ufanyaji kazi wao.

By Jamhuri