Tanzania imepokea na kupongeza azimio la kuanzishwa kwa Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) na kusisitiza kuwezesha utekelezaji wa Mkakati wa Dunia wa Kuhifadhi Bioanuai kupitia Mikakati ya Kitaifa ya Kuhifadhi Bionuai.

Hayo yamebainishwa wakati wa Mkutano Mkuu wa Saba wa Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) unaofanyika Vancouver nchini Canada ambapo Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Mary Maganga wakati anaongoza Ujumbe wa Tanzania kushiriki.

Pamoja na kuzipongeza nchi zilizotoa ahadi ya kuchangia Mfuko huo, Tanzania imeziomba nchi zilizoendelea na zinazoendelea kuwezesha ukusanyaji wa fedha za kutosha katika Mfuko husika. 

Mfuko wa Mazingira wa Dunia ni moja ya Mifuko wa Kimataifa inayowezesha shughuli za uhifadhi wa mazingira duniani hususan katika nchi zinazoendelea.

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Mary Maganga (wa pili kulia) akiongoza Ujumbe wa Tanzania katika kushiriki Mkutano Mkuu wa Saba wa Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) unaofanyika Vancouver nchini Canada kuanzia tarehe 22 hadi 26 Agosti, 2023. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi, Hifadhi ya Bioanuai, Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Thomas Bwana.

Shughuli zinazowezeshwa ni pamoja na Hifadhi ya Bioanuai, Mabadiliko ya Tabianchi, Matumizi bora ya Ardhi, Udhibiti wa Taka hatarishi na Kemikali pamoja na Hifadhi ya maji yanayovuka mipaka.

Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazofaidika na mfuko huu katika kuwezesha shughuli za kuhifadhi mazingira nchini.

Pamoja na mambo mengine, moja ya masuala muhimu yaliyopitishwa na Mkutano Mkuu wa GEF ni kuanzishwa kwa Mfuko wa Dunia Kuhifadhi Bioanuai.

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Mary Maganga (wa pili kushoto) akizungumza na Naibu Mtendaji Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP) Bi. Elizabeth Mrema (kulia) aliposhiriki Mkutano Mkuu wa Saba wa Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) Vancouver Canada tarehe 22 Agosti, 2023 hadi 26 Agosti, 2023. Kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi, Hifadhi ya Bioanuai Idara ya Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Thomas Bwana

Watalaamu wengine kutoka Tanzania wanaoshiriki ni Mshauri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa masuala ya Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi, Dkt. Richard Muyungi, Mkurugenzi Msaidizi, Hifadhi ya Bioanuai Idara ya Mazingira, Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Thomas Bwana, Afisa Mazingira Mwandamizi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Thomas Chali na Bw. Charles Faini wa Ubalozi wa Tanzania nchini Canada.

Mkutano huo umefunguliwa tarehe 22 Agosti 2023 unatarajiwa kuhitimishwa tarehe 26 Agosti, 2023.

By Jamhuri