Tanzania,Romania kuimarisha ushirikiano, zatia saini makubaliano maeneo haya

Na Mwandishi Wetu JAMHURI MEDIA Dar es Salaam.

Tanzania na Romania zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika maeneo ya kimkakati ikiwemo afya, kilimo, elimu, mazingira na madini.

Pia zimetia saini hati za makubaliano kushirikiana kwa pamoja kukabiliana na maafa na misaada ya kimataifa ya kibinaadam, pia hati ya makubaliano ya Sayansi katika kada za kilimo na mazingira.

Makubaliano hayo yamefikiwa leo Novemba 17, 2023 katika Ikulu ya Dar es Salaam na kusainiwa na Mawaziri wa pande zote mbili mbele ya Rais Samia na Rais wa Romania Klaus werner Iohannes ambaye yuko nchini kwa ziara ya kikazi.

Akizungumza mbele ya waaandishi wa habari baada ya utiaji saini huo Rais Samia amesema, ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Romania ni wa kihistoria na hatua za pamoja zitachukuliwa kuendelea kuuimarisha kwenye maeneo ya kimkakati.

“Tumezungumzia fursa zilizopo kwenye sekta ya Afya na utengenezaji wa Madawa usindikaji wa mazao ya kilimo na fursa za kubadilishana uzoefu katika sekta za kilimo na sekta, madini lakini pia maeneo ya kukabiliana na majanga.”Amesema Rais Samia

Katika kupande wa elimu amesema, wamejadili namna ya kuongeza wigo wa ufadhili wa masomo hususani kwenye fani za udaktari na famasia ambapo Romania imekubali kwa mwaka huu kutoa nafasi kumi za masomo kwa watanzania katika maeneo watakayoyachagua.

Lakini pia amesema tanzania imetoa nafasi tano za ufadhili wa masomo kwa vijana wa Romania kuja kusoma katika vyuo vya Tanzania.

“Hatua hii itachangia jitihada zetu za kujengeana uwezo wa rasilimali watu na kuboresha huduma zetu katika sekta mbalimbali.” Amesema Rais Samia

Vilevile akizungumzia suala la biashara Rais Samia amesema, urari wa kibiashara kati ya Tanzania na Romania umekuwa mdogo sana kulinganisha na fursa zilizopo hivyo kukuza ushirikiano huo ametaka yawepo mazungumzo baina na wafanyabiashara wa pande zote mbili.

“Tumezungumzia zaidi kukuza biashara kuangalia maeneo ambayo tunaweza kufanya kwa pamoja, kualika wafanya biashara wa Romania waje Tanzania au wa Tanzania waende Romania wajadiliane na kuona maeneo gani wanaweza wakafanya kwa pamoja.” Amesema

Katika hatua nyingine Rais Samia amesema kuhusu kuimarisha uhusiano katika majukwaa ya kimataifa ikiwemo kuongeza nguvu katika mkutano wa mabadiliko ya tabianchi wa COP 28 utakaofanyika katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE)

Amesema hatua hiyo ni katika kuhakikisha Tanzania inapata uungwaji mkono katika ajenda zaje kwenye mkutano huo kuhusu masuala ya nishati na nishati safi ya kupikia lengo ikiwa ni kupambana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

“Katika mkutano kuhusu mabadiliko ya tabia nchi nadhani nilishasema lengo ni kupunguza athari zinazojitokeza na Romania na wenyewe wamesema wana majanga kama ya kwetu na kwa hiyo tushirikiane katika kuyasemea na kupata nguvu ya pamoja” amesema.

Kwa upande wake Rais wa Romania Klaus Iohannes amepongeza utiaji saini wa hati za makubaliano kwamba ni hatua mpya ya kuimarisha uhusiano uliopo na kutaka uzidi kudumu kwa kuchukua hatua madhubuti kutekeleza makubaliano hayo.

Pia amesema anatambua suala la kiusalama liliopo katika ukanda wa nchi yake kutokana na vita inayoendelea kati ya Urusi na Ukraine na hivyo ameahidi kupunguza athari zitokanazo na vita hiyo ikiwa ni pamoja na kurahisha usafirishaji wa ngano kwa nchi za Afrika Tanzania ikiwemo

“Sisi kama Romania tuliweza kujadiliana namna gani tunaweza tukapunguza zile athari za vita tukiangalia pia katika namna gani tunaweza tukasaidia suala zima la chakula na pia njia mbalimbali za kilogistiki na kiutawala ambazo zimefanyika na nchi ya Romania ili kuweza kuhakikisha ya kwamba usafurishaji wa ngano katika nchi za kiafrika usiweze kuathiriwa.”

Ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya siku nne nchini hapa, Rais Klaus anatarajia kuelekea Zanzibar ambako atakutana na kuzungumza na Rais Hussein Mwinyi na kisha kuhitimisha ziara yake kwa kurejea Dar es Salaam ambako ataagwa rasmi.

Kiongozi huyo anakuwa Rais wa kwanza kufanya ziara ya kikazi Tanzania tangu uhusiano baina ya mataifa hayo mawili uasisiwe.

Uhusiano baina ya Tanzania na Romania ulianza mwezi Mei mwaka 1964 ikiwa ni mwezi mmoja tu baada ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambapo taifa hilo limekuwa likitoa ufadhili wa masomo ya udaktari na Famasia kwa Watanzania pia Tanzania imekuwa ikiagiza bidhaa kama vile mashine na vifaa kutoka Romania.