Na Allan Kitwe, JamhuriMedia, Tabora

Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wilayani Kaliua Mkoani Tabora wanatarajia kutumia zaidi ya sh bil 17 kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kwa ajili ya matengenezo ya barabara ili kuhakikisha barabara zote zinapitika.

Hayo yamebainishwa juzi na Meneja wa Wakala huo Wilayani humo Mhandisi Robert Kisandu alipokuwa akiwasilisha makisio ya bajeti ya Ofisi yake kwa mwaka wa fedha 2024/2025 katika kikao cha baraza la madiwani.

Amesema kuwa mapendekezo ya bajeti hiyo yatatokana na vyanzo vinne vya fedha ambavyo ni Fedha za Kawaida za Matengenezo kutoka Mfuko wa Barabara, Fedha za Majimbo, Fedha za Tozo ya Mafuta na Fedha za Mfuko wa Maendeleo.

Amebainisha kuwa katika mpango huo kiasi cha sh bil 5.219 ni bajeti ya matengenezo ya barabara yenye ukomo ambayo itatekelezwa kwa fedha zitakazotoka katika vyanzo hivyo vinne na kwa bajeti isiyokuwa na ukomo wakitarajia kutumia sh bil 12.65.

Kisandu amefafanua kuwa fedha za Mfuko wa Barabara zitatengeneza jumla ya km 44 za barabara za kawaida kwa gharama ya sh mil 431.9, km 18 za sehemu korofi kwa sh mil 154.08 na matengenezo ya muda maalumu ya km 5 kwa sh mil 75.3.

Aidha jumla ya makaravati 8 yenye urefu wa km 36 yatatengenezwa kwa gharama ya sh mil 184.62, gharama za usimamizi na ufuatiliaji wa miradi hiyo ni sh mil 44.6 wakati gharama za uendeshaji wa ofisi wanatarajia kutumia sh mil 38.04.

Ameongeza kuwa fedha za Mfuko wa Jimbo zinatarajia kutengeneza barabara 4 zenye urefu wa km 81 na makaravati 29 kwa gharama ya sh mil 950, barabara hizo ni Usimba-Kazaroho (km 20), Kaliua-Imalamihayo (15), Ichemba-Kanoge-Mwongozo (km 16) na Ichemba-Nwande (km 30).

Kwa upande wa fedha za Tozo za Mafuta ameeleza kuwa zitatengeneza barabara 7 za changarawe zenye urefu wa km 111 kwa gharama ya sh bil 1.7 na barabara 3 zenye urefu wa km 1.1kwa kiwango cha lami kwa gharama ya sh mil 557.6

Mhandisi Kisandu ametaja barabara zitakazojengwa kwa kiwango cha lami kuwa ni barabara ya Shamsheli (km 0.4), Msongeni-Aleale-Misufini-Sokoni (km 0.3) na barabara ya Boni (km 0.36).

Aidha barabara 3 zenye urefu wa km 1.37 zinatarajiwa kujengwa kwa kiwango cha lami kwa fedha za Mfuko wa Maendeleo kwa gharama ya sh mil 980.5, ametaja barabara hizo kuwa ni Banyanga (km 0.65), Masudi-Silimu-Msufini (km 0.32) na barabara ya Kisamvu km 0.4.

Kwa upande wa bajeti isiyokuwa na ukomo, Mhandisi Kisandu ameema kuwa wanatarajia kutengeneza jumla ya barabara 25 zenye urefu wa km 356.2 kwa gharama ya sh bil 9.29 na makaravati 277 kwa gharama ya sh bil 1.73 hivyo gharama zote kufikia bil 12.65.

By Jamhuri