‎Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
‎
‎Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imewekeza zaidi ya Shilingi bilioni 2.76 katika ununuzi wa vifaa vya kisasa vya uchunguzi wa udongo “Geotechnical Investigation” hatua inayolenga kuimarisha usanifu wa barabara na madaraja, kuongeza ubora wa miundombinu na kupunguza gharama za ujenzi nchini.
‎
‎Akielezea uwekezaji huo, Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Victor Seff amesema jukumu kuu la Wakala huo ni usimamizi, ujenzi na matengenezo ya mtandao wa barabara za wilaya zenye urefu wa kilomita 144,149.18 unaojumuisha barabara za lami, changarawe na udongo.
‎
‎Ameeleza kuwa kati ya mtandao huo, takribani kilomita 3,900 ni barabara za lami, zaidi ya kilomita 47,000 ni za changarawe huku zaidi ya kilomita 92,000 zikiwa ni barabara za udongo hali inayoonesha umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika teknolojia na tafiti zinazoweza kuongeza ufanisi wa ujenzi na matengenezo ya barabara za wilaya nchini.
‎
‎”TARURA ina jukumu la kuhakikisha kazi zinazotekelezwa zinafikia viwango vinavyotakiwa, jukumu hili linatekelezwa kupitia Kitengo cha Tafiti na Udhibiti wa Ubora ambacho hufanya uchunguzi wa udongo, kupima ubora wa kazi na kufanya tafiti za malighafi zinazoweza kutumika katika ujenzi wa barabara”, amesema.
‎
‎Mhandisi Seff amefafanua kuwa ununuzi wa vifaa hivyo vya kisasa utawezesha TARURA kupata taarifa sahihi kuhusu sifa na uwezo wa udongo kubeba mizigo taarifa ambazo ni muhimu katika usanifu wa barabara na madaraja imara na yenye kudumu kwa muda mrefu.
‎
‎Ameongeza kuwa vifaa hivyo vitaiwezesha TARURA kufanya tafiti kwa ufanisi zaidi, kuimarisha uwezo wa wataalamu wa ndani na kubaini mbinu zinazoweza kupunguza gharama za ujenzi bila kuathiri ubora wa miundombinu.
‎
‎”TARURA ina maabara kuu jijini Dodoma na maabara zingine zaidi ya 15 katika mikoa mbalimbali nchini zinazotekeleza majukumu ya kupima udongo, kuthibitisha ubora wa kazi za ujenzi na kufanya tafiti za malighafi zinazopatikana katika maeneo mbalimbali”, amesema.
‎
‎Amebainisha kuwa tafiti hizo ni muhimu kwa sababu malighafi zinazotumika katika ujenzi wa barabara muda mwingine hupatikana mbali na eneo la mradi jambo linalosababisha kuongezeka kwa gharama za usafirishaji lakini kupitia tafiti hizo TARURA huchunguza malighafi zinazopatikana maeneo ya miradi na kuthibitisha kama zinafaa kutumika na zimekidhi viwango vinavyotakiwa.
‎
‎Amesisitiza kuwa Maabara za TARURA zina jukumu muhimu la kupima na kuthibitisha ubora wa udongo na kazi zinazofanyika ili kuimarisha ubora wa miundombinu inayojengwa, kuongeza uimara wake na kuhakikisha fedha zinazotumika katika miradi ya barabara zinatoa thamani inayokusudiwa.
‎
‎Katika kuimarisha matumizi ya maabara hizo, Mtendaji Mkuu amewakaribisha Makandarasi na Wahandisi Washauri wanaotekeleza miradi ya TARURA au taasisi nyingine kutumia huduma za maabara za Wakala huo zilizopo Dodoma na katika mikoa mbalimbali nchini.
‎
‎Amesema maabara hizo zina vifaa vya kisasa vinavyoendana na mahitaji ya sasa ya sekta ya ujenzi huku wataalamu wa TARURA wakiwa wamepatiwa mafunzo yanayowawezesha kufanya uchunguzi na tafiti za udongo kwa ufanisi.
‎
‎Aidha, ameeleza kuwa TARURA itaendelea kuongeza vifaa na kuimarisha maabara zilizopo mikoani ili kupanua wigo wa huduma, kuboresha upatikanaji wa huduma za upimaji na udhibiti wa ubora na kuchangia ujenzi wa barabara na madaraja yenye ubora na uimara zaidi.
‎
‎Uwekezaji huo ni sehemu ya jitihada za TARURA za kutumia sayansi, teknolojia na tafiti za kitaalamu kuboresha usimamizi wa miundombinu ya barabara, kupunguza gharama zisizo za lazima na kuimarisha mtandao wa barabara unaochochea shughuli za kiuchumi na kijamii nchini.
‎


‎