Usikivu wa Serikali umeiwezesha TASAC kuongeza gawio kutoka bil.9.1 hadi bil.43.4

Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

SHIRIKA la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), limesema usikivu wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, umewezesha shirika hilo, kuongeza mchango wake serikalini kutoka Sh bilioni 9.1 mwaka 2018/19 hadi Sh bilioni 43.4 mwaka 2021/22.

Hayo yamebainishwa leo na Oktoba 5, 2023 Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Nelson Mlali wakati kikao kazi kati ya wahariri wa vyombo vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Akiwasilisha taarifa ya utendaji ya shirika hilo, amesema kuwa kuna fursa nyingi ambazo Watanzania wakiweza kuzitumia kikamilifu zitawanufaisha wao na Taifa kwa ujumla.

“Tangu kuanzishwa kwa shirika hili mwaka 2017 na kuanza utekelezaji mwaka 2018, mchango wake serikalini umekuwa ukiongezeka. Mwaka 2018/19 ulikuwa shilingi bilioni 9.1, mwaka 2019/20 ulikuwa shilingi bilioni 20.1, mwaka 2020/21 shilingi 31.8 na mwaka 2021/22 imepanda hadi shilingi bilioni 43.4.

““Zipo fursa nyingi katika sekta ya usafirishaji wa majini.Ipo fursa ya kusajili meli kwa njia rafiki na fursa ya kuwekeza katika vituo vya kufanya matengenezo ya vyombo vya majini.” amesema.

Amesema shirika hilo, limefanikiwa kuongeza idadi ya kadhia zilizohudumiwa kutoka 6,000 mwaka 2019/20 hadi zaidi ya kadhia 10,000 mwaka 2021/22 na kuunda nyenzo za udhibiti wa usafiri majini ikiwa ni pamoja na Kanuni na Miongozo mbalimbali ili kuwezesha utekelezaji wa Sheria katika kudhibiti usafiri majini.

Kwa mujibu wa Mlali idadi ya nyenzo za udhibiti imeongezeka kutoka mwaka 2018 nyenzo zaidi ya tano hadi zaidi ya 20 mwaka 2022.

Aidha, alisema TASAC imefanikiwa kuongeza idadi ya watoa huduma wanaodhibitiwa na shirika hilo kwa maana ya idadi ya leseni na vyeti vya usajili vilivyotolewa ambapo limetoa vyeti vya usajili 1,038 mwaka 2021/22 kutoka 796 mwaka 2018/19 na limetoa leseni 240 mwaka 2021/22 kutoka 145 mwaka 2018/19.

“Pia shirika limeongeza idadi ya vyeti vinavyotolewa kwa mabaharia waliokidhi masharti na kufikia vyeti 17,689 mwaka 2021/22 kutoka 5,699 mwaka 2018/19 na imeongeza idadi ya leseni za vyombo vidogo kutoka 2,006 mwaka 2018/ hadi 6,366 mwaka 2022,” alieleza.

Katika eneo la ukaguzi wa meli, Mlali amesema wameongeza idadi ya meli wanazozikagua kutoka meli saba mwaka 2018 hadi kufikia 39 mwaka 2022 na wanatarajia mwaka huu watakagua meli 233 hadi 300.

“Mafanikio mengine ni kuimarisha udhibiti wa huduma za bandari baada ya urasimishaji wa maeneo 20 ya kibandari katika mwambao wa bahari na Maziwa na tunaendelea kusimamia utekelezaji wa mikataba, itifaki na miongozo inayotolewa na Shirika la Bahari Duniani (IMO) na kuridhiwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema.

Ametaja sababu za mafanikio pamoja na usikivu wa serikali pia ni kwa shirika hilo kuzingatia miongozo inayotolewa na serikali pamoja na kamati za Bunge na ushirikishwaji wa wadau wa sekta ya usafiri kwa njia ya maji katika masuala yanayoihusu sekta.

Kuhusu fursa zinazopatikana katika eneo la usafiri wa majini alizitaja kuwa ni uanzishwaji wa Maegesho ya Boti Ndogo katika Ukanda wa Pwani, uanzishwaji wa viwanda vya utengenezaji malighafi za ujenzi wa boti za plastiki, ujenzi wa bandari rasmi za uvuvi na kukidhi mahitaji ya soko la Comoro.

Vile vile, amesema kupitia kanuni na ufuatiliaji mzuri wamefanikiwa kudhibiti umwagikaji wa mafuta majini jambo ambalo linaendelea kuyafanya mazingira ya majini kuwa salama.

Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu huyo, Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania limeanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Uwakala wa Meli Tanzania Sura ya 415 na kuanza kutekeleza majukumu yake rasmi kuanzia Februari 23, 2018 kufuatia Tangazo la Serikali Na. 53 la Februari 16, 2018.

“Majukumu ya shirika ni kusimamia na kudhibiti sekta ya usafiri wa majini, kuwezesha biashara ya usafirishaji majini na kufanya biashara ya uwakala wa meli.”

Amesema, misingi mikuu ya kuanzishwa kwa shirika ni kuwajibika kwa Taifa na kwa wadau katika kutekeleza mamlaka na makujumu yaliyo chini ya dhamana ya shirika.

Pia,kuwa mfano wa kuigwa katika mwenendo wa kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu kwenye shughuli zote.“TASAC inatoa huduma kwa weledi na kuhakikisha wateja wanapata huduma iliyo bora na kwa wakati.

“Huduma zinazotolewa na TASAC ni biashara ya usafirishaji,usalama wa usafiri wa majini, usajili wa vyombo vya majini na udhibiti wa uchumi.”

Aidha, amesema kazi kuu za msingi za shirika kisheria ni kuboresha huduma za usafirishaji wa majini, kuboresha usalama wa usafiri wa majini.

By Jamhuri