TAUS:Kuna uhaba wa madaktari bingwa wa upasuaji maradhi ya mkojo,uzazi

Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia, Arusha

Tanzania inakabiliwa na uhaba wa madaktari bingwa wa upasuaji wa maradhi ya njia ya mkojo na uzazi ambapo waliopo ni 100 tu ambao hawakidhi mahitaji kulingana na idadi ya wagonjwa hao waliopo.

Hayo yamesemwa jijini Arusha na Rais wa Chama cha Madaktari bingwa wa upasuaji wa maradhi ya njia ya mkojo na uzazi (TAUS),Prof.Chalonde Yongolo wakati akizungumza kwenye kongamano la kisayansi pamoja na mkutano mkuu wa TAUS unaofanyika jijini Arusha.

Rais wa chama cha madaktari bingwa wa  upasuaji wa  maradhi ya njia  ya mkojo na uzazi  (TAUS),Prof.Chalonde Yongolo  

Profesa Yongolo amesema kuwa,idadi ya madaktari bingwa katika sekta hiyo bado ni changamoto ambapo kwa idadi hiyo ya madaktari 100 ni sawa na daktari 1 kuhudumia wagonjwa laki 6.

“Changamoto ya kuwepo madaktari bingwa inachangiwa na kutokuwepo kwa mafunzo ya awali hapa nchini juu ya maswala ya udaktari katika mfumo wa mkojo na uzazi kwani mafunzo hayo yalikuwa yanatolewa nje ya nchi ila kwa sasa mafunzo hayo yameanza kutolewa rasmi hapa nchini hivyo tunatarajia kupata idadi ya madaktari bingwa wa kutosha’amesema Profesa Yongolo.

Ameongeza kuwa, wanataka kuhakikisha wanakuwa na mikakati wa kuwa na madaktari bingwa katika kila wilaya ili kuziba pengo hilo .

Mkuu wa  mkoa wa Arusha ,John Mongela  akisikiliza maelezo  katika moja ya banda la maonyesho katika mkutano wa  TAUS jijini Arusha.

Awali akifungua kongamano hilo ,Mkuu wa Mkoa wa Arusha,John Mongela amesema uwepo wa hama hicho utasaidia sana kutoa elimu kwa jamii juu ya changamoto hizo na kuweza kuwaona wataalamu mapema na hivyo kupunguza ukubwa wa tatizo.

Naye Katibu mkuu wa TAUS ,Dokta Deogratius Mahenda amesema kuwa, watu wenye umri kuanzia miaka 50 na kuendelea ndio wanakabiliwa na changamoto ya matatizo ya mfumo wa mkojo na uzazi na hiyo ni kutokana na wengi wao kutokuwa na elimu ya kutosha na kuweza kuwahi kwa wataalamu kabla ya tatizo hilo kuwa kubwa zaidi.

Dokta Mahenda amesema kuwa, kwa kipindi hiki elimu inaendelea kutolewa na kusaidia wananchi wengi kufika vituo vya afya na kupata huduma na kuongeza uelewa zaidi kwa wananchi hao.

Katibu Mkuu wa TAUS Dk.Deogratius Mahenda akizungumza na waandishi wa  habari jijini Arusha 

Amesema kuwa, wamejipanga kuhakikisha wanatoa elimu zaidi kwa jamii ili kuhakikisha wanakuwa na uelewa wa kutosha katika maswala hayo ili kuweza kupata matibabu mapema na kupata ushauri wa kutosha kutoka kwa wataalamu kabla tatizo halijawa kubwa zaidi.

Naye Daktari bingwa wa upasuaji katika mfumo wa mkojo , uzazi kwa wanaume na upandikizaji wa figo,Dk Victor Sensa amesema kuwa , wamejipanga kuhakikisha wanahamasisha vijana wengi waliopo vyuoni wanajiunga na fani hiyo,huku wakiiomba serikali iwanunulie vifaa kwani viliyopo ni vichache havitoshi ,hivyo iongeze nguvu kwenye ununuzi wa vifaa katika fani hiyo.