……………………………………………………………

Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii  inatarajia kuongeza wanyama jamii ya Simba, Chui, fisi,mbuni,kobe na mamba katika bustani ya asili ya Luhira Manispaa ya Songea.

Antony Masebe ni Kamanda wa  Kituo Kidogo cha Kanda Kusini Mashariki amesema utengenezaji wa vibanda maalum vya kuwahifadhi Wanyama hao (cages) na vyoo vya kisasa unaogharimu shilingi milioni 78 unaendelea katika bustani ya Luhira.

Msitu wa asili katika bustani ya asili ya Luhira yenye ukubwa wa hekta 600 ikiwa umbali wa kilometa saba kutoka Songea mjini

Amesema kituo hicho ambacho kipo chini ya TAWA kinasimamia bustani ya asili ya Luhira ambayo ilianzishwa mwaka 1973 na imekuwa inapokea watalii wa aina mbalimbali kutoka ndani ya nje ya nchi.

“Bustani ya Luhira imekuwa inatoa elimu na kuwasaidia wanafunzi kuanzia shule za msingi,sekondari na vyuo kuweza kujipatia maarifa tofauti kuhusu utalii ’’,alisisitiza Masebe.

Daudi Tesha ni Afisa Mhifadhi katika Bustani ya Luhira ameitaja bustani  hiyo kuwa ndiyo bustani pekee Tanzania yenye uoto wa asili ikiwa na ukubwa wa hekta 600 ipo umbali wa kilometa saba kutoka mjini Songea.

Amewataja Wanyama ambao wanapatikana katika bustani hiyo kuwa ni pundamilia, pofu, kakakuona, kuro, swalapala, sungura,nyumbu,jamii ya nyani ambapo amesema bustani hiyo ina madhari ya kuvutia ikiwemo maeneo ya michezo ya Watoto,maeneo mazuri ya kupigia picha na kuweka kambi kwa ajili ya utafiti.

Amekitaja kiingilio cha bustani hiyo kuwa ni shilingi 2,360 kwa mtu  wa kuanzia umri wa miaka 18,chini ya miaka 17 ni shilingi 1180 na  kwa Watoto chini ya miaka mitano wanaingia bure hivyo ametoa rai kwa wakazi wa Mkoa wa Ruvuma na watanzania wote kutembelea bustani hiyo asili.

Kamanda wa Kituo Kidogo cha Kanda ya Kusini Mashariki Songea Antony Masebe akizungumzia uboreshaji wa bustani ya Luhira iliyopo Manispaa ya Songea iliyoanzishwa mwaka 1973 

Amesema bustani ya Luhira imeweka mkakati wa kuwa na aina mbili za makazi ya Wanyama wakiwemo Wanyama huru kama pundamilia na pofu na kwamba hivi sasa wanatarajia kuongeza Wanyama wanaishi kwenye vizuizi yaani cages  ambapo mpango uliopo ni kuleta Wanyama wanaovutia wengi kama mfalme wa msituni  simba na chui.

“Hifadhi ya Luhira ina eneo kubwa, ambalo linahitaji uwekezaji mkubwa,tunafikiria kuwaleta wanyama wakubwa kama  simba na kuongeza maeneo ya kuvutia wageni wanapokuwa ndani ya bustani ya Luhira’’,amesisitiza Tesha.

Ameitaja mikakati mingine ya kuboresha bustani hiyo kuwa ni kuanzisha michezo ya kutekeleza kwenye waya (Zipline) kama inavyofanyika katika nchi ya Afrika ya Kusini,kuweka bwawa la kisasa la kuogelea na kuboresha eneo maalum la kupigia picha.

Amesema baada ya kuoresha bustani hiyo na kuongeza vivuito wanatarajia pia idadi ya watalii kutoka ndani na nje pia itaongezeka.

Ametoa rai kwa wakazi wa Mkoa wa Ruvuma na mikoa ya kusini kufika katika hifadhi ya Luhira kujionea fursa za utalii zilizopo katika hifadhi hiyo  pekee ya asili nchini Tanzania iliyopo mjini Songea.

Tesha amesisitiza kuwa hifadhi ya Luhira ni eneo la asili lenye utajiri wa miti ya miyombo, misuku, mitumbitumbi, miwanga, minyonyo, mizambarau, mininga, na mikuyu,na kwamba ni miongoni mwa bustani chache zenye uoto wa asili kabisa zilizopo mjini. 

Afisa Mhifadhi Bustani ya Luhira Daudi Tesha akizungumzia vivutio vya utalii vilivyopo katika bustani ya Luhira na mpango mkakati wa kuongeza vivutio vingine vya utalii ili kuongeza idadi ya watalii wa ndani na nje

Amesema ndani ya Luhira,mtalii anaweza kufanya utalii wa kutembea kwa miguu,kupiga picha,kuangalia wanyama na ndege,utalii wa kuweka kambi(camping) na kwamba mapumziko ya mchana(picnic) hufanyika ndani ya eneo maalum katika bustani hiyo.

“Watalii kutoka nje ya nchi pia wanatembelea hifadhi yetu, tumepokea watalii toka Ujerumani,Afrika ya Kusini, India, Marekani, Ufaransa,Italia, Uholanzi na wageni toka mikoa mbalimbali nchini,wanafanya utalii wa kuchunguza aina ya mimea na ndege’’,alisema Tesha.

Hifadhi ya asili ya Ruhila,inafikika kwa urahisi kwa ndege au kutumia barabara ya Njombe hadi Songea,Mtwara hadi Songea ambayo ni ya lami.

Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Mkoa wa Ruvuma

By Jamhuri