Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ni taasisi ya Serikali iliyoanzishwa chini ya Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania Na.12 ya 2003, na kupewa jukumu la kusimamia Sekta ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta nchini Tanzania. 

TCRA imebaini kuwepo kwa makampuni na watu binafsi wanaofanya biashara ya kutoa huduma za televisheni kupitia satelaiti bila kuwa na leseni halali pamoja na uingizaji wa vifaa vya mawasiliano, ikijumuisha visimbuzi vya Canal Plus na vifaa vingine vinavyofanana na hivyo ambavyo havijaidhinishwa na TCRA. 

Kwa mujibu wa Kifungu cha 23 (1) (b) na (c) cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022, ikisomwa pamoja na kanuni ya 40 (a) ya Kanuni za Leseni za 2018 zinaelekeza wasambazaji wa vifaa vya kieletroniki kuwa na leseni. Pia kifungu cha 83(1) cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta kinaelezea umuhimu wa vifaa vya kieletroniki vinavyoingia nchini kuidhinishwa na TCRA kabla havijaanza kutumika. 

TCRA, inautaarifu Umma na wafanyabiashara wote wanaofanya biashara ya huduma za televisheni kupitia satelaiti bila kuwa na leseni halali pamoja na wanaoingiza nchini vifaa vya mawasiliano, ikijumuisha visimbuzi vya Canal Plus na vifaa vingine vinavyofanana na hivyo ambavyo havijaidhinishwa na TCRA kuacha mara moja kufanya hivyo na badala yake kufuata utaratibu wa kupata leseni. 

Kwa atakayeshindwa kutekeleza ilani hii, TCRA itachukua hatua za kisheria na za kiudhibiti bila kutoa taarifa nyingine. 

IMETOLEWA NA 

MKURUGENZI MKUU 

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA 

30 Desemba 2022

By Jamhuri