WENYEJI, Simba SC wamefunga mwaka vizuri baada ya ushindi wa mabao 7-1 dhidi ya Tanzania Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara leo Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.

Mshambuliaji na Nahodha, John Bocco amefunga mabao matatu dakika za 12, 46 na 62 wakati akichezea kwa mara ya kwanza timu yake mpya, kiungo Mrundi Saido Ntibanzokiza pia amefunga mabao matatu dakika za 60, 63 na lingine limewekwa nyavuni na Shomari Kapombe dakika ya 88.

Ushindi huo unaoifanya Simba ifikishe pointi 44 katika mchezo wa 19, ingawa inabaki nafasi ya pili ikizidiwa pointi tatu na mabingwa watetezi, Yanga SC.
Kwa Tanzania Prisons ambayo bao lake limefungwa na Jeremiah Juma dakika ya 29 baada ya kichapo kikali cha leo inabaki na pointi zake 21 za mechi 19 nafasi ya 11.

Mechi nyingine Singida Big Stars imeutumia vyema uwanja wake wa CCM Liti mjini Singida baada ya kuichapa mabao 2-1 Geita Gold FC na kufikisha Pointi 37 nafasi ya nne huku Geita Gold FC wakibaki nafasi ya saba wakiwa na Pointi zao 24.

Ligi hiyo itaendelea kesho kwa Mechi mbili kupigwa katika Viwanja tofauti, vinara Yanga SC watakuwa ugenini kucheza na Mtibwa Sugar uwanja wa Manungu Complex na Azam FC atakuwa katika uwanja wake wa Chamazi Complex kucheza na Mbeya City kutoka jijini Mbeya majira ya saa moja usiku.

By Jamhuri