Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),Deodatus Balile, amesema mchakato wa mabadiliko ya sheria ya habari una matumaini chanya baada ya Serikali kuchukua hatua na kuhakikisha kukamilisha mchakato huo.

Balile amesema kuwa kwa hatua hiyo wadau wa habari nchini wanasubiri kwa matumaini mabadiliko sheria ya habari nchini.

‘‘Kwa hakika sisi kama wadau wa habari tumefika hatua nzuri n ahata kuwa na matumaini chanya hasa baada ya kikao cha mwisho kati ya wanahabari na serikali.

“Wakati unaofuata ni wa serikali na hatua zake katika kuelekea mabadiliko sheria ya habari., lakini mpaka hapa tulipofika, tunaamini kuna jambo linakwenda kutokea,’’ amesema.

Amesema, jambo linalofurahisha zaidi ni ushirikishwaji wa taasisi zote za habari nchini katika mchakato wa mabadiliko ya sheria ya habari.

“Kwa kuwa wadau wa habari tunapigania kitu kimoja, tuliamua kwa pamoja kujiweka chini ya mwavuli tunaouita CoRI (Wadau wa Kupata Habari).

“Jambo hili limerahisisha kuwa na sauti moja lakini pia limerahisisha serikali kujua wanazungumza na watu gani. Tusingekuw Pamoja pengine mambo yasingekwenda kwa namna tulivyoona,” amesema Balile.

Zinazohusiana

  –‘Sheria inakwaza vyombo vya habari na kuzidi kusinyaa’

‘Vyombo vya habari vinahitaji sheria rafiki’

Hivi karibuni, Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari amewahakikishia wadau wa habari kwamba, serikali itakamilisha mchakato wa mabadiliko ya vipengele vya sheria ya habari.

Alitoa kauli hiyo kwenye kikao chake na wadau wa Haki ya Kupata Habari (CoRI), Novemba 21,2022, jijini Dar es Salaam.

Nape amesema,Serikali imepokea maoni yao kuhusu mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari Na 12 ya 2016.

” Niwahakikishie kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, inayo nia ya dhati katika jambo hili. Nimekuja mwenyewe kuwasilikiliza na imani yangu ni kuona sekta inaendelea kukua” amesema.

Miongoni mwa mapendekezo ya CoRI kwa serikali ni pamoja na mamlaka haya ya Mkurugenzi wa Habari (MAELEZO) yafutwe na kiundwe chombo ambacho pamoja na mambo mengine, kitashughulikia masuala ya usuluhishi yanapotolewa malalamiko dhidi ya chombo cha habari, badala ya kazi hiyo kufanywa na mtu mmoja.

Wadau wanataka marekebisho dhidi ya kifungu cha 6 (e) kinachoelekeza magazeti kupatiwa leseni badala ya usajili wa moja kwa moja.

Pia wadau hao wanapendekeza magazeti yasiendeshwe kwa kupewa leseni, badala yake yapewe usajili wa kudumu au wa muda mrefu, ili kudhibiti changamoto ya ufutwaji holela wa leseni na kuvutia wawekezaji.