Wagonjwa 105 wagundulika kuwa na maambukizi ya COVID-19 Tanzania

Mtaalam na mbobezi wa masuala ya chanjo kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), Dkt.Caroline Akim amesema hadi kufikia Novemba 25 ,mwaka huu,Tanzania ilikuwa na wagonjwa wapya 105 waliogundulika na maambukizi ya Covid19.

Ameeleza kundi la vijana wengi wao hawajachanja kwa dhana potofu kuwa hawapo katika hatari ya kupata ugonjwa huo.

Akitoa somo kwa waandishi wa habari mkoani Pwani, Akim ameeleza silaha ni kuchanja kwani Covid-19 bado haina tiba.

Mtaalam huyo mbobezi wa masuala ya chanjo kwa takriban miaka 30 duniani ,alitaja Tanzania imefikia asilimia 92 ya utoaji wa chanjo ya UVIKO-19, huku Mkoa wa Pwani ukiwa na asilimia 63 na ni mkoa wa tatu kutoka mwisho kwa takwimu za utoaji chanjo.

Akim amesema Watanzania wasijisahau kuona ugonjwa umekwisha bali waendelee kujilinda pamoja na wale ambao hadi sasa hawajapata chanjo waone umuhimu wa kuchanja .

Hata hivyo ameeleza ,tangu kugundulika kwa ugonjwa huo Tanzania wagonjwa waliogundulika kuwa na ugonjwa huo ni 38,205, vifo 845 kati ya hao 3,409 walikuwa watalaamu wa afya na kwamba chanjo milion 28.4 zimetolewa.

Akim ameeleza, takwimu za dunia wagonjwa wa UVIKO-19 ni miln 6.3, vifo 6.6 chanjo zilizotolewa ni biln 12.9 na kwa Afrika miln 9.3 .

“Changamoto ya vijana kutojitokeza ni tatizo la dunia nzima ,na kundi hili ndilo lenye mizunguko , ni rahisi zaidi kueneza ugonjwa kutokana na kuwa na mizunguko na shughuli za mihangaiko ,hivyo hawana budi kujitokeza “
Kundi hili ni miongoni mwa makundi yaliyo kwenye hatari ya kupata ugonjwa huo , wakiwemo vijana, wajawazito,wanaonyonyesha,wazee na wote wanatakiwa kujitokeza kupata chanjo” amesisitiza Akim.

Akim ameeleza, ili kuwezesha wananchi wengi kupata chanjo ya UVIKO-19 waandishi wanapaswa kuwakumbusha kushiriki katika kuhamasisha na kutoa taarifa sahihi ya ugonjwa .

“Waandishi mnatakiwa sasa kuwakumbusha wananchi umuhimu wa kuchanja lakini pia kuwaeleza faida zake ili kuepuka kuingia kwenye athari wanapopata ugonjwa huu”ameeleza Akim.

Nae Mratibu wa Chanjo mkoa wa Pwani Dk Abbas Hincha ameeleza kwamba, wanatarajia kuanza kampeni ya nyumba kwa nyumba ya chanjo ya UVIKO-19 ili kuwafikia wananchi walioko nyumbani ambao bado hawajapata chanjo.

Amesema Mkoa huo unatarajia hadi kufikia Desemba 30, mwaka huu, kuwafikia wananchi 757,465 na kwamba hadi kufikia Novemba 22, mwaka huu, walengwa 468,187 tayari wamepata chanjo sawa na asilimia 63.